MIZENGWE inayoashiria kuwapo kwa wingu la rushwa, imeanza kujidhihirisha ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati kikielekea kuhitimisha harakati za uchaguzi baadaye mwaka huu.
Hali hiyo imefikia hatua ya kumfanya Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba, kutoa tahadhari kuwa chama hakitasita kuliondoa katika orodha ya wagombea jina la mwanachama yeyote atakayebainika kujihusisha na rushwa na kampeni chafu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam jana, Makamba alisema kuwa CCM itawachukulia hatua kali, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha katika Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU), wanachama wake watakaohisiwa kujihusisha na rushwa katika uchaguzi unaoendelea ndani ya chama hicho.
Aidha, chama hicho kimeonya kuwa mbali ya rushwa, kitawashughulikia pia wanachama wake watakaobainika kuendesha kampeni kinyume cha taratibu zilizoanishwa.
Mbali ya kuyafikisha majina ya watoa rushwa TAKURU, chama hicho pia kitayaondoa majina ya watu hao katika orodha ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama.
Kauli hiyo ya Makamba inakuja wakati tayari malalamiko yameanza kusikika kutoka katika maeneo mbalimbali nchini, kuhusiana na baadhi ya wagombea ambao wanatumia mbinu chafu, ikiwamo kutoa rushwa, ili kuvutia wapiga kura.
Sambamba na hatua hiyo, Makamba alisema pia kuwa majina hayo yatapelekwa TAKURU kwa ajili ya uchunguzi wa kina, na endapo itathibitika kuwa kuna tuhuma za rushwa, yatafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Makamba alisema hatua hiyo inalenga kuwaondoa katika harakati za kuwania uongozi watu wote wanaotumia rushwa kama silaha ya kampeni.
“Kama kuna mgombea ana mchezo mchafu kama huu, tukijua majina yao, tuko tayari kuyapeleka TAKURU ili hatua zinazofaa ziweza kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria zilizopo,” alisema Makamba.
Alisema mara zote CCM imekuwa mstari wa mbele kupiga vita rushwa na haiwezi kukubali kuona kuwa uchaguzi huo unatawaliwa na rushwa.
Alisema iwapo hali hiyo itaachiwa iendelee, kuna hatari chama hicho kikaongozwa na watoa rushwa.
“Endapo mtu amesikia jina la kigogo fulani anayejihusisha na vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili ya chama, aje kuniambia au alipeleke TAKURU ili liwe funzo kwa wengine,” alisema Makamba.
Akifafanua kuhusu kampeni kuendeshwa kinyume cha taratibu, Makamba alisema kwa mfano kuwa Ibara ya 33 (14) ya kanuni za uchaguzi za chama hicho, inamkataza mgombea yeyote kutengeneza fulana au vifaa vingine vya kampeni, kabla ya uchaguzi na kuzigawa.
Alisema endapo mgombea yeyote atabainika kufanya hivyo, adhabu ya kwanza atakayochukuliwa na chama ni kuondoa jina lake mara moja na hataruhusiwa kugombea ndani ya chama.
“Hata kama (mgombea) ni mkubwa kama tembo, hatutamuogopa, tutaliondoa jina lake na kumzuia kugombea,” alisisitiza Makamba.
Kuhusu nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania Bara ambayo imekuwa na mchuano mkali, Makamba alisema hadi sasa hakuna mvutano kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
“Nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara inayoshikiliwa na John Malecela haina tatizo kabisa, na ile ya Katibu Mkuu haina mvutano kama inavyodaiwa… chama chetu kinafuata kanuni ili kupata watu wanaofaa kushika nyadhifa hizo,” alisema Makamba.
Kuhusu madai kuwa hali si shwari ndani ya chama hicho, Makamba alisema hali ndani ya CCM ni shwari na hakuna tatizo lolote kama inavyodaiwa.
“Nimesoma gazeti moja la kila siku (si Tanzania Daima), linadai kuwa uchaguzi CCM ni fitina tupu, nani kasema? Hali ndani ya CCM ni shwari kabisa… na kwamba suala hili halina ukweli wowote,” alisema Makamba.
Kwa upande wa zoezi la uchaguzi wa ngazi za mashina, matawi na kata, Makamba alisema uchaguzi umeendelea vizuri licha ya dosari ndogo ndogo zilizojitokeza.
Alisema miongoni mwa dosari hizo, ni pamoja na baadhi ya wagombea katika kata za Kisutu na Kitunda kusimamishwa kugombea nafasi walizoomba kutokana na makosa mbalimbali yakiwamo ya vitendo vya rushwa.
Alisema mgombea wa Kitunda alikutwa na kosa la kuandaa wapiga kura bandia kwa kuwanunua wakati wa Kisutu alisimamishwa kutokana na kosa kama hilo.
Uchaguzi mkuu wa CCM umeshaanza na unatarajiwa kukamilika baadaye mwaka huu wakati mkutano mkuu wa chama hicho utakapowachagua viongozi wa kitaifa.
Leo ndiyo siku ya mwisho kwa wanachama wanaowania nafasi mbalimbali kuchukua na kurejesha fomu za kuomba kugombea.
Kauli hiyo ya Makamba inakuja siku chache tu baada ya chama hicho mkoani Ruvuma kuwafuta uanachama wanachama wake watano, akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Hatua hiyo imewafurahisha wanachama wa CCM katika Wilaya ya Njombe, mkoani Iringa, na kutuma salamu za pongezi kwa Halmashauri Kuu ya CCM, Mkoa wa Ruvuma kwa uamuzi huo.
Walisema uamuzi huo ni muafaka na unaostahili kuigwa na wenzao wa Njombe, kwa kumuadabisha aliyekuwa mbunge wa Njombe Magharibi, Thomas Nyimbo, anayedaiwa kuwatolea maneno ya kashfa madiwani.
Nyimbo anatuhumiwa kuwaita madiwani hao kuwa ni wahuni.
“Kauli kama hizi ni moja ya vigezo vilivyopaswa kufanyiwa kazi na halmashauri kuu ya CCM ya mkoa, kwa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya Nyimbo,” alisema Said Bangu.
Awali, Katibu wa madiwani katika Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo ya Njombe, John Mwandoloma, alionya kwamba madiwani watalazimika kuchukua hatua kali dhidi ya Nyimbo, ikiwa CCM haitaliona hilo kama kosa.
Hata hivyo, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Njombe, Mpagiki, alisema kwamba CCM haina nia ya kumfichia madhambi Nyimbo, na kuwataka madiwani wenye uhakika na suala hilo kuwasilisha malalamiko yao haraka.
Hata hivyo, wanachama hao wamehoji uhalali wa Nyimbo aliyewaita viongozi wa CCM wahuni kuamua kuchukua fomu kugombea nafasi ya mwenyekiti wa mkoa.
“Ni kweli alisema kwamba CCM ni wahuni, na kila mtu anayekutana naye hapa Makambako, Njombe, Ilembula, Wanging’ombe na mahala pengine popote pale, husema wazi kwamba CCM ni wahuni,” alisema Jeremia Sawala.
Sawala alisema ameamua kuwasilisha pingamizi binafsi kwa CCM mkoa ili jina la Nyimbo, liondolewe katika kinyang’anyiro hicho kutokana na kauli zake dhidi ya viongozi wa chama hicho.
“Nimetuma barua kwa Katibu wa CCM mkoa kuhusu suala la Nyimbo, nimemuwekea pingamizi kwamba hastahili kuingia katika mchakato huo, si kwa malengo ya kuwasaidia wagombea wengine, bali ni kwa ajili ya kutetea maadili na kanuni za chama,” alisema Sawala.
Wakati huohuo, orodha ya wana CCM wanaowania uongozi iliongezeka jana baada ya Mbunge wa Maswa, John Shibuba, Mhariri wa Habari wa gazeti la Mtanzania, Manyerere Jackton, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Naibu Waziri wa Fedha wa zamani na Mbunge wa Magu, Festus Limbu, kuchukua fomu kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC).
Wengine waliochukua fomu jana ni Tambwe Hiza, mmoja wa wana CCM aliyepata umaarufu baada ya kujiunga na chama hicho akitokea Chama cha Wananchi (CUF), pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communications, Ali Mwambola.
Akizungumza wakati wa kuchukua fomu, Shibuda, ambaye aliwahi kuwania urais mwaka 2005, aliwaponda wanachama wa CCM ambao wametoka upinzani na kudai kuwa hawawezi kuwa viongozi wa CCM bila kupitia chuoni.
“Mtu hawezi kuwa sheikh bila kupitia madrasa, aidha mtu hawezi kuwa askofu bila kupitia chuoni, seminari. Hivyo hivyo deni la kuwa NEC ndani ya CCM ni la wana CCM wanaotokana na malezi ya chama, si mtu akisilimu au kubatizwa anakuwa sheikh au paroko wa kanisa,” alisema Shibuda.
Kujitokeza kwa wanachama wengi katika uchukuaji wa fomu hizo katika Mkoa wa Dar es Salaam kumefanya idadi ya watu waliochukua fomu katika kuwania nafasi mbalimbali kufika 313.