Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Joto urais Zanzibar lafukuta
Joto urais Zanzibar lafukuta
By Habari Tanzania | Published  06/3/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu, Zanzibar


KAMPENI za kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar mwaka 2010 zimechukua sura mpya na kuna uwezekano mkubwa mgombea wa CCM kwa mara ya kwanza kutokea Kisiwa cha Pemba.

Uwezekano huo umeanza kujitokeza kutokana na kundi lililokuwa likitegemewa kutoa mgombea kugawanyika, ikiwa imebakia takriban miaka miwili na nusu kabla ya Rais Karume kumaliza muda wake.

Kundi hilo ambalo lilikuwa likiongozwa na Dk. Salmin Amour na kumtetea mgombea wake, Dk. Mohammed Gharib Bilal, limegawanyika na kuanza kupoteza nguvu za kisiasa na kutoa mwanya kwa uwezekano wa mgombea huyo kutoka Pemba.

Taarifa zaidi zinasema kuwa uamuzi wa Rais Karume kuwateua baadhi ya wajumbe wa kundi hilo na kuwaingiza katika serikali yake ya awamu ya sita ndio ulikuwa mwanzo wa kuanguka kwa kundi hilo kisiasa.

Baadhi ya wanachama wa CCM walisema kwamba vigogo aliowachukua Rais Karume walikuwa na nguvu ya kisiasa na tegemeo la kambi hiyo, lakini sasa wamepoteza uaminifu wa kisiasa.

Vigogo aliowabeba Rais Karume ambao walikuwa watu wa karibu na Dk. Salmin ni aliyekuwa Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Kiongozi, Amina Salum Ali na Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamuhuna.

Wengine ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Hassan Mussa Takrima ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi, pamoja na Ali Ameir Mohammed, ambaye amewekwa Mshauri wa Rais Karume, Mambo ya Siasa.

Uchunguzi wa Tanzania Daima umegundua hadi sasa wagombea wawili kutoka kisiwani Pemba wapo katika maandalizi ya kuwania nafasi hiyo na kufanyika kampeni za chini kwa chini kupitia wanachama maarufu wa CCM kwa jina la wapambe, wakisukumwa na siasa za Tanzania Bara.

Habari za ndani zilizopatikana zimesema kwamba hadi sasa kiongozi mmoja wa juu katika Serikali ya Zanzibar anafanya kampeni za kuhakikisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Ali Mohamed Shein, anagombea nafasi hiyo mwaka 2010 kwa kuamini kwamba ni mwanasiasa aliyekomaa, mkimya na mwenye utulivu wa kisiasa.

Hata hivyo baadhi ya wanachama wa CCM Unguja na Pemba wamekuwa wakitoa upinzani wa chini kwa chini wakidai kwamba Dk. Shein bado hajajiimarisha kwa siasa za Zanzibar, pamoja na kukaa katika nafasi ya umakamu wa Rais kwa vipindi viwili.

Kutokana na watu hao kubeba nguvu kubwa za kisiasa Zanzibar, ndiyo maana baadhi ya wana CCM wanasema kuna uwezekano mkubwa kwa Pemba kuandika historia mpya.

Wanachama hao wa CCM mbali na kuendeleza kampeni za chini kwa chini dhidi ya Dk. Shein kutokana na matakwa ya kiongozi mmoja wa juu, kundi jingine linaonekana kumuunga mkono Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Mohammed Aboud, ambaye pia ni kutoka kisiwani Pemba.

“Tunazo taarifa kuwa Dk. Shein ndiye anayetakiwa na Rais Karume, lakini kwa siasa za Zanzibar, bado hana mizizi ya kisiasa, hasa kisiwani Pemba, ndiyo maana tunasema afadhali aandaliwe Naibu Waziri wa Usalama wa Raia kama lengo ni rais kutoka Pemba,” alisema mjumbe mmoja wa NEC kutoka Unguja.

Alisema kwamba kuwa na mgombea anayetokana na utashi wa kiongozi anayeondoka madarakani ni hatari na kunaweza kusababisha kiongozi huyo kulinda udhaifu uliojitokeza kabla ya kutokea mabadiliko ya uongozi.

Taarifa zaidi zinasema kwamba misimamo ya Dk. Bilal katika kutetea misingi ya utawala bora na demokrasia inawatia wasi wasi wanasiasa wengi waliopo madarakani, kwamba huenda itawaweka katika nafasi ngumu, licha ya kwamba anaungwa mkono na wana CCM walio wengi.

Hata hivyo, kundi la Dk. Bilal bado lina matumaini makubwa kama atajitokeza tena kuwania nafasi hiyo, kutokana na uungwana aliouonyesha baada ya kukubali kuondoa jina lake usiku wa kuamkia uchaguzi wa mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM mwaka 2005.

Baadhi ya makada wa CCM Unguja na Pemba wamesema kwamba kitendo cha Dk. Bilal kuongoza katika kura za maoni Zanzibar mwaka 2000 na jina lake kutozingatiwa na vikao vya juu vya chama huko Dodoma kulionyesha kukomaa kisiasa, na kile kitendo cha kutakiwa kuondoa jina mwaka 2005.

Wanachama wengine wa CCM wanasema kwamba kwa itifaki ya uongozi haijawahi kutokea mtu kushika nafasi ya Uwaziri Kiongozi na baadaye akaja kuwa Rais wa Zanzibar, hivyo nafasi kubwa inatolewa kwa wagombea kutoka kisiwani Pemba.

Aidha, hatua ya kutoa mgombea kisiwani humo pia inachukuliwa kuwa itawezesha kuipunguza nguvu ngome ya CUF, ambayo imekuwa ikitumia ajenda ya kutopatikana rais kutoka Pemba tangu mapinduzi ya mwaka 1964.

Wanaharakati wa kampeni za kuwania urais hadi hivi sasa wamekuwa wakijipenyenza kwa wanachama wa CCM wa mikoa mitano, kila upande ukijaribu kuimarisha mizizi ya kisiasa kwa kutumia mikusanyiko ya kijamii kama vile maziko, harusi na maulidi.

Kundi la wanachama wanaomtaka Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, linasema kwamba Aboud hana makundi, ya mikoa kama walivyo wagombea wengine.

Hadi sasa wana CCM wengine wanaotajwa kuwa na nia ya kuwania nafasi hiyo ya urais ni Dk. Hussein Mwinyi, ambaye hatua ya kuhamia kugombea ubunge katika Jimbo la Kwahani, Unguja kutoka Mkuranga, kumeelezwa ni moja ya hatua ya kumjenga kisiasa na kumuandaa kwa nafasi hiyo.

Hata hivyo wana CCM wanasema kwamba karata alizozichanga hazikusoma nyakati za kisiasa kwa vile hali hiyo haitakuwa sura nzuri, anayetoka madarakani ni mtoto wa rais na anayeingia pia ni mtoto wa rais.

“Kama itakuwa hivyo, basi itakuwa sawa na kukaribisha utawala wa kisultani kwa mlango wa nyuma,” alisema ofisa mwandamizi mmoja kutoka Makao Makuu ya CCM Unguja.

Pamoja na nafasi hiyo kuwa ni kubwa kutoka Pemba, kundi la wanachama wa CCM kutoka Mkoa wa Kusini Unguja wamekuwa wakimnadi chini kwa chini Waziri wa Habari wa Serikali ya Muungano anayeshughulikia Habari na Michezo, Muhammed Seif Khatib, pamoja na Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha.

Wana CCM hao wanadai kuwa, Khatib ni kiongozi anayezijua siasa za Zanzibar na Muungano na amepikwa ndani ya chama kwa muda wa kutosha.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Rais Karume anamaliza muda wake mwaka 2010.

Hata hivyo, hivi karibuni, Rais Karume alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wa Zanzibar kuwa ni mapema kufanya harakati za kugombea urais wakati muda wake ukiwa bado.

Rais Karume aliingia madarakani mwaka 2000, baada ya kuwaangusha washindani wake katika vikao vya chama ambao waliongoza katika kura za maoni Zanzibar.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.