WABUNGE watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa wilaya za Ulanga na Kilombero, wanatarajiwa kushitakiwa kwenye Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC), wakidaiwa kushindwa kutekeleza ilani ya uchaguzi.
Wabunge hao na majimbo yao kwenye mabano ni Dk. Juma Ngasongwa, (Ulanga Magharibi), Celina Kombani (Ulanga Mashariki) na Gastor Ligalama (Kilombero).
Hatua ya wana CCM hao kuwashitaki wabunge wao ambao pia ni mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, ni kutokana kulalamikiwa kushindwa kusimamia miradi na kudorora kwa maendeleo katika majimbo hayo.
Dk. Ngasongwa ni Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, wakati Kombani ni Naibu Waziri Ofisi wa Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Hata hivyo, wabunge hao kwa nyakati tofauti wamekanusha madai yanayotolewa dhidi yao wakidai CCM wilaya za Ulanga na Kilombero inajua fika wajibu wao, jinsi wanavyosimamia na kutekeleza ilani ya uchaguzi.
Kombani alisema kwamba suala la utekelezaji wa ilani ya CCM si la mbunge pekee, bali kila mtu linamhusu, lakini kwa kiasi kikubwa amejitahidi kufanya.
“Sitaweza kusema mengi, kwani nipo barabarani, lakini nimefanya kwa kiasi changu, itakuwa vema kama wanaolalamika wakatoa ufafanuzi hata katika mazingira niliyofanya vyema,” alisema naibu waziri huyo.
Dk. Ngasongwa kwa upande wake alisema hayo ni mambo ya kawaida wakati wa uchaguzi, ambapo baadhi ya watu huibua hoja kali dhidi ya wabunge.
“Mimi nimekuwa kiongozi wa CCM si kwa Wilaya ya Ulanga pekee, bali hata kuwakilisha mkoa mzima, ninaelewa vema malalamiko haya yanatokea wapi,” alisema Dk. Ngasongwa.
Hata hivyo, akiri kwamba hali ya mambo si shwari katika jimbo lake la uchaguzi, lakini tayari maofisa wa TANROADS wameahidi kuzifanyia ukarabati barabara hizo.
“Si kwamba hatutaki kutekeleza ilani ya uchaguzi, bali kuna kila namna ya kufikia hatua moja na nyingine ya utekelezaji, sisi kama wanasiasa na wenzetu wataalamu tunategemeana,” alisema Dk. Ngasongwa.
Waziri huyo mkongwe alikanusha vikali habari za wanachama hao kwamba wanapaswa kupigwa chini kwa vile wameonekana kutowiana na falsafa ya Rais Jakaya Kikwete, ya Ari, Kasi na Nguvu Mpya.
“Si kweli kama tumeshindwa kufanya kazi, lakini kila mtu anaona jinsi tunavyohangaikia maendeleo ya watu wetu, kwa maana ya Ulanga kama wilaya na pengine mkoa mzima,” alisema Dk. Ngasongwa.
Ligalama, hakuweza kupatikana kuzungumzia sakata hilo, lakini baadhi ya wasaidizi wake walidai kwamba amekuwa mwoga kukutana na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi wa hali ya maendeleo ya jimbo lake.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wana CCM walidai kwamba wabunge wa majimbo hayo ni mzigo kwa maendeleo yao.
Wanachama hao wamelalamikia fedha zilizotolewa na Serikali ya Afrika Kusini chini ya Rais mstaafu wa nchi hiyo, Nelson Mandela, ambazo zilipaswa kutengeneza barabara kuanzia Mikumi hadi Mahenge kwa kiwango cha lami.
“Walikutana katika vikao vyao na kukubaliana kuifanyia matengenezo barabara hiyo kuanzia Mikumi mpaka Mkamba, lakini sehemu nyingine zimeachwa kama zilivyo, na Dk. Ngasongwa akiwa mjumbe katika vikao hivyo kila wakati,” alisema Juma Shame.
Shame alidai kuwa mazingira ya maisha katika ukanda huo hayakupaswa kuwa magumu kama yalivyo sasa ambapo kiasi kikubwa cha vijana wameamua kujiingiza katika ujambazi na ujangili wa wanyamapori kwenye hifadhi.
“Ni matokeo mabaya ya kuwa na wabunge wanaopita kutokana na ujanja ujanja, au kwa mazingira ya rushwa wakati wa uchaguzi, lakini kama ni uamuzi wa wananchi, wabunge hawa wote hawawezi kupata nafasi,” alisema Shame, mkazi wa Malinyi.
Alisema inasikitisha kuona barabara ya Malinyi, Lupilo si zaidi ya kilomita 50, lakini wanapata shida hasa pale inapojitokeza kwamba kuna mgonjwa anatakiwa kukimbizwa katika Hospitali ya St. Francis, Ifakara.
Alisema ubovu wa barabara hiyo umesababisha wenye magari kusitisha huduma za usafiri, na kuwa hivi sasa magari yanayofanya safari hiyo ni ya mizigo ambayo hutumia saa kati ya 7 hadi 8 kufika Ifakara.
Yahaya Semi, na Jordan Kwayeta, wakazi wa vijiji vya Utete katika Tarafa ya Mtimbira, jimbo la Dk. Ngasongwa, walidai kuwa hali ya barabara hiyo na huduma nyingine za kijamii katika maeneo yao ni mbaya sana.
Semi alisema kwamba mtu anayetoka Malinyi hulazimika kutumia zaidi ya saa kati ya tano na sita, kufika njia panda ya Mahenge, eneo la Tarafa ya Lupilo.
Aliongeza kwamba wakati hali ikiwa hivyo, mbunge wao ameendelea kubaki jijini Dar es Salaam, na kama akifika jimboni humo hukutana na baadhi ya madiwani kwa siri ambapo hupewa maelezo kwamba miradi mbalimbali ya maendeleo inaendelea vema.
Kwa upande mwingine wananchi wa vijiji katika Tarafa ya Mwaya, Jimbo la Mashariki walimlalamikia mbunge wao kushindwa kutekeleza ilani hiyo ya uchaguzi ya CCM.
“Akija huku, amekuwa akikutana na madiwani kwa siri, mambo yanayozungumzwa hakuna mtu wa kawaida anayefahamu,” alisema Ismail Jumanne.
Jumanne alisema kuwa matatizo yanayowakabili wananchi katika majimbo mawili ya Wilaya ya Ulanga yamesababishwa na viongozi hao.
“Mifumo ya barabara zetu kutoka maeneo ya vijijini kuja Mahenge ni mibaya, haikubaliki hata kidogo, huku viongozi wetu wakijichimbia Dar es Salaam,” alisema Solomon Mkwaze.
Mkwaze alisema kwamba viongozi wa CCM ngazi za wilaya na mkoa ndio wanaostahili lawama za kupatikana viongozi wasiowajibika.
“Sisi wananchi tunaoshirikishwa katika uchaguzi, ndio tunaopata shida sasa, kwani badala ya kuja kusikiliza kero hutumia muda wao kuwasiliana kwa simu,” alisema Mkwaze.
Katika Jimbo la Kilombero, wanachama hao wamekiomba chama hicho kuifanyia mabadiliko katiba iweze kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi pindi wananchi wakibaini mbunge hawezi kazi.
Mbunge wetu amedhihirisha kwamba ameshindwa kufanya kazi, kwa misingi ya kutekeleza ilani ya chama ya uchaguzi, ambayo pia ilipaswa yeye kuilinda na kuitetea,” alisema John Katane.
Katane alilalamikia hali hiyo huku akidai katika vipindi ambavyo jimbo limebahatika kufanya vibaya, basi ni katika hatua ya mbunge aliyepo hivi sasa, kwani tangu amechaguliwa hataki kukutana na wananchi kueleza mipango yake ya maendeleo.
Wanachama hao walimlalamikia mbunge wao Ligalama, kwa kushindwa kuonyesha nia ya wazi kuwasaidia watu wake, hasa katika mazingira mabaya ya miundombinu.
“Ukiachilia mbali barabara inayoanzia Mkamba, ambayo kila mbunge anadai ni mali ya Tanroads, ile ya Ifakara, Mlimba, haijafanyiwa kazi kwa muda mrefu, wakati aliahidi kuifanyia kazi baada ya uchanguzi,” alisema Sharifa Juma.
Sharifa, mkazi wa Ifakara mjini alisema wanawake wilayani Kilombero hivi sasa wamekuwa wakilalamikia ubovu wa barabara hizo, kwani zimeanza kusababisha madhara makubwa kwao, hasa wanapotakiwa kuwahishwa hospitali kwa ajili ya uzazi.
“Tangu Ligalama amechaguliwa kuwa mbunge wa Kilombero, ameshindwa kufanya mkutano na wananchi, kueleza mikakati yake ya kutekeleza ilani ya uchaguzi,” alisema.