Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mangula aitega CCM
Mangula aitega CCM
By Habari Tanzania | Published  06/3/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu


UAMUZI wa Katibu Mkuu wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Japhet Mangula, wa kujishusha hadi kuwania umakamu mwenyekiti wa mkoa, umeibua hisia nzito miongoni mwa Wana CCM.

Kwa kiasi kikubwa, Mangula mwenye uzoefu wa kukiongoza chama hicho, hakutarajiwa kuibuka tena kuutaka uongozi tangu awekwe kando mwaka jana na Mwenyekiti mpya wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Badala ya Mangula, Kikwete alimnyanyua Yusufu Rajab Makamba, kutoka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam hadi Katibu Mkuu wa Chama tawala, CCM. Hiyo ilikuja wiki moja baada ya kuteuliwa na Rais kuwa mbunge.

Lakini ghafla Mangula ameibuka, lakini katika nafasi ya chini, tofauti na aliyokuwa nayo, akiwania kuwa mwenyekiti wa CCM mkoani Iringa, nafasi inayoachwa na Tasili Mungwe’nywa Mgoda.

Mbali ya Mangula, aliyerudisha fomu rasmi jana, wengine anaochuana nao ni Mbunge wa Njombe, Thomas Nyimbo na Mahamod Mgimwa. Kama ilivyo kwa Mangula, Mgimwa naye amesharudisha fomu.

Lakini uamuzi wa Mangula bado umeacha maswali mengi, hasa kwa wachambuzi wa masuala ya siasa za ndani ya CCM wanaotafakari ujasiri wa kiongozi huyo aliyeiwezesha CCM kutembea kifua mbele wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, kwani tayari ilikuwa na wanachama 3,200,000, kati yao viongozi wa mashina wakiwa 300,000 na chama kilikuwa na matawi zaidi ya 12,500 nchi nzima.

Kuna wanaojiuliza kama ni janja ya Mangula ya kutaka kuingia NEC kwa tiketi ya Mkoa wa Iringa, hasa baada ya kubaini kwamba, hana nafasi ya kuingia kwa urahisi katika NEC inayodhaniwa inawaniwa na ‘wanamtandao’ wengi.

Na ingekuwa aibu kubwa kwa katibu mkuu mstaafu kushindwa kuingia NEC kupitia kundi la Bara.

Itakumbukwa kwamba, Mangula, kwa nafasi yake ya katibu mkuu, aliingia kwenye kapu la NEC mwaka 2002. Wengine alioingia nao NEC kwa kundi la Bara mwaka huo na kutarajiwa kumaliza muda baadaye mwaka huu ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aliyetumbukiza tena kete yake baada ya kurejea kutoka masomoni Marekani, alikokwenda kusomea shahada ya uzamili katika masuala ya uongozi.

Pia wamo Jackson Msome, Edward Lowassa, ambaye kwa sasa ni Waziri Mkuu katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete, ambaye pia alikuwa katika kundi hili kabla ya kuunyakua Urais na Uenyekiti wa CCM, akirithi mikoba ya Benjamin Mkapa.

Wengine ni Abdulrahman Kinana, Kingunge Ngombale-Mwiru, Makamba, Brigedia Jenerali mstaafu Hassan Ngwilizi aliyekuwa msaidizi wa Mangula katika CCM.

Wengine ni Kapteni John Komba, Profesa Juma Athumani Kapuya, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ulinzi, Profesa Philemon Sarungi, Paul Kimiti, William Vangimembe Lukuvi, Dk. Masumbuko Lamwai, Charles Keenja, Isdore Shirima, Stephen Mashishanga na Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby.

Lakini hofu kubwa zaidi kwa ‘wanamtandao’ ndani ya chama tawala ni kwamba, huenda Mangula ametia mkono kupima fukuto ndani ya chama hicho, lakini akiwa na lengo jingine.

Inaelezwa kwamba, Mangula aliyeacha gumzo mwaka jana kutokana na kauli yake ya kukiri kwamba kuna makundi ndani ya CCM, huenda ni miongoni mwa Wana CCM walioamua kurejesha nguvu, lakini kwa staili nyingine ambayo bado inadaiwa kufanyiwa kazi.

“Si siri, ametikisa. Hatujui anafikiria nini…” kimeeleza chanzo chetu cha habari.

Lakini Mangula mwenyewe, akizungumza jana baada ya kurudisha fomu alisema kwamba, ni haki ya kila Mtanzania kuchagua na kuchaguliwa, na kuongeza kuwa kutokana na hali hiyo amesukumwa kuchukua fomu ya kuomba kuchaguliwa katika ngazi ya mkoa.

Alisema Watanzania wanatakiwa kumuenzi hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa kufanya kazi zinazoliletea manufaa taifa, na kuwa katika kumuenzi kwake akichaguliwa atafanya kazi bila kuchoka.

Mwanasiasa huyo aliyepikwa kisiasa katika nchi za kijamaa, kwa sasa ni mkulima anayeishi kijijini Kinenulo, wilayani ya Njombe, anakolima viazi mviringo katika ekari zaidi ya 30.

“Viongozi si wakae Dar es Salaam na kufungua NGO’s na kusahau kabisa kazi za kilimo. Wanatakiwa waende shambani kulima, ili kumuenzi Mwalimu Nyerere alichofanya baada ya kung’atuka,” alisema huku akisisitiza jinsi ya kujenga chama imara kuanzia ngazi za tawi, jambo ambalo amedai atalipa kipaumbele mkoani Iringa akichaguliwa kuwa mwenyekiti.

Shangwe Thani kutoka Shinyanga anaripoti kwamba; kinyang’anyiro cha kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa CCM mkoani Shinyanga na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), sasa kimechukua sura mpya baada ya wafanyabiashara maarufu mkoani humo na wanasiasa wakongwe kujitosa kugombea nafasi hizo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Chama Cha Mapinduzi mkoani hapa jana, mpaka jana asubuhi wanachama 19 wa chama hicho wamechukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa chama hicho ngazi ya mkoa na taifa.

Katibu wa CCM mkoani Shinyanga, Gustav Muba, aliwataja waliochukua fomu kuwa ni wakurugenzi wa makampuni mbalimbali yakiwamo ya ununuzi, uchambuzi na usafirishaji wa zao la pamba, wenyeviti wa zamani wa CCM wilaya, wabunge na naibu waziri mmoja.

Wanaogombea ujumbe wa NEC taifa kuwakilisha Mkoa wa Shinyanga ni Mkurugenzi wa makampuni ya Phantom, Hilal Hamad, Mkurugenzi wa makampuni ya Simon Agency, Robert Kisena na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Dk. Charles Mlingwa.

Muba alimtaja Mkurugenzi wa makampuni ya Mombasa Raha na Nchambi’s ambaye pia ni Mweka Hazina na Naibu Kamanda wa Vijana wa CCM Wilaya ya Kishapu, Suleiman Masoud ndiye mwanachama pekee aliyechukua fomu ya kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia kundi la vijana.

Alimtaja mwanamke pekee aliyejitokeza kuwania moja ya nafasi za uongozi katika kinyang’anyiro hicho kuwa ni mbunge wa zamani wa Viti Maalumu, Eisha Stima na wanaowania ujumbe wa NEC viti vya wote kuwa ni Masunga Lyabuyenze, Julius Maunde na Athanas Simon.Wanawaowania nafasi ya uenyekiti wa mkoa ni Diwani wa Kata ya Kilago na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama, mwenyekiti mstaafu wa Umoja wa Vijana wa CCM na mjumbe wa zamani wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM Taifa, Hamisi Mgeja.

Wengine ni mwenyekiti wa zamani wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Jacob Nsumbula, Mwenyekiti wa zamani wa CCM Wilaya ya Bariadi, Charles Nkenyenge na mjumbe wa NEC Mkoa wa Shinyanga anayemaliza muda wake, Juma Matondo.

Wanaogombea nafasi ya Katibu Mwenezi Mkoa ni Hassan Mwendapole anayetetea kiti hicho, Maximin Mazula, Jumanne Donda na Julius Maunde.

Wanaogombea nafasi ya Uweka Hazina Mkoa ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Gaki Investment inayojishughulisha na ununuzi, uchambuzi na usafirishaji wa zao la pamba ambaye pia ni kamanda wa vijana wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Gasper Kileo na Mbunge wa Kishapu, Fred Mpendazoe.

Naye Didas Kaswamila kutoka Musoma anaripoti kwamba; Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Musoma Vijijini, Mara, kinatarajiwa kumjadili Diwani wa Kata ya Nyambono, Arstariko Gamba, kutokana na kauli aliyoitoa kwa waandishi wa habari kwamba anataka Jimbo la Musoma Vijijini ligawanywe na kuwa majimbo mawili.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Fidelis Kisuka, aliwaambia waandishi wa habari, mjini hapa mwishoni mwa wiki kuwa Gamba amekiuka maadili ya chama hicho kwa kudai kuwa baadhi ya viongozi wa chama hicho walizima hoja ya kutaka kugawa jimbo hilo, kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Kisuka alidai chama hicho hakijawahi kujadili hoja ya aina hiyo katika vikao vyake na wala hakuna kiongozi yeyote wa chama hicho aliyezima hoja ya kutaka kugawa jimbo kama ilivyodaiwa na diwani huyo.

Wiki iliyopita Diwani Gamba aliwaambia waandishi wa habari kuwa kikao cha Baraza la Madiwani kiliwahi kutoa hoja ya kutaka kugawanywa jimbo hilo mwaka juzi, lakini kiongozi mmoja alipinga na kuwaita katika hoteli moja na kuwataka kupinga hoja hiyo na kuahidi kuwapatia pikipiki za kufanyia kazi.

Alidai kuwa baada na kupewa ahadi ya kupatiwa pikipiki hizo na huduma nyingine za vinywaji na chakula katika hoteli hiyo, madiwani hao walikataa hoja ya kugawa jimbo na kudai kuwa kiongozi huyo (jina linahifadhiwa) amekwishawaita mara mbili kuwasihi kuendelea kupinga hoja hiyo.

Gamba alithibitisha kuitwa na kuhojiwa na katibu wa wilaya kuhusiana na hoja yake hiyo ya kutaka kugawa jimbo ambapo katibu huyo alimtaka athibitishe kwa maandishi.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.