WAHADZABE wanaoishi katika bonde la Yaeda Chini katika Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara, wamepinga kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Philip Marmo, juu ya hatua ya ardhi yao kukabidhiwa kwa Kampuni ya Arab Emirates kutoka Falme za Kiarabu.
Wakazi hao wa eneo hilo, wamedai kuwa, uamuzi wa kulitoa eneo hilo kwa wawekezaji wageni, umetokana na shinikizo binafsi la kiongozi huyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari juzi mjini hapa, baadhi ya viongozi wawakilishi wa Wahadzabe hao, Judith Yesaya na Merkizedeki Mwengelo, walidai kuwa, Marmo, ambaye ni mbunge wa jimbo hilo, ameamua kuwauza kwa maslahi yake binafsi.
Walisema kama Rais Jakaya Kikwete hatoingilia kati suala hilo, basi naye atakuwa ameshiriki kutokomeza kabila hilo hapa nchini, kwani wanaamini baada ya kampuni hiyo kuanza kazi, hatma ya maisha yao itakuwa hatarini.
Walitoa madai hayo huku wakikumbusha mambo kama hayo yaliyotokea miaka ya nyuma katika Wilaya ya Meatu, mkoani Shinyanga.
Walisema kuwa, eneo lililokuwa linakaliwa na Wahadzabe katika wilaya hiyo, lilitolewa kwa kampuni ya uwindaji ya wageni na baada ya hapo, Wahadzabe wengi waliishia kufungwa jela na wengine kutokomea kusikojulikana.
Mapema wiki hii, Marmo alitumia fursa aliyopewa kuzungumza kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya Muasisi wa Hospitali ya Kilutheri ya Haydom, marehemu Dk. Quisten Oslen, kutangaza msimamo wake wa kuunga mkono kampuni hiyo kuwekeza huko Yaeda Chini.
“Marmo anajua kabisa asili ya tatizo lililopo kwa watu wa jamii ya Kihadzabe, sasa akiwa kiongozi wa serikali na mbunge wetu, kwa nini alishindwa kuja Yaeda Chini, badala yake analizungumzia suala hili huku Haydom?” alihoji Yesaya.
Alisema mgogoro uliopo kati ya Wahadzabe kwa upande mmoja na serikali na kampuni hiyo kwa upande mwingine, ni matokeo ya kutowashirikisha Wahadzabe katika mchakato wa kulitoa eneo hilo kwa mwekezaji huyo.
Alisema hatua za awali za kulikabidhi eneo hilo linalotumiwa na Wahadzabe kwa makazi na chakula kinachotokana na matunda, mizizi, asali na wanyamapori, zilihusisha vitendo vya ubaguzi miongoni mwao.
Naye Mwengela alisema shughuli za uwekezaji katika eneo hilo, zinahofiwa kuwaondoa Wahadzabe kwenye maeneo yao na hivyo kuwa chanzo cha kupotea kwa mila, desturi na utamaduni wao.
Alisema watu wanaounga mkono uwekezaji kupitia Kampuni ya Arab Emirates, wanapotosha umma kuwa Wahadzabe hawapendi maendeleo na badala yake wanataka kuendelea kuishi kwenye hali duni na umaskini.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Henry Shekifu na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Eliasi Goroi, walifanya ziara kwenye eneo hilo ili kumuwezesha mkuu huyo mpya wa mkoa kutambua kinachoendelea katika eneo hilo, na pia kuwahamasisha Wahadzabe kukubali na kushirikiana na Kampuni ya Arab Emirates.
Ziara hiyo ilifanyika siku moja baada ya Marmo kuzungumzia mgogoro huo mjini Haydom na kumtaka Shekifu kuzitambua changamoto mbalimbali zinazotokana na upinzani kutoka kwa Wahadzabe, dhidi ya mpango wa uwekezaji kwenye bonde hilo.
Mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu sasa, huku Wahadzabe wakielezea msimamo wa kupinga, na serikali ikiwahimiza kukubali kushirikiana na kampuni hiyo, inayotekeleza majukumu yake kwa mujibu sa sera ya taifa ya uwekezaji.