Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wizara katika kashfa ya bil. 4/=
Wizara katika kashfa ya bil. 4/=
By Marshy Abdu | Published  06/2/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
Wizara katika kashfa ya bil. 4/-
na Mwandishi Wetu


WIZARA ya Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, inadaiwa kuisababishia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) hasara ya mabilioni ya shilingi.

Habari zilizopatikana, zinasema kuwa hasara hiyo, inayotokana na mpango wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Zanzibar, inafikia sh bilioni nne.

Inadaiwa kuwa, hasara hiyo ilitokana na uamuzi wa baadhi ya viongozi ndani ya wizara hiyo, kuisamehe kiasi hicho cha fedha, kampuni ya China, Huash Enterprises iliyokuwa ikijenga uwanja wa ndege wa Zanzibar.

Kampuni hiyo ilishindwa kufanya kazi ya upanuzi wa uwanja huo kwa kuzingatia masharti ya mkataba, na hivyo mkataba huo kuvunjwa na serikali baada ya kushauriana na mfadhili wa mradi huo ambaye ni Benki ya Dunia.

Taarifa zilizopatikana zinaonyesha kuwa, Benki ya Dunia ilianza kuingiwa na shaka kuhusu mradi huo baada ya wajumbe wake kuzuru Zanzibar mwezi Januari mwaka 2005.

Baada ya ziara hiyo, kampuni hiyo ya Kichina ilipewa miezi mitatu, hadi Machi mwaka huo, kuwa imekamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi huo. Muda uliokuwa umewekwa awali kukamilisha awamu hiyo ni Septemba, 2004.

Hata hivyo, hadi muda huo unatimia, mradi huo, ambao ulikuwa ugharimu shilingi bilioni 9.5, ulikuwa haujakamilika hata kwa asilimia 70.

Uchunguzi zaidi umebaini kwamba, hadi serikali inavunja mkataba wa upanuzi wa uwanja huo, ulikuwa umefikia asilimia 16 tu ya ujenzi.

Taarifa kutoka ndani ya wizara hiyo zinasema kwamba, kwa mujibu wa mkataba wa ujenzi wa mradi huo, kampuni hiyo ya China, ilitakiwa kulipa jumla ya dola za Kimarekani milioni nne, ikiwa ni fidia ya dhamana ya mradi ya dola milioni moja na gharama za ucheleweshaji mradi zinazofikia dola milioni tatu.

Hata hivyo, baada ya kampuni hiyo kulipa dola milioni moja ya dhamana ya mradi kupitia benki moja ya China, inadaiwa kuwa baadhi ya viongozi wa wizara hiyo walizichukua fedha hizo na kuzirejesha kwa kampuni hiyo ya China katika mazingira ya kutatanisha.

Uchunguzi zaidi umegundua kwamba, mbali ya kurejesha fedha hizo, viongozi wa wizara hiyo walichukua juhudi za kuiomba kampuni hiyo ya China kuondoa kesi iliyokuwa imefungua katika mahakama ya kibiashara ya kimataifa na kuisababishia serikali kupoteza shilingi bilioni tatu, ambazo zilitakiwa ilipwe kama hasara ya ucheleweshaji mradi.

“Serikali ilikuwa na nafasi kubwa ya kushinda katika kesi hii, kwa sababu kampuni ya China, Huash ilishindwa kuzingatia mkataba na mashahidi walikuwa Benki ya Dunia, lakini hatua za viongozi zilisababisha fedha hizo kutoweka,” kilisema chanzo kimoja cha habari ndani ya wizara hiyo.

Kilisema kuwa, kitendo hicho kimeivunja moyo Benki ya Dunia na ndio maana hadi sasa wizara hiyo imeshindwa kutangaza zabuni na kuwasilisha maombi mapya ya mkopo kwa Benki ya Dunia ili mradi huo uendelee.

Kataibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Salmin Senga, alithibitisha serikali kuomba kuondoshwa kwa kesi hiyo katika mahakama ya kimataifa, hivyo kutoa fursa kwa suala hilo kumalizwa kwa maelewano.

Hata hivyo, hakutaka kueleza serikali imenufaika vipi katika maelewano hayo, lakini alisema kwamba, wizara inaandaa ombi jingine la mkopo ili lijadiliwe katika kikao cha Benki ya Dunia, Julai, mwaka huu.

“Tunatarajia mradi utaendelea hapo baadaye, kwa vile hivi sasa akaunti ya mradi imefungwa na Benki ya Dunia, hadi hapo tutakapowasilisha maombi mapya ya mkopo na kuidhinishwa,” alisema.

Kwa mujibu wa mkataba, kampuni hiyo ilitakiwa kuongeza urefu wa njia ya kurukia ndege kutoka meta 2,462 hadi kufikia urefu wa meta 3,022.

Uwanja huo ulikuwa ufanyiwe matengenezo kutokana na kukabiliwa na uchakavu mkubwa na kusababisha baadhi ya mashirika ya ndege kusitisha safari zake visiwani humu. Upanuzi wa uwanja huo ulipangwa kukamilika mwaka 2004, lakini hadi 2005 mradi huo ulishindwa kukamilika.

Huo ni mradi wa pili kukwama, ambapo sasa pia ujenzi wa Bandari Kuu Zanzibar unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU) umekwama, ambao ulikuwa umepangwa kutumia kiasi cha shilingi bilioni 43.

Chanzo cha kukwama kwa mradi huo, ni mvutano kati ya Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar kupitia Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) na kampuni ya ujenzi kutoka Denmark, PIHL, juu ya mfumo wa bandari hiyo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.