UMOJA wa vyama vya upinzani, bado umesimama kwenye madai yake, kuitaka serikali iwalipie wanafunzi 29, waliokwama nchini Ukraine, baada ya kushindwa kulipia gharama za masomo na kujikimu.
Safari hii, wapinzani wameyajenga madai yao juu ya madai kuwa, serikali hiyohiyo, ambayo imesisitiza kuwa haiwatambui wanafunzi hao, imewalipia wanafunzi watatu miongoni mwao.
Katika mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa jana na vyama hivyo, ilidaiwa kuwa, wanafunzi hao watatu wamepatiwa mikopo kupitia Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Tamko la wapinzani hao lilisomwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Shaibu Akwilombe, kwa niaba ya Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Tanzania Labour (TLP) na NCCR-Mageuzi.Akwilombe alisema kuwa, vyama hivyo vimesikitishwa na majibu ambayo serikali iliyatoa, ya kudai kuwa wanafunzi hao waliondoka nchini bila ridhaa ya serikali.
Alisema kama serikali haiwatambui wanafunzi hao wote, ieleze ni vigezo gani vimetumika kuwapatia mikopo wanafunzi watatu kati yao na kuwaacha wengine.
Akwilombe aliitaka serikali itoe hadharani barua ya maelekezo kwa wanafunzi hao, ikiwataka waachane na mpango wa kwenda kusoma nje ya nchi kwa kuwa serikali haikuwa na fedha ya kuwasomesha.
“Tunaiomba wizara husika kuweka wazi hadharani majina ya wanafunzi wote waliokubaliwa mikopo kwa mwaka 2005, 2006,” alisema.
Akwilombe alisema kabla ya wanafunzi hao kwenda Ukraine, walihitaji kupata viza, na kwa kuwa Tanzania haina ubalozi nchini Ukraine, walipeleka pasi zao za kusafiria Nairobi, Kenya ili wapatiwe viza.
“Mihuri (viza) hiyo haiwezi kupigwa hadi ijulikane mdhamini ni nani, kama haiwatambui wanafunzi hao, ilikuwaje Ubalozi wa Tanzania na Kenya upitishe pasi za vijana hawa kwa Ubalozi wa Ukraine bila kujua mdhamini?” alihoji.
Wakati huo huo, Akwilombe alidai kuwa, tamko lililotolewa na wapinzani hao siku kadhaa zilizopita, kuhusu kukusanya fedha kwa ajili ya kuwasadia, limetoa imani kwa vyuo vilivyowafukuza wanafunzi hao na kuamua kuwarejesha.
Alisema baada ya vyama hivyo kuwasiliana na vyuo hivyo na kukubali kuwawekea dhamana wanafunzi hao, vyuo viliwarudisha kwa sharti la kuhakikisha kuwa wawe wamelipa madeni yao, ifikapo Juni 10.
Alisema kuwa, vyuo hivyo vinataka hadi tarehe hiyo, viwe vimelipwa jumla ya dola za Kimarekani 10,000 ambazo ni sawa na sh milioni 13.13.
Vyama hivyo tayari vimechanga sh milioni moja na kuwakaribisha Watanzania wengine wenye nia ya kuchangia kupitisha michango yao katika akaunti ya Taasisi ya Elimu na Sheria (Tanlet) namba 201660043 iliyo katika benki ya NMB.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, alisema wapinzani wana vielelezo vyote vinavyoonyesha kuwa wanafunzi watatu wamelipiwa na wanasubiri tamko la serikali kuhusu hoja hiyo ili wavitoe vielelezo hivyo.
“Hivi ni kama vita, hivyo sisi tunataka wao waseme kusudi sisi tuweze kutoa vielelezo vyetu,” alisema Mbatia.
Naye Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, alisema kuwa kitendo cha wanafunzi watatu kulipiwa, kinaonyesha upendeleo wa wazi. Alisema wameshabaini watoto hao ni wa nani na mbinu walizotumia kuweza kuwaingiza katika mikopo hiyo.
“Hatuwataji watoto hao, tunataka wabishe ili tutoe vielelezo vyetu, ni watoto wa vigogo gani ambao wameenda wizarani wakazunguka mbuyu na watoto wao wakalipiwa na wenzao 26 kubaki,” alisema.