SERIKALI ya Ufaransa imeifutia Tanzania deni la sh bilioni 7.5 sanjari na kusaini mkataba wa kuipatia msaada wa sh bilioni 12.
Makubaliano hayo yalitiwa saini jana na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, na Balozi wa Ufaransa hapa nchini, Jacques Champagne de Labriolle, katika ofisi za wizara hiyo.
Akizungumza mara baada ya kuwekeana saini, Waziri Meghji alisema kuwa chini ya mikataba hiyo miwili, Serikali ya Ufaransa itaisaidia Tanzania kiasi cha sh bilioni 19.5.
Fedha hizo zimetolewa kwa ajili ya kusaidia kusambaza huduma za maji na miradi ya kimaendeleo katika miji ya Bukoba na Musoma.
Meghji alisema deni lililofutwa litatumika kusaidia maendeleo ya elimu ya sekondari chini ya Mkakati wa Taifa wa Kupunguza Umaskini.
Kwa mujibu wa Meghji, utekelezaji wa mradi wa kusambaza maji katika miji ya Bukoba na Musoma ulioanza mwaka jana, utaendelea hadi mwaka 2010.
Awali, Waziri Meghji aliishukuru Serikali ya Ufaransa kwa niaba ya serikali na Watanzania kwa ujumla na kusema kuwa miradi hiyo itawasaidia Watanzania hasa kina mama ambao ndio watafutaji wakubwa wa maji, hasa katika maeneo ya vijijini.
Aidha, alisema inafurahisha kuona kuwa Serikali ya Ufaransa hivi sasa imeonyesha nia ya kuisaidia Tanzania.
“Hivi sasa Wafaransa wamejitokeza kuja Afrika Mashariki kusaidia na wako tayari kusaidia katika mambo ya kimaendeleo,” alisema Meghji.
Alisema hii ni mara ya pili kwa Serikali ya Ufaransa kuisaidia Serikali ya Tanzania ambapo mara ya kwanza iliisaidia Tanzania mwaka 2003 kiasi cha sh bilioni 5.124.
Naye Balozi wa Ufaransa hapa nchini, Jacques Champagne de Labriolle, alisema kuwa, kufutwa kwa deni hilo kutachangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha elimu ya msingi na sekondari.
Fedha zilizosamehewa zitatumika katika mradi ambao utekelezaji wake umepangwa kuwa kipindi cha Juni 2006 hadi Machi 2011, ikiwa ni mpango unaoendeshwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Alisema lengo la mpango huo ni kuinua kiwango cha elimu katika shule za msingi na sekondari ikiwa ni pamoja na kuanzisha mfuko wa elimu.
Kwa upande wa maji katika miji ya Bukoba na Musoma, Jacques alisema kuwa, mradi huo utasaidia upatikanaji wa maji ya kunywa katika mpango unaoendeshwa na kusimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Vijijini (UWSAs) kwa niaba ya Wizara ya Maji.
Alisema mpango huo utatekelezwa kwa kuimarisha miundombinu na usambazaji wa maji.