Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Tumeona ya ANBEN, hatutaki kusikia ya SAKI
Tumeona ya ANBEN, hatutaki kusikia ya SAKI
By Habari Tanzania | Published  05/30/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

Mkapa umefanya biashara Ikulu!

“SIAMINI kama mstaafu wetu, Benjamin Mkapa, tuliyemsifia kuwa ni Mr Clean, anaweza kutufanyia hivyo, Watanzania tuwe imara na tuamke na kumbana atuambie kulikoni.” Anaingia Mkurupukaji, anaimba hata hasalimii.

Mgosi Machungu hamkopeshi. “Mgosi hata hutiamkii umeona kuimba ndiyo dii?”

Kama aliyekuwa usingizini anatupa salamaleko na kuendelea. “Mwenzenu siimbi bali naomboleza kugundua kuwa kumbe Kampuni ya ANBEN ni Anna na Ben! Yaani hapa tumemvua nguo mwalimu.

Mkapa, Mkapa, unafanya biashara ukiwa Ikulu! Kweli mbwa hafanani na bwana wake.”

Mgosi anazidi kushangaa. “Mgosi mbona hatikuelewi!”

Mpayukaji naingilia. “Mgosi tatizo lenu ni kujali sana mambo ya tunguli na kudharau uchunguzi.

Hujui kuwa Ben na mkewe kumbe walikuwa wakikopa pesa walipokuwa Ikulu kiasi cha kuanzisha Kampuni ya ANBEN?”

Mgosi hajibu bali kujishika tama na kutamka neno ambalo haliandikiki. Hayo tuyaache.

Mpemba hana hamu na salamu, anachomekea. “Mie nilijua Nkapa si Mr Clean pale nkewe alipokopa pesa na kununua lile jumba pale Barabara ya Morogoro Road na asinkataze,”. Mbwa mwitu anaingilia. “Morogoro Road, maana road ni barabara,”

Mpemba haukubali uchitaaahiro na ukihiyo anajitetea. “Nafahamu sana. Sema hasira nimeghafilika yakhe. Mie najua Nkapa alikuwa alala yule nchaga ndiye kanzindua.”

Mkurupukaji naye hana simile anadonoa mic. "Taarifa nilizo nazo ni kwamba Mkapa na mkewe walianzisha ANBEN pindi tu walipotia mguu Ikulu.

Alipokufa Mchonga wakaisajili na kuendelea kujichotea pesa kwenye mabenki. Hadi naongea wanadaiwa kitu kama bilioni. Walizifanyia nini, nani anajua? Hata hiyo Fursa sawa ilikuwa ni fursa sawa kati ya nani na nani maana ukiwauliza akina mama iliwasadiaje, sijui kama wanajibu.

Mzee Maneno hangoji habari iishe analamba mic. “Mie nilijua walipofichua Waingereza. Nakumbuka yule Mama Shoto alivyotua uwanja wa ndege amefura utadhani angemtimua Mkapa.”

Kabla ya kuendelea Mbwa mwitu anamkosoa. "Ni Clara Short siyo shoto."

Mzee Maneno anasema. "Shoti hiyo hiyo huoni alipowekwa ndani na kupewa lugha tamu akaondoka kwa furaha akatuachia shoti zetu! Kweli wanasiasa ni uchwara hata wawe Wazungu kumbe Nkapa alikuwa akitwambia kwa mafumbo alivokuwa akiwaambia wenzake uchwara, hatukumuelewa!"

Mgosi naye anakwanyua mic. “Mie naona Kikwete aache kuingilia usaama wa nchi hii, aache Mkapa asimame atieleze tiandastandi kwanini yeye na mkewe wamefanya hivyo? Bado tinahisi japo si moja kwa moja, ana mkono kwenye rada, Tanesco, NBC tena na kuanzisha kampuni wakiwa madaakani.

Pia atiambie kwanini aliondoka bila kutaja mali zake na lile hekau la pale Ushoto alijenga kwa bei gani? Mimi naamini kuna mengi kuliko haya tinayoambiwa.”

Makengeza anadakia. “Kikwete hamtetei Mkapa anajitetea mwenyewe. Maana ukiangaria ilipotoka EOTFL imeingia WAMAAAA. Usishangae leo kusikia ANBEN. kesho ukakuta kumbe kuna SAJA, tena zimeungana.

Hapa ni ulaji mtindo mmoja. Huoni wahusika wa Richmond walivyojikausha utadhani watu hawaoni ujambazi tunaofanyiwa.

Sasa kama rais anawatetea wezi kazi yake ni nini hapo Ikuru, sasa hili naro atatwambia nini tumuelewe?"

Mpayukaji nami siwezi kuondoka bila kumwaga cheche, nakula mic. “Kumbukeni Jakaya alisema tumuache mzee Mkapa akatanue. Huenda yeye aliona mizigo ya aibu na kashfa alizo nazo vinatosha lakini akasahau kuwa pesa iliyoibwa kwenye rada na miradi mingine ni yetu siyo yao.

Hapa ndipo bomu letu linaloitwa Katiba linapaswa kubadilishwa haraka kama anavyolalama Mzee Mtei."

Mzee Kidevu naye anatia timu. “Nyie hamjui. Hapa ni kata mti weka mti. Toa kibaka weak kibaka.” Anakohoa na kuendelea. “Kwanza wa kulaumu ni sisi. Asiyesikia la mkuu? Maana Mchonga pamoja na kutuletea kinyago chake cha mpapure alisema wanaokimbilia Ikulu inabidi tuwaulize wanakimbilia nini huko?.

Je, sisi tuliwauliza? au tulishabikia sura na mipasho. Inabidi tukome na kujilaumu huku tukijipanga upya kuwakabili kwa kila hali.”

Matai anachomekea. “Wewe unataka kuvuruga amani sasa.”

Mzee Kidevu hakopeshi. “Amani au ukondoo katikati ya ujambazi? Amani gani iwapo Ikulu inatumika kufanyia biashara? Hivi nyinyi Watanzania nani aliwaroga? Yaani nyinyi mmeridhika na Ikulu yetu kuwa pango la wezi na wachumia tumbo?”

Msomi naona amesukuti muda mrefu. Maana kila anayeongea anamtazama ili achonge. Anatia guu. “Kusema ukweli Mkapa ameamua kujivua nguo. Yeye aliona ni siri. Tunajua kuwa ANBEN ilisajiliwa mwaka 1999 baada ya kuona Mchonga amekufa. Acha hiyo kuna na nyingine ya Ikulu humo humo.

Yaani tumekuwa wa ovyo kuruhusu Ikulu yetu ifanyiwe umachinga na uchafu huu!” Anatuangalia na kubwia tangawizi yake na kuendelea. “Hapa inabidi wananchi tuache woga tumtake rais achague moja, kuongoza au kumtetea huyo mwenzake. Hapa lazima wapinzani waungane na wananchi mitaani kuendesha migomo na maandamano ili tuwabane hawa.

Nakumbuka Mrema alishtuka mwanzo akasema huyu si Mr. Clean, akaonyesha jinsi alivyopokea bonge la dhahabu watu hawakujali. Sasa uwezo tunao, sababu zipo za kumhoji Mkapa. Maana nakumbuka ubabe wake akitukana waandishi kuwa ni uchwara na wana wivu wa kike na uvivu wa kufikiri. Hivi ni tamaa gani kwa rais aliyeko madarakani kujiingiza kwenye umachinga Ikulu?

Nyerere alisema ogopa rais anayetawaliwa na kushauriwa na mkewe lakini hatukuelewa.”

Anakohoa na kujifuta jasho na kuendelea. “Mie nachukia wanafiki sawa na nguruwe. Heri hata ya Mobutu maana alijionyesha alivyokuwa jambazi badala ya mashetani wanaojionyesha kama malaika.

Nchi hii inahitaji rais aina ya Mwanawasa badala ya kulindana. Sasa lazima tutoe shinikizo kwa rais maana nchi hii si yake kwamba Mkapa lazima aseme mbele ya umma, mbele ya sheria ili liwe somo kwa wengine.

Rais wetu namheshimu asitake tumdhanie vibaya. Yeye atakuwa mtu wa kashfa za wengine hadi lini?

Nyumba zetu kachuna, Richmond usanii, Mkapa oh! Mara mzee Mkapa. Hapa hakuna cha mzee Mkapa angetaka iwe hivyo angeigiza mfano wa mtu aliyembeba hadi akafika hapo alipokuwa hapaotei wala kujiandalia.

Kikwete badala ya kulipwa mshahara na marupurupu yetu kwa kumkingia kifua lazima aweke msimamo wake kama ni kulinda mali zetu au kuwalinda wanaoiba mali zetu. Hapa ndipo wapinzani wana kete ya wazi.

Wangeanza kuwashawishi wafadhili wenye akili kama nchi za Japan na Scandinavia kuanza kutoa shinikizo wanaotafuna nyumba yetu, wangeshughulikiwa.

Kumbe wakati Nyerere alisema tuwaogope kama ukoma alishajua kuwa wako wanakuja na sasa tunao!”

“Msomi sikubaliani nawe. Hapa ni suala la Watanzania kuingia mitaani kwa maandamano na migomo ili kieleweke kama kazi ya Jakaya ni kuwalinda wahalifu au kupambana nao.

Hawezi kukaa kwenye Ikulu ya wananchi na akaendelea kuwalinda wabaya wao.

Naye kama amechoka si atimke tu maana hatuoni hata sera wala la maana zaidi ya kashfa. Tumechoka sasa na isitoshe mtu mzima hasutwi.” Anachomekea Mchunguliaji aliyekuwa amenyamaza kitambo.

Msomi anaendelea. “Jakaya inabidi ajikumbushe Mkapa alivyokuwa na ubabe, sasa viko wapi anaishi kwa kujificha maana madhambi yake yanamfuata. Isitoshe miaka mitano au kumi si mbali, kesho anaweza kujikuta walipo kina Chiluba. Pia afahamu kuwa kutokuwa na miiko ya uongozi ni hatari kwa rais, maana watu wengi watajifanyia wanavyotaka lakini atakayeulizwa baadaye ni yeye.

Jamani mwalimu mbona ametuachia hazina ambayo tunaichezea kama mataahira!”

Jana nilikunywa sana. Wakati maongezi ndiyo yananoga, si tumbo la…. lilinishika. Kilichofuatia unafahamu! Tuonane wiki ijayo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.