TULIANDIKA, tukaandika tena, na sasa tunaandika kwa mara nyingine.
Na kama tulivyopata kuahidi mara kadhaa huko nyuma, tutaendelea kuandika na kulifuatilia suala hili hadi hapo tutakapoona limemalizika na kuhitimishwa.
Ni miezi kadhaa imepita tangu Rais Jakaya Kikwete na baadaye Naibu Waziri wa Miundombinu, Makongoro Mahanga, walipotangaza kuhakiki na kuanza kufikia urejeshwaji wa baadhi ya nyumba za serikali zilizouzwa katika mazingira yaliyoibua shaka.
Uamuzi wa serikali wa kuzirejesha nyumba hizo za serikali ulitangazwa hadharani kwa mara ya kwanza na Rais wakati alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, Ikulu jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa mwezi Oktoba.
Zaidi ya mwezi mmoja tangu atoe kauli hiyo, Mahanga aliusisitizia uamuzi huo bungeni mjini Dodoma.
Kama alivyosema Rais Kikwete, Makongoro katika kauli yake hiyo ya bungeni alieleza kwamba, baadhi ya nyumba zitakazorudishwa ni zile ambazo ziko katika maeneo nyeti kama vile hospitalini na katika maeneo ya majeshi.
Hata hivyo, Makongoro hakuishia hapo, bali alikwenda mbali zaidi na kusema kwamba, sehemu ya nyumba zitakazorejeshwa ni zile ambazo uuzwaji wake haukufuata taratibu halali za kiserikali.
Tukiwa ni sehemu ya Watanzania ambao tumekuwa tukilifuatilia jambo hili kwa muda mrefu, msimamo wetu wa kupingana kabisa na maamuzi ya serikali kuuza nyumba za serikali unaendelea kubakia ule ule.
Kama tulivyokwisha kuandika mara kadhaa siku zilizopita, sisi wa Tanzania Daima, kwa dhati kabisa tunaamini kwamba, uamuzi wa Baraza la Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tatu, wa kuuza nyumba za serikali kwa watumishi wake, bila kujali iwapo walikuwa na sifa au hawakuwa nazo, ni mbaya na ambao kimsingi ulipaswa kubatilishwa.
Tunasema ni wa ovyo, kwa sababu uamuzi huo ulifanywa katika misingi ya kibinafsi na iliyolenga kulisaidia kundi dogo la viongozi na kusahau kwamba, dhamana ya mtu kuwa mtumishi au kiongozi wa serikali ni ya muda tu na wala haimpi nafasi ya kumiliki mali ambazo kimsingi zingekuja kutumiwa na viongozi wajao wa umma.
Ni kwa kuzingatia ukweli huo basi, ndiyo maana tunakiona hata hiki kitendo cha serikali kuendelea kukaa kimya pasipo kueleza mahali ilikofika katika kufanikisha zoezi hili muhimu kwa masilahi ya taifa, kuwa si kizuri.
Hata hivyo wakati tukitaka kusikia matokeo ya operesheni hiyo ya kimya kimya ya serikali, tunapenda kutumia fursa hii kusisitiza msimamo wetu wa kutaka nyumba zote zilizouzwa zirejeshwe na si baadhi ya nyumba.
Tunasema hivyo tukitambua kwamba uamuzi mzima wa kuziuza zile nyumba ulifikiwa kwa makosa tu na kwa hiyo unapaswa kutenguliwa na serikali kuangalia namna ya kulipana na hao wanunuzi wake.
Ni jambo lisiloingia akilini kwa serikali kudai kwamba kulikuwa na kasoro katika suala zima la uuzwaji wa nyumba hizo, na halafu ikasisitiza tu kuwa zitakazorejeshwa ni baadhi tu ya nyumba.
Tunachokiona sisi ni kwamba, iwapo uamuzi wa kuzirejesha nyumba utafanywa nusunusu, basi kuna hatari kubwa kwa makosa kama yale yaliyotokea wakati wa operesheni ya mwanzo yatatokea tena.
Tunasema hivyo tukitambua kwamba, baadhi ya viongozi walioamua kuuza zile nyumba wakati ule wangali wapo ndani ya baraza hili la mawaziri na kuwa haitakuwa rahisi kwao kutengua maamuzi ambayo kimsingi ndio walioyasimamia.
Ili tuweze kuondokana na wingu la shaka ambalo tayari limeshaanza kutanda, tunaiomba serikali yetu kutueleza kwa wazi kabisa ilipofikia sasa katika kulisimamia suala hilo ambalo lilitolewa kauli na rais mwenyewe miezi zaidi ya minne iliyopita.