Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mtikila akamatwa mara mbili
Mtikila akamatwa mara mbili
By Marshy Abdu | Published  05/30/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
Mtikila akamatwa mara mbili
na Irene Mark


MWENYEKITI wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa tuhuma za kumjeruhi mwanamke.

Aidha, mwanasiasa huyo ambaye pia ni kiongozi wa dini, alikamatwa mara baada ya kuachiwa kwa dhamana, na kupelekwa kituo cha Polisi huko Temeke, ambako aliandika maelezo yake kuhusiana na tukio la kupigwa kwa dereva wa daladala.

Mbele ya Hakimu Catherine Revocati, Mtikila alidaiwa kumpiga mwanamke huyo, mlinzi katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili.

Alipofikishwa katika Mahakama ya Kisutu, ilidaiwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Charles Kenyela, kwamba Aprili 19 mwaka huu, majira ya saa tano asubuhi, kinyume cha sheria, Mtikila akiwa katika Ofisi za Msajili wa Vyama vya Siasa, alimpiga Maimuna Muya, makofi na ngumi, hali iliyomsababishia majeraha.

Baada ya kusomewa maelezo ya kosa, Mchungaji Mtikila alikana kosa na wakili wa kujitegemea anayemtetea katika kesi hiyo, Daimu Halfan, aliiomba mahakama kumpatia dhamana mteja wake.

Upande wa mashitaka haukuwa na pingamizi na ombi hilo la dhamana kwa mtuhumiwa, ambapo mahakama ilimpatia dhamana kwa masharti ya kusaini mkataba wa sh milioni 20 pamoja na wadhamini wawili watakaosaini kiasi hicho cha fedha kila mmoja.

Upande wa mashitaka katika kesi hiyo namba 744/2007 ulidai kuwa, upelelezi umekamilika na kuomba tarehe ya kusomwa kwa maelezo ya awali. Hakimu aliahirisha shauri hilo hadi Juni 25 mwaka huu kesi itakapoanza kusikilizwa.

Habari zaidi kutoka nje ya mahakama, zimeeleza kuwa siku ya tukio Mtikila, akiwa kwenye teksi alifika katika ofisi hizo na kutaka kufunguliwa geti.

Alipotakiwa kufuata taratibu za kiofisi, ikiwa ni pamoja na kuandikisha jina, aligoma kufanya hivyo kwa madai kuwa yeye ni mheshimiwa, majibu yaliyomfanya Muya ampe kitambulisho cha kuingia ndani ya ofisi hizo.

Wakati anapewa kitambulisho hicho, Mchungaji Mtikila alidaiwa kumpiga vibao na ngumi mlinzi huyo kabla ya watumishi wengine wa ofisi hiyo kuamua ugomvi huo.

Aidha, baada ya kupatiwa dhamana na kutoka nje ya mahakama hiyo, Mtikila alitiwa mbaroni na Mkuu wa Makosa ya Jinai Wilaya ya Temeke, aliyejulikana kwa jina moja la Hamisi na akapelekwa katika Kituo cha Polisi Chang’ombe kwa ajili ya kuandika maelezo ya tuhuma za kumjeruhi dereva wa daladala.

Mtikila anadaiwa kumshambulia kwa ngumi na makofi dereva Ramadhan Shaaban (45) wa daladala namba T261 ACE, linalofanya safari zake kati ya Mbagala na Kivukoni.

Imeelezwa kwamba tukio hilo lilitokea Mei 20 mwaka huu majira ya saa moja usiku eneo la Mbagala Zakheem, baada ya gari alilokuwamo Mtikila aina ya Mercedes Benz, lenye namba za usajili T930 ACQ, kuguswa kioo cha mbele na daladala hilo, hali iliyomfanya kupandwa jazba.

Baada ya kupigwa na Mchungaji Mtikila, dereva huyo alitoa taarifa katika kituo kidogo cha polisi huko Mbagala na kupatiwa RB namba MBL/RB/4340/2007, hali iliyosababisha Jeshi la Polisi Wilaya ya Temeke kumsaka mtuhumiwa huyo.

Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Temeke, Emmanuel Kandihabi, alithibitisha kutiwa mbaroni na kuhojiwa kwa Mchungaji Mtikila katika Kituo cha Polisi Chang’ombe, lakini alishindwa kulizungumzia suala hilo kwa undani kwa maelezo kuwa yupo kwenye msiba.

Habari zilizopatikana baadaye, zilieleza kuwa Mtikila alihojiwa na kuachiwa kwa dhamana ya polisi baada ya kutimiza sharti la kuwa na mdhamini mmoja, na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi kuhusiana na tukio hilo.

Alipoulizwa na gazeti hili kama amepewa sharti la kuripoti kituoni hapo kila mara, alisema kuwa hakupewa sharti hilo na polisi walimweleza kuwa iwapo watamhitaji watamtafuta.

Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusiana na ‘mikasa’ hiyo, Mtikila alisema anaamini kuwa hayo yanatokea kutokana na juhudi zake za kuhakikisha sheria za nchi zinaheshimika.

Aidha, aliyahusisha matukio hayo na kile alichokiita ufisadi unaofanywa na viongozi katika Jeshi la Polisi kwa nia ya kujipendekeza ili wapandishwe vyeo.

“Ni ufisadi wa viongozi wa polisi kwa kuwa wana njaa ya kupanda vyeo…ukizingatia hili la kwanza lilitokea Februari, wakati hili la pili lilitokea siku nane zilizopita.

“Kisheria haya ni makosa madogo madogo lakini wao wanayashabikia sana, ila lengo langu la kumuona Rais Jakaya Kikwete lipo pale pale,” alisema Mchungaji Mtikila.

Matukio hayo yanakuja siku chache tu baada ya mwanasiasa huyo kufungua kesi ya mauaji dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.