SIKU moja baada ya wapinzani kutoa mchango wa sh milioni moja kuwasaidia wanafunzi 29 Watanzania waliokwama Ukraine kwa kukosa ada, serikali imejitokeza kukataa kuwasaidia.
Tamko la serikali lililotolewa jana limewataka wanafunzi hao kuondoka mara moja katika Ubalozi wa Uingereza nchini Ukraine walikokimbilia kuomba hifadhi baada ya kufukuzwa katika hosteli au kurejea nyumbani haraka.
Akisoma tamko la serikali kwa waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Celestin Gesimba, alisema serikali haiwajibiki kwa gharama zilizojitokeza kwa wanafunzi hao kwa vile walikwenda nchini humo kwa utaratibu binafsi, tena baada ya wazazi wao kupinga ushauri wa serikali wa kuwataka watafute nafasi ya kusoma hapa nchini.
“Serikali haiwajibiki na gharama zozote zilizojitokeza kwa wanafunzi wa elimu ya juu walioko nje ya nchi kwa vile walikwenda wao binafsi,” alisema Gesimba.
Alisema sababu nyingine ya serikali kushindwa kuwasaidia wanafunzi hao inatokana na kutokuwa na bajeti ya fedha kwa ajili ya kazi hiyo kwa sasa.
Alisema kwa vile wazazi wao waliamua wao wenyewe kwa nia njema kuwapatia elimu ya juu nje ya nchi watoto wao kwa gharama binafsi, wao wenyewe ndio wanaopaswa kuwajibika na gharama za masomo ya watoto wao na wala si serikali.
Aidha, alisema kutokana na hali hiyo, serikali inawaagiza wanafunzi wote waliopiga kambi katika Ubalozi wa Uingereza mjini Moscow, Urusi kuondoka mara moja au kurudi kwenye vyuo vyao kuendelea na masomo.
“Kama watashindwa kufanya hivyo, basi warejee nyumbani Tanzania ili waanze utaratibu wa maombi kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu hapa nchini,” alisema Gesimba.
Alisema kwa wanafunzi wasiokuwa na nauli ya kuwarudisha nyumbani, wanapaswa kujaza fomu maalumu za kuomba mkopo wa nauli ili wakirudi nchini wafanye utaratibu wa kurudisha mkopo huo mara moja.
“Serikali imekubali na itatuma tiketi za ndege mara baada ya kupata majina kamili ya wanafunzi wote, ili warudi nyumbani… lakini mara baada ya kufika wanapaswa kurudisha gharama ya tiketi hizo kwa vile wamekopeshwa,” alisema Gesimba.
Alisema katika mwaka wa masomo 2005/06 jumla ya wanafunzi 130 walipata udahili katika vyuo vikuu mbalimbali nchini Ukraine, ambapo kati ya hao 84 tu ndio walioweza kukamilisha taratibu za kuondoka nchini pamoja na taratibu za kupata mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Alisema wanafunzi 46 hawakuweza kukamilisha taratibu hizo, hivyo hawakuweza kuondoka katika mwaka huo wa masomo.
Kutokana na kukwama, wanafunzi hao walishauriwa wajiunge na vyuo vya elimu ya juu ndani ya nchi, kwa vile serikali haikuwa na uwezo wa kifedha kuweza kuwakopesha wanafunzi wapya nje ya nchi.
“Wanafunzi 17 kati ya 46 walikubali kutafuta udahili kwa vyuo vya elimu ya juu hapa nchini na hadi sasa wanaendelea na masomo, lakini wanafunzi 29 ambao sasa wamekumbwa na matatizo huko Ukraine hawakukubali ushauri wa serikali wa kutafuta udahili hapa nchini na hivyo kuamua utaratibu wao binafsi kwenda Ukraine,” alisema Gesimba.
Alisema kila mmoja atakuwa na kumbukumbu kwamba mwaka 2006/2007 serikali haikukopesha mwanafunzi yeyote mpya wa mwaka wa kwanza kwenda nje ya nchi kwa ajili ya masomo.
Alisema mwaka wa masomo 2005/2006 ndio mwaka wa kwanza wa kutekeleza sheria namba 9 ya 2004 na wanafunzi waliopata udahili wa vyuo vya elimu ya juu waliomba mikopo kwa sababu chombo cha kutambua wanafunzi wanaohitaji mikopo kilikuwa bado hakijawa tayari.
Alisema baada ya maelekezo hayo yote, wanafunzi hao walishauriwa kutafuta udahili katika vyuo vya elimu ya juu nchini, lakini kwa uamuzi wao waliamua kujilipia nauli na kwenda Ukraine bila idhini ya serikali au ahadi ya maandishi kuwa wangeweza kusaidiwa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Juzi viongozi wa muungano wa vyama vinne vya upinzani vya CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi na TLP walianzisha harambee yenye nia ya kukusanya fedha kwa ajili ua kuwasaidia wanafunzi hao 29 waliokwama nchini Ukraine.