Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Lowassa akumbusha enzi zake na Kikwete
Lowassa akumbusha enzi zake na Kikwete
By Habari Tanzania | Published  05/29/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Tamali Vullu


WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, jana kwa pamoja walikwenda katika Ofisi za CCM Mkoa wa Dar es Salaam kuchukua fomu za kuomba kugombea ujumbe wa Halmshauri Kuu (NEC) ya chama hicho.

Hii inakuwa ni mara ya pili kwa Lowassa kwenda kuchukua fomu za kugombea uongozi kwa staili hiyo hiyo ya kusindikizana, baada ya kufanya hivyo miaka 12 iliyopita alipoongozana na Rais Jakaya Kikwete (wakati huo akiwa Waziri wa Nishati na Madini) kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania urais kupitia chama hicho.

Akizungumza kabla ya kuchukua fomu hizo jana katika Ofisi za CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, Makamba alitamba kushinda ujumbe wa NEC wakati Lowassa aliyezungumza baada ya tukio hilo, aliwaomba wajumbe wa NEC kumwamini na kumchagua tena.

“Tunakwenda kuchukua fomu tukiwa na uhakika wa kushinda,” alisema Makamba.

Lowassa, alifika ofisi ndogo za CCM-Lumumba saa 2.55 asubuhi akiwa katika msafara rasmi wa magari ya Waziri Mkuu akiwa katika sare rasmi za chama hicho, shati la kijani na suruali nyeusi na dakika zisizozidi tano, Makamba akawasili hapo na wote wakaongozana kwenda kuchukua fomu hizo katika Ofisi za CCM Mkoa wa Dar es Salaam.

Baadhi ya makada wa chama hicho waliokuwapo katika maeneo ya ofisi hizo, walionekana wakijaribu kuwasindikiza kwa maandamano viongozi hao wawili kabla hatua hiyo haijatulizwa kimya kimya kwa maelezo kuwa mmoja kati ya wanasiasa hao wawili, aliupinga utaratibu huo usio rasmi.

Akizungumza kabla ya kuwakabidhi fomu hizo, Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kapteni John Barongo, aliwapongeza kwa kukubali kuomba uongozi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

“Nawapongeza kwa kusimamia chama kama viongozi wa juu wa kitaifa kwa nyadhifa zenu na kwa kumsaidia Rais Jakaya Kikwete. Endeleeni kumsaidia ndani ya chama na serikali.

“Mwaka huu ni wa uchaguzi ndani ya chama chetu. Wanachama wengi wamejitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi. Ni haki yao ya msingi ya kikatiba. Tunataka viongozi wa aina ipi ili kwenda sambamba na wakati?” alihoji Barongo.

Alieleza kuwa, hawachagui viongozi kutokana na uwezo wao wa kifedha, ingawa wapo wazuri wanaokielewa, walio na uchungu na chama hicho na kuongeza kwamba, hawachagui viongozi kwa sababu ni masikini. Tuwachague viongozi kutokana na uelewa wao wa chama chenyewe, uzoefu wao, umakini na uadilifu wao na mchango wao katika chama bila ya kujali fedha.

“Tuwachague viongozi wanaokipenda kwelikweli, wanaoweza kuchangia katika mikakati ya kuimarisha chama, si viongozi wa kupitia chama walinde maslahi yao au iwe ndio njia ya kupata madaraka ya juu. Tunao wanachama wazuri, tuwachague hao bila ushawishi wa fedha. Tujenge chama imara,” alisema katibu huyo.

“Bado CCM ina hazina kubwa ya viongozi bora, lakini iwapo hatutaweka mikakati ya makusudi katika kuwabaini vijana wenye vipaji vya uongozi na kuwaandaa vijana kimadili na kitaaluma, basi taasisi za kisiasa na serikali wanaweza wakaendeshwa na watu wasio wazalendo, wahuni na wababaishaji,” alieleza katibu hiyo.

Mbali na Makamba na Lowassa, wanachama wengine waliokwishachukua fomu kuwania ujumbe wa NEC ni, Profesa Juma Kapuya, Frederick Sumaye, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi, Zakhia Meghji, Nalaila Kiula, Regina Chonjo, Jacob Mbawala, Mwadawa Lugongo, Kimwana Sherally, Tarimba Abbas na Mosses Kabambala.

Waliochukua fomu kuwania ujumbe wa NEC kupitia vijana ni Nape Nnauye, Sixtus Mapunda, Anastazia Rugaba, Zainabu Kawawa, Alhaji Salum Londa na Ashura Abubakari. Walioomba kupitia wazazi ni Wilbard Lorri, Salimu Mwaking’inda, Salim Dossi, Zahoro Madeni, Sofia Simba, Tarimba Abbas, Kennedy Shine na Brigedia Jenerali Mwilipanga Lupembe.

Waliiomba ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa ni Regina Chonjo, Mustapha Yakub, Nelson Ngajilo na Shaban Chawila amechukua fomu kuwania ujumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa.

Kwa upande wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, waliochukua fomu ni Hemed Mkali, John Guninita na Kawawa Wasenga. Salum Londa amechukua fomu kuwania ujumbe wa NEC Mkoa na Salim Mwaking’inda amechukua fomu kuwania nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi.

Salim Dossi na Tarimba Abbas wamechukua fomu kuwania nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.