Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Edward Lowassa ameonya kuwa serikali haitawavumilia wakuu wa wilaya watakaoshindwa kusimamia kikamilifu kilimo cha zao la pamba.
Akizungumza na wadau wa sekta ndogo ya zao hilo kwenye ukumbi wa Karimjee, mjini Dar es Salaam jana, Lowassa alisema serikali haitaki kusikia visingizio vyovyote kutoka kwa watendaji hao vinavyohusiana na kushindwa kwao katika kusimamia maboresho ya zao la pamba.
“Chini ya usimamizi bora tutaweza kuboresha kilimo cha pamba, kwa hiyo sitaki kusikia visingizio vyo vyote,” alisema na kuongeza: “Mbona tulipojipanga vizuri tuliweza kujenga madarasa na kuwapatia nafasi za kuendelea na masomo wanafunzi ambao awali waliachwa kutokana na kukosa nafasi?”
Kikao hicho kiliitishwa na Waziri Mkuu kwa lengo la kubadilishana mawazo na wadau hao kuhusu vikwazo kwa maendeleo ya kilimo cha pamba na jinsi ya kuviondoa ili kiweze kuwa na manufaa kwa wakulima na taifa.
Lowassa alisema serikali inataka kuboresha kilimo, na hasa cha pamba, kwa vile inaamini kinaweza kutoa ajira nyingi zaidi endapo kitasimamiwa ipasavyo.
Aliitaja sababu nyingine ya uamuzi huo kuwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka jana, ambayo inahimiza sekta ya kilimo ipewe kipaumbele ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Katika kuhakikisha kilimo cha pamba kinafanikiwa, Waziri Mkuu aliwahakikishia wadau hao kuwa serikali itashughulikia matatizo yanayowakabili wakulima, hata kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa kilimo.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Joseph Mungai alisema kilimo cha pamba kinakabiliwa na matatizo mengi ambayo yamechangia katika kuwazuia wawekezaji kujitokeza kuwekeza hapa nchini.
Alitoa mfano kwamba hadi sasa wakulima wanaendelea kutegemea mvua, utaratibu ambao ni kinyume na unaotumika nchi za nje, ambapo asilimia 53 ya eneo linalotumika kwa kilimo hicho linatumia umwagiliaji.
“Siyo hivyo tu, bali hata wanapojitahidi na kuzalisha, wakulima wanavunjwa moyo kutokana na kukopwa mazao yao au kukatwa fedha kwa ajili ya kulipa kodi mbalimbali,” alisema na kuongeza kuwa kupitia mfumo huo, wakulima wameweza kupoteza sh. bilioni 32.
Mungai alisema hali hiyo imeathiri pia mauzo ya pamba kutokana na kupoteza masoko ya nje katika nchi mbalimbali, zikiwemo Italia na Ujerumani ambazo alisema awali zilichangamkia kununua pamba ya Tanzania kutokana na sifa kubwa iliyopewa ya ‘dhahabu nyeupe’ kutokana na ubora wake.
Wakati huo huo, malalamiko yanayotokana na wakulima kukopwa pamba yao yalitawala kikoa hicho, ambapo baadhi ya wadau waliielezea hali hiyo kuwa inaua ari yao katika kuendeleza zao hilo.
Katika kuwaondolea wakulima kikwazo hicho, wajumbe wa mkutano huo walimwomba Waziri Mungai kutumia kasi kuondoa kero hiyo ili kuwarejeshea wakulima uwezo ambao kwa kiasi fulani umetetereka.
Mkuu wa mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, alisema kilimo cha pamba kimekuwa mzigo kwa wakulima kwa vile kadri wanavyoongeza kulima ndivyo wanavyozidi kukopwa.
Mwenyekiti wa chama cha siasa cha UDP, John Cheyo alidai kuwa kilimo cha pamba ni mchezo uliobuniwa na wajanja kwa ajili ya kuwazidishia wananchi umasikini. “Inawezekanaje mkulima akatwe sh. 40 kutoka katika kilo ya pamba anayouza kwa bei ya sh. 225?” alihoji.
Kutoka gazeti la Uhuru