Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Dhehebu la kuua watu halijasajiliwa
Dhehebu la kuua watu halijasajiliwa
By Habari Tanzania | Published  05/28/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Tamali Vullu


SERIKALI imekana kulitambua kanisa moja lijulikanalo kama Faraja, lenye makao yake makuu jijini Mwanza, ambalo huendesha ibada za kafara ya damu.

Gazeti hili limethibitisha kuwa kanisa hilo, lenye makao yake eneo la Butimba B, mkoani Mwanza ambalo hutoa kafara za damu za binadamu na kusali uchi, halijasajiliwa katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya hiari.

Akizungumza na Tanzania Daima jana ofisini kwake, Msajili wa Vyama, Frolian Mushi, alisema kumbukumbu zilizopo ofisi kwake, hazionyeshi kuwepo kwa dhehebu au kanisa la aina hiyo.

Aliongeza kuwa hado hivi sasa, ofisi yake haijawahi kupokea watu wenye maombi ya kutaka kusajili dhehebu au kanisa lenye jina kama hilo.

“Hata kama wangekuja hapa wasingepata usajili, kwani kabla chama chochote hakijapatiwa usajili, kinapaswa kueleza malengo yake na jinsi kitakavyojiendesha,” alisema msajili huyo.

Hata hivyo, dhehebu hilo tayari limeshasambaa katika mikoa ya Mwanza, Mara, Morogoro, Arusha na Dodoma.

Hayo yamebainishwa kutokana na uchunguzi ulioanzia mkoani Mwanza, ambako tayari Jeshi la Polisi mkoani humo sasa linamshikilia muumini wa dhehebu hilo.

Habari zaidi ambazo gazeti hili limezipata, zinaeleza kuwa huko Musoma, mkoani Mara, dhehebu hilo liliibuka wakati wa kipindi ambacho taifa lilikuwa linakabiliwa na upungufu wa chakula.

Inadaiwa kuwa waliokuwa viongozi wa dhehebu hilo, walikuwa wakiwavuta watu kuwa waumini wao kwa kugawa mahindi, hasa wakati wa ibada.

“Katika kipindi hicho walikuwa wakigawa mahindi mjini Musoma na watu waliokuwa wametumia mahindi hayo walijikuta wakiingia katika dhehebu hilo. Suala hili linahusishwa na imani za kishirikina,” kilieleza chanzo chetu.

Chanzo hicho kiliendelea kueleza kuwa lilipoingia mkoani Mwanza, dhehebu hilo liliingia kupitia mihadhara iliyokuwa inafanywa na viongozi wake.

Taarifa zinaonyesha kuwa, mbali ya dhehebu hilo kutoa kafara watu, hususan watoto vipenzi vya waumini wake, misa huendeshwa wakati waumini wote wakiwa watupu, pasipo mavazi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Zelothe Stephen, alilithibitishia gazeti hili kukamatwa kwa mtu mmoja anayetuhumiwa kuwa muumini wa kanisa hilo, aliyemtaja kwa jina la Yunus Simon.

Kwa mujibu wa Kamanda Stephen, mtuhumiwa huyo ambaye bado anaisaidia polisi kuendesha uchunguzi wake, amefunguliwa jalada katika Kituo Kikuu cha Polisi Mwanza, lenye namba MWS/IR/796/07.

Taarifa za polisi mkoani Mwanza kulibaini dhehebu hilo lililopo katika maeneo ya Butimba, zimekuja takriban miezi miwili tangu gazeti hili liandike kwa mara ya kwanza kuhusu kuwapo kwa kanisa la aina hiyo katika mikoa kadhaa nchini.

Kukamatwa kwa muumini huyo, kunahusishwa pia na kupatikana akiwa amefichwa ndani ya kanisa hilo, mama mmoja aliyetajwa kwa jina la Marium Pius, akionekana kuwa katika hali ya kupagawa na kurukwa akili baada ya kushawishiwa kujiunga na kanisa hilo.

Polisi hao bado wanachunguza madai yanayomhusisha muumini Simon kuwa ndiye mtu aliyemshawishi mama huyo kujiunga na dhehebu hilo, ili siku moja yeye na mwanawe ajulikanaye kwa jina la Angel Michael (5), watolewe kafara.

Kwa mujibu wa Kamanda Zelothe, baada ya uchunguzi wa awali wa polisi uliofanikisha kumtia mbaroni mtuhumiwa huyo dhidi ya tuhuma hizo za awali, jeshi lake sasa linaendelea kuwasaka waumini wengine wa kanisa hilo, linaloendesha ibada zinazokwenda kinyume cha maadili ya kiutu.

Kuhusu kupatikana kwa mwanamke huyo, Kamanda Stephen alisema tayari walikuwa wameshamkabidhi kwa ndugu zake walioko wilayani Magu, ambako anapatiwa matibabu.

Mume wa mwanamke huyo, Michael Laurent, aliliambia gazeti hili kuwa wazazi wa mwanamke huyo walikataa kumpeleka hospitali ili apatiwe matibabu na badala yake wakampeleka kwa waganga wa kiasili, kwa madai kwamba nguvu za giza ndizo zitaweza kumponya.

Aidha, uchunguzi wa muda mrefu wa gazeti hili umebaini kuwa, waumini wa dhehebu hilo hufanya maombi yao nyakati za usiku.

Akizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, mmoja wa waumini aliyelikimbia kanisa hilo, alidokeza kuwa, inapofika wakati wa maombi katika ibada ambayo hufanyika usiku, waumini wote hutakiwa kuvua nguo na kubaki uchi wa mnyama.

Alisema unapowadia wakati huo, watoto waliopo hutolewa nje na waumini wakishavua nguo zao, huendelea kusali na kuimba.

Kwa kawaida, watoto ambao huambatana na mama zao kwenye ibada, hutunzwa katika chumba kingine kanisani hapo, na wengine hupelekwa katika nyumba za waumini na kupatiwa huduma zote, ikiwamo chakula.

Alisema kuwa imani ya kanisa hilo inawataka watu waliooana kuachana na kumfuata Yesu.

Aidha, familia ikiwa ina mtoto ambaye wanampenda sana, hulazimishwa wamtoe kafara ili kuonyesha kuwa wanampenda Mungu zaidi ya mtoto huyo.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, baadhi ya watoto ambao wazazi wao wameachana kutokana na imani ya kanisa hilo, wamehamishiwa katika vituo mbalimbali, ambavyo ni wakala wa kanisa katika mikoa ya Morogoro, Arusha, Mara na Dodoma.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.