MUUNGANO wa vyama vinne vya upinzani nchini wameanzisha harambee, yenye nia ya kukusanya fedha kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wa Kitanzania wapatao 29 ambao wamekwama nchini Ukraine.
Wanafunzi hao wamejikuta katika hali mbaya baada ya kushindwa kulipia gharama za masomo na kuishi nchini humo, baada ya serikali kukataa kuwapatia mikopo chini ya mfumo wa kuwakopesha wanafunzi wa elimu ya juu.
Umoja huo wa vyama ulisema jana kuwa lengo ni kukusanya kiasi cha kutosha cha fedha ili kuhakikisha kuwa wanafunzi hao wanamaliza masomo yao katika Chuo cha Kharzin, nchini Ukraine.
Vyama hivyo vya upinzani vimefikia hatua hiyo baada ya jitihada za wanafunzi hao na wazazi wao kuitaka serikali iwasaidie kulipia gharama za masomo kupitia mfumo wa kuwakopesha wanafunzi wa elimu ya juu kugonga mwamba.
Uamuzi huo ulitangazwa jana na viongozi wa vyama hivyo vya siasa, katika mkutano na waandishi wa habari, ambao pia ulihudhuriwa na baadhi ya wazazi wa wanafunzi hao.
Wakizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika ofisi za Chama cha Wananchi (CUF), Buguruni jijini Dar es Salaam, viongozi hao walisema kuwa wameguswa sana na mateso ambayo wanafunzi hao wanapitia kutokana na kiu yao ya kupata elimu.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alitangaza kuwa umoja huo wa wapinzani umechanga sh milioni moja kwa kuanzia, na watafungua akaunti ya benki, ili wasamaria wema wengine wanaopenda kuwasaidia wanafunzi hao, wachangie.
Profesa Lipumba alisema fedha hizo ni mchango wa dharura kwa ajili ya kuokoa maisha ya Watanzania hao ambao imeelezwa kwa muda wa siku kadhaa sasa, hawana hata makazi maalumu.
Habari zinasema kuwa licha ya kufukuzwa shuleni na pia katika hosteli walizokuwa wanaishi baada ya kushindwa kulipia gharama zake, wanafunzi hao wamezuiliwa kurudi nyumbani hadi watakapolipa fedha wanazodaiwa.
“Watanzania tuwe na huruma, tunaomba kila mmoja atoe mchango wake kupitia namba ya akaunti ambayo itatangazwa baadaye. Fedha hizi si za chama, ni kwa ajili ya kuwasaidia wananfunzi hao wanaoteseka… lengo letu ni kuwasaidia aidha waendelee na masomo au waweze kurudi nyumbani,” alisema.
Profesa Lipumba aliitaka serikali kufahamu kuwa maisha ya dhiki ambayo wanafunzi hao wanaishi yanaweza kuwasababishia mauti na kwamba si ufahari kupokea maiti za Watanzania wanaoishi nje.
Profesa Lipumba alionyesha kushangazwa na wanafunzi hao kususwa na serikali hivi sasa wakati walipoondoka mwaka jana walipewa baraka zote na serikali hiyo hiyo na kuahidiwa kupelekewa fedha za ada kupitia mfumo wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
“Inashangaza kuwa sasa serikali inawakana wanafunzi hao na kusema kuwa haiwatambui,” alisema baada ya kubainisha kuwa juhudi za wanafunzi hao kuwasiliana na Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia hazikuweza kuwapatia ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili.
Profesa Lipumba alidai kuwa wanafunzi hao walifikia hatua ya kuwasiliana na waziri wa wizara hiyo, Profesa Peter Msolla, lakini akadai kuwa waziri huyo amekuwa akikata simu kila wanapompigia.
Alisema katika jitihada za kuwasaidia watoto wao ambao wapo mbali, wazazi wa vijana hao waliwasiliana na viongozi wa Bodi ya Mikopo na wizara husika, lakini jitihada hizo nazo zimegonga mwamba baada ya maofisa katika ofisi hizo kushindwa kutoa ushirikiano wa kutosha.
“Inasikitisha kwa sababu hakuna hata ofisa mmoja wa serikali aliye tayari kusema wazi msimamo wa serikali kuhusiana na wanafunzi hao… wazazi wamekuwa wakipigwa danadana kama mpira kutoka ofisi moja hadi nyingine bila mafanikio yoyote,” alisema.
Akielezea jitihada za wanafunzi hao, alisema baada ya kushindwa kwa Waziri Msolla, walimpigia simu Waziri Mkuu ambaye naye hakuweza kuwasaidia na mwisho wakaamua kuwasiliana na Rais Jakaya Kikwete.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Profesa Lipumba, Rais Kikwete aliurudisha mpira huo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo, Nimrod Mkono na Waziri Msolla, na kuwataka wanafunzi hao wawasiliane na maofisa hao.
Mbali na hilo, Profesa Lipumba alisema wamepata habari kuwa Ubalozi wa Uingereza nchini Ukraine, ulisema uliipa Serikali ya Tanzania ofa ya kuwasaidia kuwalipia vijana hao na kuwapa misaada mingine ya kibinadamu endapo tu Serikali ya Tanzania itaandika barua ya kuahidi kurudisha fedha hizo kwa Serikali ya Uingereza, lakini serikali haijatoa jibu lolote hadi leo.
Alisema habari walizonazo ni kuwa wanafunzi hao walilazimika kujisalimisha katika Ubalozi wa Uingereza uliopo mjini Kiev, kuomba msaada wa hifadhi baada ya kutimuliwa katika hosteli walizokuwa wamepanga. Alisema vijana hao wapo ubalozini hapo kwa muda wa siku 14 hivi sasa.
“Mbali na kusimamishwa masomo, wanafunzi hao kwa sasa wamepewa hadi Mei 29 mwaka huu kulipa fedha wanazodaiwa vyuoni, la sivyo watanyang’anywa hati zao za kusafiria na kisha kufukuzwa kwenye mabweni wanamoishi, pia hawaruhusiwi kurejea nchini hadi walipe madeni wanayodaiwa," alisema Profesa Lipumba.
Alisema ukiondoa wanafunzi wa Ukraine, kuna wanafunzi wengine nchini Cuba, na Urusi ambao wana matatizo yanayolingana na hayo.
Alisema matatizo kama hayo yanatokea kutokana na Bodi ya Mikopo kuwa na sera za kibaguzi dhidi ya nchi zinazofuata siasa za kijamaa.
Profesa Lipumba alisema ingempasa Waziri Msolla kujiuzulu kutokana na matatizo lukuki yanayoikabili wizara hiyo, lakini imekuwa ni utamaduni wa viongozi wa Tanzania kutowajibika.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, alionyesha mshangao wake kwa msimo wa serikali kutokuwa na huruma na wananchi wake.
Alisema inashangaza kuona kuwa hata Rais Kikwete hajalizungumzia suala hilo, licha ya kushindwa kutoa msaada kwa wanafunzi hao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema kwa sasa watalizungumzia suala hilo kama wazazi ambao wameonyesha kuumizwa nalo na si kama wapinzani, ili wanafunzi hao waweze kupata misaada ya kutosha kutoka kwa wahisani mbalimbali.
Akizungumza huku akibubujikwa machozi, mmoja wa wazazi wa wanafunzi hao aliyejitambulisha kwa jina la Isais Magombana, ambaye mtoto wake Isabela Magombana naye amekwama Ukraine, alisema wanashangazwa na serikali kuwageuka na kuvunja mkataba waliofikia nao mwanzoni na kuwasababishia watoto wao adha kubwa ughaibuni.
Mzazi mwingine, Elinipa Sonda, alisema kuwa ametaarifiwa na mtoto wake, Adam Yusuph ambaye yupo Ukraine, kuwa walilala nje ya bweni kwa muda wa wiki mbili kabla ya kwenda ubalozini kuomba msaada baada ya kutishiwa kunyang’anywa hati zao za kusafiria.