HABARI kubwa katika gazeti hili leo, inahusu kujitokeza kwa wanasiasa wakongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuchukua fomu za kuwania ngazi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.
Kama ilivyotarajiwa, tayari baadhi ya wagombea wameanza kulalama kuwa mizengwe na mbinu nyingine chafu zimeanza kutumiwa na baadhi ya washindani wao kuwachafua.
Malalamiko haya yametolewa tangu uchukuaji fomu ngazi za mashina, matawi na kata ulipoanza, na kama ilivyo desturi ya chama hicho ya kumaliza migogoro ya wanachama wake kwa njia ya vikao vya ndani, tayari baadhi ya tume zimekwishaundwa kufuatilia baadhi ya malalamiko yaliyotolewa.
Hata hivyo, tofauti na malalamiko ya kuchezeana rafu, ambayo yamekuwa ya kawaida katika kila uchaguzi wa chama hicho, malalamiko yanayotolewa na baadhi ya wagombea safari hii yanaonekana kuwa mazito zaidi.
Uhasama wa kisiasa uliojengeka kipindi cha kura za maoni wakati wa kuwania kuteuliwa wagombea wa mwaka 2005, unaonekana kuwa wa kudumu baina ya walioshinda na walioshindwa.
Ingawa viongozi wakuu wa chama hicho wamekuwa wakipinga mara kwa mara kuweko kwa makundi yenye upinzani mkali wa kisiasa ndani ya chama hicho, malalamiko yanayotolewa sasa na wanaCCM wanaokanyagana kuwania uongozi katika chama hicho, yanadhihirisha pasipo shaka kuwa kuna makundi.
Si kazi yetu kujadili makundi yanayowindana usiku na mchana, kila moja likitumia njia zinazofaa na zisizofaa kuchafua kundi jingine, kisa kikiwa kutaka ukubwa.
Lakini ni wajibu wetu kusema pale tunapoona dosari yoyote inayaokwenda kinyume cha taratibu za mwenendo wa kawaida wa uchaguzi, si kwa CCM tu, bali kwa chama chochote cha siasa au muungano wa aina yoyote.
Tumelisema hili mapema, wakati CCM kikiwa kingali katika uchaguzi wa ngazi za chini baada ya kuona msururu wa wanasiasa wakongwe wa CCM wanaojitokeza kuchukua fomu za uongozi.
Kilichotusukuma kulisema hili la mchezo mchafu, ni historia iliyoandikwa mwaka 2005 ambapo makundi ya wagombea ndani ya chama hicho yaliendesha siasa za kuundiana kashfa na kuchafuana, jambo lililosababisha baadhi ya watu wenye sifa zinazostahili kuwa viongozi, kukosa nafasi hizo.
Mvutano mkali unaoendelea sasa baina ya mafahari wawili, Dk. Harisson Mwakyembe ambaye ni Mbunge wa Kyela na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, ambao ulimlazimu Dk. Mwekyembe kufikisha malalamiko yake mbele ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, hivi karibuni, ni dalili kwamba yaliyotokea mwaka 2005, sasa yanatokea tena.
Aidha, kuibuka kwa Frederick Sumaye ambaye alitangaza kustaafu siasa baada ya serikali ya Awamu ya Tatu kuondoka madarakani na kuamua kwenda zake Marekani kusoma, ni dalili nyingine za kuibuka kwa ushindani mkali wa kuwania madaraka katika chama hicho.
Kitendo cha Sumaye kurejea tena ulingoni, kimetupa picha kwamba bado anao mtandao wake ndani ya CCM na bila shaka ndio utakuwa mhimili wake mkubwa katika adhima yake hiyo ya kuwania nafasi anayoitaka.
Kwa sababu hiyo, kile ambacho kimekuwa kikikanushwa na viongozi wakuu wa CCM kuwa hakuna makundi ndani ya chama baada ya uchaguzi kuisha, sisi tunadhani kuwa kipo.
Na iwapo CCM yenyewe haitakiri ukweli huo, hatari ya kuharibika kwa mwenendo wake wa mambo katika siku za usoni ni kubwa, na itakapofikia hatua hiyo, itakuwa vigumu kukirejesha chama katika hali yake ya kawaida ya siasa za kistaarabu.