UAMUZI wa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, wa kuchukua fomu za kusaka ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), umetafsiriwa kuwa ni hatua yake ya pili ya kujipanga upya kwa ajili ya madaraka makubwa zaidi ndani ya chama hicho.
Habari ambazo Tanzania Daima Jumapili imezipata kutokana na mazungumzo ya makada mbalimbali wa chama hicho, na kutoka miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, zinaonyesha kuwa, hatua hiyo inaonyesha kwamba, mwanasiasa huyo bado ataendelea kubakia kilingeni katika kipindi kirefu kijacho.
Vyanzo kadhaa vya habari vinaiona hatua hiyo kuwa ni jitihada ya pili ya mwanasiasa huyo kujipanga upya baada ya ile ya kwanza ya kwenda nje ya nchi kusomea shahada ya uzamili katika masuala ya kiuongozi.
Sumaye, waziri wa tisa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye keshokutwa atatimiza umri wa miaka 57, kwa muda mrefu tangu aliposhindwa kuteuliwa na chama chake kuwa mgombea urais, amekuwa akielezwa kuwa na malengo ya kuhakikisha anashika moja ya nafasi mbili za juu katika chama hicho.
Lakini Februari Mosi 2006, wakati anawaaga waandishi wa habari tayari kwenda Marekani kuanza masomo ya shahada ya uzamili ya masuala ya uongozi katika chuo cha John F. Kennedy kilichopo chini ya Chuo Kikuu cha Harvard, alidai kwamba: “Nimekuwa Waziri Mkuu kwa miaka kumi, lakini kwa kuwa CCM ina taratibu zake, siwezi kupingana.
“Nakwenda masomoni. Na hata baada ya miaka kumi ya utawala wa Rais Kikwete (Jakaya), tayari nitakuwa na umri wa miaka 65, katika umri huo nitakuwa na ndoto za urais?” aliwahi kuhoji Sumaye akiwa nyumbani kwake Kiluvya, Kibaha, mkoani Pwani.
Lakini uamuzi wa Sumaye umezua minong’ono zaidi, kiasi cha kuonekana mwenye dhamira ya kujipenyeza zaidi ndani ya chama.
Inaelezwa kwamba, Sumaye anautaka kwa udi na uvumba Umakamu Mwenyekiti wa CCM, nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na kiongozi mkongwe, lakini mwenye nguvu kubwa za kisiasa ndani ya CCM, John Samuel Malecela, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, achilia mbali nafasi nyingine nyeti za ndani na nje ya nchi.
Malecela aliyezaliwa miaka 73 iliyopita huko Bugiri, Dodoma, ingawa anaonekana kuchoka kiumri, bado ni tegemeo ndani ya CCM katika siasa na amekuwa akitumiwa zaidi kurekebisha mambo, pale ambapo mambo yanaonekana kuwa magumu kwa chama, hasa katika chaguzi ndogondogo.
Hata hivyo, dhamira ya Sumaye, Waziri Mkuu aliyekaa madarakani kwa miaka kumi, ukiwa ni muda mrefu zaidi kuliko Waziri Mkuu mwingine yeyote aliyemtangulia, huenda ikakumbana na dhoruba, kwani siku moja baada ya kujitokeza kuwania ujumbe wa NEC, wakubwa wengine wa chama na serikali, wametangaza kuwania nafasi hiyo.
Hao ni pamoja na Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Yussuf Makamba, Katibu Mkuu wa CCM ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Katibu Mkuu, Ofisi Ndogo ya CCM ya Lumumba, Dar es Salaam, Lowassa na Makamba watachukua fomu za kuwania ujumbe wa NEC kesho.
Mbali ya Lowassa na Makamba, wengine wanaoonekana kumpima ubavu Sumaye aliyeingia madarakani Novemba 28, 1995 akimrithi Cleopa Msuya, ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia ni Mbunge wa Urambo, Profesa Juma Kapuya na Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Salum Londa.
Pia yumo Brigedia Jenerali mstaafu, Hassan Ngwilizi ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Taifa.
Wafuatiliaji wa mambo ya kisiasa ndani ya CCM, wamekuwa wakimhusisha Sumaye na nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, kwa kuwa haijawekwa bayana iwapo Malecela ataamua kujiuzulu madaraka ya kichama au atafanya jitihada za kupigania kiti chake.
Hata hivyo, bado suala la nani anaweza akawa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara linaweza likaendelea kubakia kuwa kitendawili, kutokana na ukweli kwamba, nafasi hiyo huwa haigombewi.
Pamoja na ukweli huo, uamuzi wa Sumaye ambaye mwaka 2001 katika kinyang’anyiro cha NEC alipata kura nyingi hata kusababisha kuibuka kwa maneno mengi, kuamua kuchukua fomu akipitia Dar es Salaam, ni ushahidi mwingine kwamba mwanasiasa huyo bado hajakata tamaa ya kuendelea kukitumikia chama hicho kiuongozi.
Kwa sababu hiyo, iwapo ataweza kuwabwaga vigogo wengine kadhaa ambao atachuana nao kusaka nafasi moja ya Mjumbe wa NEC kutoka Dar es Salaam, basi atapata fursa ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kusaka viongozi wa ngazi mbalimbali ndani ya chama hicho katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Kwa upande mwingine, uamuzi wake wa kuamua kusaka nafasi ya ujumbe wa NEC kupitia Dar es Salaam na si kutokea Arusha au Manyara, unaonyesha dhamira yake ya kutokuwa tayari kukabiliana ama na Waziri Mkuu Edward Lowassa na mawaziri wengine ambao kwa namna yeyote ile watakuwa wakichuana kuchukua fomu kupitia mikoa hiyo.
Mbali ya Sumaye, zoezi la uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali katika NEC linakirejesha chama hicho tawala, katika vita nyingine kali ya kisiasa, ambayo imekuwa ikitokea kila mara unapofika wakati huu.
Mkoani Iringa, Waziri wa Elimu ya Juu, Profesa Peter Msolla, amejitosa kuwania ujumbe wa NEC, kumpinga anayeshikilia nafasi hiyo, Joseph Mungai ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani.
Lakini duru za kisiasa mkoani humo zinaonyesha kwamba, licha ya umri wa miaka 64 alionao, Mungai ambaye ni mchumi na mtawala aliyesomea chuo alichotoka Sumaye majuzi, ana mvuto kisiasa mkoani Iringa kuliko Msolla, ambaye pamoja na kuwa na umri wa miaka 62, anaonekana kuwa bado ni mchanga kisiasa. Alijitosa katika siasa mwaka 2005, akitokea Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) ambako alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo.
Mungai alichukua fomu jana, ikiwa ni siku moja baada ya Profesa Msolla kuchukua, pengine kwa dhamira ya kweli au kwa kutaka kumpima upepo Mungai ambaye kwa mara ya kwanza alikuwa waziri mwaka 1972, akianzia Wizara ya Kilimo.
Mkoani Mbeya kwa mfano, kiti cha uwakilishi wa NEC hivi sasa kitakuwa kikigombewa na wanasiasa wawili, Profesa Mark Mwandosya, Waziri anayeshughulikia mazingira ambaye ndiye mjumbe wa NEC anayemaliza muda wake mkoani humo na Thomas Apson, mbunge kijana wa kuteuliwa na rais.
Uamuzi wa wanasiasa hao kupigania kiti hicho, umesababisha kwa miezi kadhaa sasa mkoa huo kuwa katika hali ya mvutano mkubwa kisiasa, ambayo inajengwa na mashabiki wa wanasiasa hao wawili wenye ushindani mkali.
Hadi kufikia jana, habari ambazo Tanzania Daima ilikuwa imezipata zilikuwa zikionyesha kuwa, jumla ya watu 27, yakiwamo majina makubwa, walikuwa wamechukua fomu za kugombea ujumbe huo wa NEC.
Akizungumza katika ofisi zake Katibu wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kapteni John Barongo aliwataja watu waliochukua fomu kuwa ni Hemed Mkali, ambaye anagombea nafasi ya Mwenyekiti Mkoa huo anayoishikilia hadi hivi sasa.
Mwingine ambaye amechukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo ni, John Guninita ambaye alishawahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Mbali ya Sumaye, Profesa Kapuya, Ngwilizi na Londa wanaovutana NEC, Nape Nnauye, Anastazia Rugaba, Zainabu Kawawa, Ashura Abubakar na Sixtus Mapunda nao wamechukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi ya NEC kwa tiketi ya vijana.
“Nafasi ya Katibu Siasa na Uenezi (Salim Mwakinginda), Katibu Uchumi na Fedha (Salim Dossi) ambaye pia amechukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi ya Mjumbe NEC kupitia Wazazi ambapo katika nafasi hii Zahoro Madeni alichukua fomu,” alisema Barongo.
Kimwana Sherally, Mwadawa Lugongo, Moses Kabambala, Regina Chonjo, Jacob Mbawala ni kati ya waliojitokeza kugombea nafasi ya ujumbe wa NEC. Nafasi nyingine ya NEC Mjumbe wa Mkutano Mkuu Mkoa, inawaniwa na Shaaban Chanda.
Kutoka Arusha, Mwandishi Wetu anaripoti kwamba, wakati wakubwa wengine wakichuana kuwania madaraka ndani ya chama tawala, Mjumbe wa NEC mkoani humo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Daniel ole Njoolay, ametangaza kutoitetea nafasi yake.
Uamuzi wa aina hiyo umechukuliwa pia na Mwenyekiti wa CCM mkoani Arusha, Yona Nnko.