*Afungua nyingine kutaka arejeshewe kesi ya mauaji
*Adai ushahidi unaonyesha aliua kwa makusudi
Na Nora Damian
MWENYEKITI wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amefungua kesi ya katiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akiomba mahakama hiyo ifungue upya kesi ya kuua bila kukusudia inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Ukiwaona Ditopile Mzuzuri ili iwe ya kuua kwa kukusudia.
Kesi hiyo namba 41 ilifunguliwa jana katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam majira ya saa 6.30 mchana na Mtikila mwenyewe.
Kesi hiyo imewasilishwa mahakamani hapo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika kesi hiyo, Mtikila ameomba mahakama imruhusu kumshtaki binafsi Ditopile badala ya DPP na aliwasilisha hoja 17 akitaka kesi hiyo ifunguliwe upya, na maafisa wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mahakama Kuu wachukuliwe hatua za kisheria kwa kuzuia haki isitendeke.
Pia, ameiomba Mahakama Kuu iwachukulie hatua za kisheria waliokuwa walinzi na wasindikizaji wa Ditopile ambao walishiriki kudharau Mahakama ya Kisutu na Mahakama Kuu kwa kitendo cha kuwazuia na kuwapiga waandishi wa habari na kuwasababishia maumivu.
Mtikila pia anaiomba mahakama hiyo iendeshe kesi hiyo mpya aliyofungua kupitia wakili wa kujitegemea.
Katika hati aliyowasilisha mahakamani hapo, Mtikila ameitaka mahakama ilinde katiba na sheria za nchi dhidi ya Ditopile kutokuchukuliwa sheria kutokana na mauaji aliyoyaita ya kinyama aliyoyafanya Novemba 4, mwaka
jana alipomuua dereva wa daladala, Hassan Mbonde.
Katika hati hiyo, Mtikila amelalamika kuwa Ditopile alipewa dhamana kinyume cha sheria kwa kubadilisha mashtaka ya mauaji na kuwa mashtaka ya kuua bila kukusudia.
Alieleza kuwa katiba ya nchi inawataka maafisa wa mahakama, DPP na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kufuata sheria na kwamba katiba inamruhusu kufungua kesi ya kulinda katiba kama akiona inavunjwa.
Ameongeza kuwa pamoja na Mahakama ya Kisutu kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji isipokuwa kusikiliza maelezo ya awali, lakini ilishindwa kumtafuta shahidi wa kwanza aliyekuwa katika tukio kwa lengo la kuzuia haki isitendeke kwa kutotumia ushahidi wa shahidi huyo.
Alidai kuwa kutotumiwa kwa shahidi huyo ni njia mojawapo iliyotumika kubadilisha shtaka la mauaji na kuwa la kuua bila kukusudia.
Alieleza kuwa kesi ya kuua bila kukusudia hutokea kwa bahati mbaya lakini Ditopile alifanya makusudi kwa kuteremka ndani ya gari lake huku akitoa maneno ya vitisho, "Nimeshaua mbwa wengi kama wewe kwa hiyo sioni shida kukumaliza ukifanya kiburi" alinukuu maneno aliyodai ni ya Ditopile aliyoyasema kabla ya kufanya mauaji hayo.
Mtikila aliendelea kudai kuwa Ditopile alifanya mauaji hayo akiwa na akili zake timamu na akiwa na malengo ya kuua kwa sababu alifyatua risasi mbili, jambo ambalo linaonyesha si la bahati mbaya.
Katika hati hiyo Mwenyekiti huyo DP, aliongeza kuwa Kapteni huyo mstaafu wa jeshi ni sawa na binadamu wengine kwa hiyo asipewe upendeleo wowote kuliko watu wengine kwani kufanya hivyo ni kinyume cha haki na katiba ya nchi.
Pia alidai kuwa Ditopile amepewa upendeleo akiwa gerezani na kutolewa usiku akiwa kama mahabusu na kupelekwa Ikulu kwa kupewa ulinzi, jambo ambalo liliwapa jeuri walinzi na wapambe wake hata kufikia hatua ya kuwapiga waandishi wa habari na kuwazuia kufanya kazi zao.
Alieleza kuwa ili haki ya katiba iweze kutendeka, mshtakiwa Ditopile arudishiwe shtaka lake la awali la mauaji na DPP azuiwe kuendesha kesi hiyo kwa sababu ndiye aliyebadilisha shtaka la mauaji kuwa la kuua bila kukusudia.
Mapema Mtikila aliingia katika viwanja vya Mahakama Kuu akiwa ameongozana na mashahidi wanne waliokuwa eneo la tukio, ambao hawakujumuishwa katika ushahidi dhidi ya Ditopile.
Mashahidi hao ni Thomas Mwita, Mmiliki wa daladala na aliyekuwa Kondakta kwenye gari hiyo, Masasi Lwenge aliyekuwa abiria katika gari hiyo mkono wa kushoto karibu na kiti cha marehemu na Edward Gervas anayedai alikuwa ni dereva msaidizi wa marehemu.
Mtikila alieleza kuwa pamoja na kufungua shauri hilo mwenyewe, lakini pia atasaidiana na mawakili 10 mara kesi hiyo itakapoanza kuunguruma.