Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  TRA yaikana Barrick kuhusu mchanga wa dhahabu
TRA yaikana Barrick kuhusu mchanga wa dhahabu
By Habari Tanzania | Published  05/26/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

Na Jackson Odoyo


KAMPUNI  ya kuchimba dhahabu ya Barrick Gold, ikidai  kuwa ndiyo iliyosababisha makontena yake ya mchanga wa dhahabu yakaguliwe bandarini, Mamlaka ya Mapato  (TRA) imepingana nayo na kusema kuwa ilifanya hivyo yenyewe baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

Akizungumza na Mwandishi kwa njia ya simu jana, Kamishna wa Kodi ya Mapato, George Lauwo, alisema TRA inazifanyia uchunguzi sampuli za michanga zinazodaiwa kuwa na dhahabu nyingi kinyume na ilivyotarajiwa na kwamba itatoa matokeo ya uchunguzi huo hivi karibuni.

"Kwa sasa tunazifanyia kazi sampuli za mchanga unaodaiwa kuwa na dhahabu ndani yake na kazi hii itakapokamilika, siwezi kutaja tunafanyia wapi uchunguzi, lakini itakapokamilika muda si mrefu tutatoa matokeo ya uchunguzi wetu," alisema.

Lauwo alisema walipewa taarifa na wananchi wenye mapenzi mema na nchi yao kuwa kuna makontena yenye michanga inayodaiwa kuwa na dhahabu, yanayosafirishwa kwenda nchi za nje na hivyo kuikosesha nchi mapato.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo, kwa kushirikiana na vyombo vya usalama, waliamua kwenda kuufanyia upekuzi na kuchukua sampuli ya mchanga huo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Alisema sio kwamba walipewa taarifa na Kampuni inayomiliki mgodi wa dhahabu ya Barrick Gold, bali walishirikiana nao katika upekuzi na kwamba makontena hayo bado yapo hapa nchini mpaka hapo watakapotoa taarifa ya uchunguzi wao.

"Tulipewa taarifa na Watanzania wenye mapenzi mema na nchi yao na tukashirikiana na vyombo vya usalama pamoja na kampuni ya Barrick kufanyia upekuzi makontena yote yaliyokuwa yanadaiwa kuwa na michanga hiyo ya dhahabu na tukachukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi zaidi na mara baada ya kumaliza uchunguzi tutatangaza," alifafanua Lauo.

Hata hivyo Lauwo alisema kwamba kwa miaka kadhaa sasa, michanga hiyo hupitishwa bandarini hapo, lakini michanga hiyo huwa haina dhahabu kama ilivyodaiwa na ndiyo sababu wakaamua kuufanyia uchunguzi ili kufahamu ni mchanga wa aina gani.

Alisema mchanga uliokuwa unapitishwa hapo awali ni ule uliokuwa umeshasafishwa na hauna mabaki ya dhahabu lakini baada ya kupata taarifa hizo, walishtuka na ndipo wakaanza kazi ya upekuzi mara moja .

Wiki iliyopita Mamlaka ya Mapato ikishirikiana na vyombo vingine vya usalama vilifanya ukaguzi huo wa ghafla chini ya ulinzi mkali katika ghala ya Mofed lililopo katika eneo la Kurasini katika Bandari ya Dar es Salaam.

Ukaguzi huo wa kushtukiza ulikuja muda mfupi kabla ya kusafirishwa kwa makontena hayo, baada ya raia wema kutoa taarifa juu ya kuwa na mashaka na mchanga huo na kuwepo kwa njama za kusafirisha dhahabu kwenda nje ya nchi kuwa zinafichwa katika mchanga huo.

Ukaguzi wa makontena hayo yanayohifadhiwa katika ghala hilo lililopo chini ya Serikali ya Zambia, ambayo vyanzo vya habari viliieleza Mwananchi kuwa ulitakiwa kusafirishwa mapema wiki iliyopita, ulifanyika kwa kushtukiza mwishoni mwa wiki iliyopita, ikiwa ni dakika za mwisho kabla ya kusafirishwa kwake.

Mchanga huo wa dhahabu ulishuhudiwa awali na waandishi wa habari hizi, ukiwa umehifadhiwa kwa kiasi cha robo kontena, kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nchi za Ulaya, China na Japan kwa ajili ya kusafishwa na kutoa kiasi cha madini ya dhahabu kilichobaki ndani ya mchanga huo.

Ukaguzi huo ulioanza saa 7.00 mchana hadi saa 11.00 jioni, uliambatana na kukatwa kwa lakiri (seal) za makontena hayo yaliyokwishafungwa na kuchukuliwa kwa sampuli za mchanga katika makontena yote yaliyokutwa katika ghala hilo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

Makontena hayo ya Kampuni hiyo ya Barrick ya Canada inayomiliki machimbo ya dhahabu ya Bulyanhulu na kusafirishwa na kampuni ya Maersk Line kwa kushirikiana na wakala wa Freight Forwaders Tanzania Limited, sasa yatalazimika kusubiri hadi hapo ukaguzi wa sampuli hizo utakapokamilika.

Mwananchi lilifika na kushuhudia sehemu ya ukaguzi huo na kushuhudia makontena matano yakiwa na mchanga ukiwa na mchanganyiko wa rangi nyeusi na kahawia.

Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, zaidi ya makontena 45 ya mchanga wa dhahabu kutoka machimbo ya dhahabu ya Bulyanhulu, Kahama, mkoani Shinyanga, yalifanyiwa ukaguzi kwa kushtukiza baada ya kudhaniwa kuwa na dhahabu ghafi badala ya mchanga kama ilivyodaiwa.

Baada ya taarifa hizo kuripotiwa na Mwananchi, kampuni ya Barrick kupitia vyombo mbalimbali imekuwa ikitoa taarifa tofauti kuonyesha kuwa yenyewe ndiyo ilizuia makontena hayo kusafirishwa ili yakaguliwe kubaini kama mchanga wake umeibwa katika mikoa ya kanda ya ziwa kabla ya kufika Dar es Salaam.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.