Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Dhehebu la kuua watu latua nchini
Dhehebu la kuua watu latua nchini
By Marshy Abdu | Published  05/25/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
Dhehebu la kuua watu latua nchini
na Jovin Mihambi


BAADA ya kuwapo kwa maneno ya chinichini yasiyo na ushahidi wa moja kwa moja ya muda mrefu, hatimaye sasa siri imeanza kufichuka kuwa Tanzania imeingia katika orodha za nchi zilizo na madhehebu ya dini yanayotoa kafara za damu za binadamu.

Taarifa za awali zinaonyesha kuwa, dhehebu moja linalojihusisha na utoaji wa kafara ya watu limeshasambaa katika mikoa mitano ya Mwanza, Mara, Morogoro, Arusha na Dodoma.

Hayo yamebainishwa kutokana na uchunguzi ulioanzia mkoani Mwanza, ambako tayari Jeshi la Polisi mkoani humo sasa linamshikilia muumini wa dhehebu hilo lijulikanalo kwa jina la Faraja.

Taarifa zinaonyesha kuwa, mbali ya dhehebu hilo kutoa kafara watu, hususan watoto vipenzi vya waumini wake, misa huendeshwa wakati waumini wote wakiwa watupu, pasipo mavazi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Zelothe Stephen, alithibitisha kukamatwa kwa mtu mmoja anayetuhumiwa kuwa muumini wa kanisa hilo aliyemtaja kwa jina la Yunus Simon.

Kwa mujibu wa Kamanda Stephen, mtuhumiwa huyo ambaye bado anaisaidia polisi katika kuendesha uchunguzi wake, amefunguliwa jalada katika Kituo Kikuu cha Polisi Mwanza, lenye namba MWS/IR/796/07.

Taarifa za polisi mkoani Mwanza kulibaini dhehebu hilo lililopo katika maeneo ya Butimba, zimekuja takriban miezi miwili tangu gazeti hili liandike kwa mara ya kwanza kuhusu kuwapo kwa kanisa la aina hiyo mkoani hapa.

Kukamatwa kwa muumini huyo, kunahusishwa pia na kupatikana akiwa amefichwa kwa mama mmoja ndani ya kanisa hilo, aliyetajwa kwa jina la Marium Pius, akionekana kuwa katika hali ya kupagawa na kurukwa na akili baada ya kushawishiwa kujiunga na kanisa hilo.

Polisi hao bado wanachunguza madai yanayomhusisha muumini Simon kuwa ndiye mtu aliyemshawishi mama huyo kujiunga na dhehebu hilo, ili siku moja yeye na mwanawe ajulikanaye kwa jina la Angel Michael (5), watolewe kafara.

Kwa mujibu wa Kamanda Zelothe, baada ya uchunguzi wa awali wa polisi kumtia hatiani mtuhumiwa huyo dhidi ya tuhuma hizo za awali, jeshi lake sasa linaendelea kuwasaka waumini wengine wa kanisa hilo, linaloendesha ibada zinazokwenda kinyume cha maadili ya kiutu.

Kuhusu kupatikana kwa mwanamke huyo, Kamanda Stephen alisema tayari walikuwa wameshamkabidhi kwa ndugu zake walioko Magu, nje ya Jiji la Mwanza ambako anapatiwa matibabu.

Mume wa mwanamke huyo, Michael Laurent, aliliambia gazeti hili kuwa wazazi wa mwanamke huyo walikataa kumpeleka hospitali ili apatiwe matibabu na badala yake wakampeleka kwa waganga wa kiasili, kwa madai kwamba nguvu za giza ndizo zitaweza kumponya.

Aidha, uchunguzi wa muda mrefu wa gazeti hili umebaini kuwa, waumini wa dhehebu la Faraja, lenye makao yake eneo la Butimba B, kwenye barabara iendayo Chuo cha Ualimu cha Butimba, hufanya maombi yao nyakati za usiku.

Akizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, mmoja wa waumini aliyelikimbia kanisa hilo, alidokeza kuwa, inapofika wakati wa maombi katika ibada ambayo hufanyika usiku, waumini wote hutakiwa kuvua nguo na kubaki uchi wa mnyama.

Alisema unapowadia wakati huo, watoto waliopo hutolewa nje na waumini wakishavua nguo zao, huendelea kusali na kuimba.

Kwa kawaida, watoto ambao huambatana na mama zao kwenye ibada, hutunzwa katika chumba kingine kanisani hapo, na wengine hupelekwa katika nyumba za waumini na kupatiwa huduma zote, ikiwamo chakula.

Alisema kuwa imani ya kanisa hilo inawataka watu waliooana kuachana na kumfuata Yesu. Aidha, familia ikiwa ina mtoto ambaye wanampenda sana, hulazimishwa wamtoe kafara ili kuonyesha kuwa wanampenda Mungu zaidi ya mtoto huyo.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, baadhi ya watoto ambao wazazi wao wameachana kutokana na imani ya kanisa hilo, wamehamishiwa katika vituo mbalimbali, ambavyo ni wakala wa kanisa katika mikoa ya Morogoro, Arusha, Mara na Dodoma.

Kwa upande wake, Laurent aliliambia gazeti hili kuwa, mke wake alirubuniwa na mmoja wa waumini katika kanisa hilo na kuondoka na mtoto huyo na baadaye kuishi katika kanisa hilo pamoja na waumini wengine.

Baada ya kufuatilia ili ampate mtoto wake, alielezwa na baadhi ya waumini kuwa mama huyo kwa sasa hayupo na amehamishiwa katika mkoa mwingine ambao hawakuutaja.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.