*Wahariri wakuu waanzisha chombo chao
Na Mwandishi Wetu
WAHARIRI wakuu na waandishi wa habari nchini wametakiwa kuwa jasiri na kuwabana wamiliki wa vyombo vya habari, ili wawape maslahi bora.
Mwito huo ulitolewa jana Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Bw. Reginald Mengi, katika hafla ya uzinduzi wa Jukwaa la Wahariri.
"Tubaneni tuwalipe vizuri, mnatarajia mmiliki aamke tu asubuhi na kusema nakuongezeni mshahara mara mbili au asilimia 50, ana kichaa!...kila mfanyabiashara nia yake ni kupata faida...msipochangamka mkatubana mtabaki hivyo hivyo," alisema Bw. Mengi.
Pamoja na hilo, Bw. Mengi aliwapongeza wahariri kwa kuanzisha Jukwaa hilo, ambalo ni umoja wa wahariri, wenye lengo la kuwalinda wao na sekta yote ya habari nchini, lakini pia ni mahali ambapo watakutana na kujadili masuala mbalimbali ya kitaaluma na maslahi ya nchi.
"Nawapongeza kwamba wazo la kuwa na chombo chenu kama wahariri sasa limetimia ingawa limechukua muda mrefu, hapa ni mahali pazuri pa kutetea maslahi yenu, lakini pia mkitukosoa sisi, mkikosoana ninyi pamoja na kuhakikisha maslahi ya Watanzania yanapewa kipaumbele," alisema Mwenyekiti wa MOAT, ambaye pia ni mmiliki wa kampuni za IPP.
Mapema akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Uanzishwaji wa Jukwaa hilo, Bibi Sakina Datoo, alisema umoja huo hauanzishwi kwa madhumuni ya kumkandamiza au kumwonea mtu, bali ni kuleta mshikamano na umoja miongoni mwa wahariri na wanahabari kwa ujumla.
Alisema lengo la Jukwaa ni kuisaidia Serikali kupambana na matatizo yanayozuia maendeleo ya wananchi kama vile umaskini, rushwa na mengineyo, lakini pia litatumika kwa wahariri wakuu kukosoana bila kuingilia sera za kila chombo.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Bw. Muhammed Seif Khatib, alisema Serikali imeipokea hatua hiyo kwa dhati kabisa na kuwaasa wanahabari kuendelea kuikosoa kwa kuandika ukweli na kamwe haitataka kuingia katika ugomvi na vyombo vya habari.
Naye Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa Benki ya CRDB, Bi Tully Mwambapa, aliahidi kuwa benki yake ambayo ndiyo iliyodhamini hafla ya jana, itaendelea kulisaidia Jukwaa hilo, ili lisimame imara katika mapambano dhidi ya umaskini na kukuza uchumi kwa kuwa ndiyo dhima kuu ya benki hiyo na waandishi wa habari nchini.
"Tutahakikisha chombo chenu hiki kinakua kwa kuwa majukumu mliyonayo ni sawa na ya kwetu ya kupambana na umaskini, lakini pia tunatambua mchango wenu katika kutiusaidia kuelimisha wateja wetu katika masuala ya kifedha ambayo ni magumu kuyafasiri," alisema.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Bw. Anthony Ngaiza, aliipongeza hatua hiyo, lakini akawataka waandishi na wahariri kuwa huru lakini wawajibike kimaadili na kujijengea heshima yao binafsi na vyombo wanavyoandikia.
Lakini pia aliwataka kuangalia masuala yanayojitokeza yenye maslahi kwa nchi kwa pamoja, lakini akasema kuhusiana na suala la maslahi na kuongezwa mishahara, ni vizuri wamiliki wakaangalia nani aongezwe kulingana na mchango wake.
Mwenyekiti wa MISA TAN, Bw. Ayoub Ryoba, aliwatahadharisha wahariri dhidi kutumiwa na watu kwa maslahi binafsi, akisema imekuwa ikitokea zaidi kwa wanasiasa na matajiri kuwatumia waandishi wa habari kwa maslahi yao huku wakiwaacha hohe hahe.
Jukwaa la Wahariri, ni chombo ambacho kinawaunganisha wahariri wakuu wa vyombo vyote vya habari nchini katika kubadilishana mawazo, uzoefu, kushughulikia masuala mbalimbali ya kitaifa, lakini pia kujenga umoja wa kitaaluma na kimaslahi. Kauli mbiu ya Jukwaa hilo ni Niamini...Mimi ni Mwanahabari.