Na Nickson Mkilanya, Morogoro
MBUNGE wa Gairo, Bw. Ahmed Shabiby, amesema mtindo wa kutoa zawadi ya sh. 5,000 kwa kila aliyetoa taarifa za mtu aliyempeleka mwanafunzi katika nyumba za kulala wageni kufanya mapenzi umesaidia kupunguza idadi ya wanafunzi wanaopata mimba jimboni mwake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi nje ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Morogoro, Bw. Shabiby alisema mbinu hiyo imemsaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kupachikwa mimba.
"Nilifikiria sana, mimi nimelenga kuleta maendeleo katika jimbo langu na maendeleo bila elimu kwa wanawake na wanaume hayatakuwapo, sasa nifanyeje kumaliza tatizo la mimba, ndiyo nikabuni mkakati huo...kila anayemwona mwanafunzi anakwenda gesti ananiletea taarifa, mwishowe nikapunguza tatizo sasa hivi ukisikia mimba Gairo ni kiasi kidogo sana," alisema Bw. Shabiby.
Alisema baadaye wanaume wakware waliacha kuwafuatilia wanafunzi kwa hofu na wanafunzi wa kike kwa upande mwingine, wakawa wanaogopa kukubali matakwa ya wanaume hao, kwani walibaini kuwa wanawindwa muda wote na raia, hususan vijana.
Hata hivyo, alisema wafuatiliaji wa ngono kwa wanafunzi hao walishindwa kumletea majibu halisi, baada ya wasichana kujenga tabia ya kukataa kufanya mapenzi na wanaume, wakiwa shuleni na hivyo walilazimika kuwafuatilia hata walipokwenda sokoni na bombani kuteka maji wakidhani kuwa wanakwenda kwa wanaume.
Alisema kabla ya kuwa Mbunge, wanafunzi wengi walikuwa wakishindwa kuendelea na masomo katika shule za msingi na sekondari chache zilizokuwapo katika jimbo hilo kabla ya kujenga zingine nyingi kwa kushirikiana na wananchi wa jimbo hilo.
Bw. Shabiby alilazimika kuzungumzia suala hilo, baada ya kutolewa taarifa na Ofisa Elimu wa Mkoa wa Morogoro, katika kikao hicho kuwa jumla ya wanafunzi 30 kati ya 80 katika shule moja wilayani Ulanga walipata mimba katika kipindi cha Septemba mwaka jana na Machi mwaka huu.