HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, imetoa notisi kwa wadaiwa sugu wa kodi za majengo wilayani humo, na kuwapa muda walipe deni hilo kabla hatua kali za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na halmashauri hiyo, wadaiwa hao sugu 49, wamelimbikiza madeni ya karibu sh milioni 308.
Miongoni mwa watu wanaodaiwa ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Salum Londa, ambaye anadaiwa sh 1,793,668.
Ofisa Habari wa Manispaa hiyo, Lucy Semindu, alipozungumza na Tanzania Daima jana, alisema iwapo mpaka Juni 30 mwaka huu wadaiwa hao watakuwa hawajalipa madeni hayo, wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.
Kwa mujibu wa Semindu, halmashauri hiyo imekuwa ikiwafuatilia wadaiwa hao na baadhi yao wameweza kulipa, baadhi ya fedha wanazodaiwa.
Alisema endapo wadaiwa hao sugu hawatalipa, manispaa inakusudia kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria ya kodi ya majengo na. 2 ya mwaka 1983 na sheria ndogo ya kodi ya majengo ya halmashauri hiyo ya mwaka 2003.
“Manispaa inakusudia kuwafikisha mahakamani endapo hawatalipa madeni hayo. Imetoa muda mpaka Juni 30 mwaka huu wawe wameshakamilisha au wanaendelea kulipa,” alisema Semindu.
Mbali na Londa, Semindu aliwataja baadhi ya wadaiwa wengine na fedha wanazodaiwa zikiwa kwenye mabano ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba Muhimbili (MUCHS – sh 12,407,026), Shirika la Msalaba Mwekundu (sh 5,347,856), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA sh 6,738,823) na Scandinavia Express (sh 3,089,872).
Wengine ni Shirika la Masoko Kariakoo (sh 18,722,726), Tanzania Postal Corporation (sh 29,840,375), Embassy Hotel (sh 14,681,201), Hospitali ya St. Bernard (sh 2,254,418), Masumin Printways (sh 1,271,126) na Chuo cha Ufundi (DIT) (sh 12,520,362).
Wengine ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF sh 1,617,904), Klabu ya Yanga (sh 6,738,823) na Klabu ya Simba (sh 2,944,533).
Ofisa habari huyo alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wamiliki wa majengo yote endapo wanakusudia kufanya badiliko la umiliki wa majengo waifahamishe manispaa ili jina liweze kubadilishwa.
Alisema pesa hizo zinazolipwa zinasaidia halmashauri katika kutoa huduma mbalimbali kama ujenzi wa shule, barabara na uzoaji taka.