Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Serikali yajitia kitanzi barabara ya Singida
Serikali yajitia kitanzi barabara ya Singida
By Habari Tanzania | Published  05/23/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Peter Nyanje na Restuta James


MPANGO wa serikali wa ujenzi wa barabara kuu nchini, huenda ukachukua muda mrefu kuliko ilivyoahidiwa awali, iwapo mtindo iliouanzisha serikali wa kukubaliana na makandarasi utaendelezwa.

Gazeti hili limebaini kuwa katika moja ya hatua kama hizo, serikali imefikia makubaliano mapya na Kampuni ya Konoike, iliyopewa kandarasi ya ujenzi wa kipande cha kilometa 127 cha barabara kati ya Dodoma na Manyoni.

Mkataba uliokuwa umesainiwa awali baina ya pande hizo, ulitaka ujenzi wa barabara hiyo uwe umekamilika ifikapo Septemba mwaka jana, lakini hadi kufikia sasa, ni kilometa 63 tu ndizo zilizojengwa kwa kiwango cha lami.

Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, jana alilithibitishia gazeti hili kuwa serikali imefikia makubaliano na mkandarasi huyo.

Hata hivyo, alipoulizwa ni makubaliano gani yaliyofikiwa, Chenge alijibu kwa mkato: “Ya ujenzi wa barabara.”

Alipotakiwa kuelezea kilichomo katika mkataba mpya, Chenge alimtaka mwandishi kutembelea eneo la mradi na kujionea mwenyewe kazi inavyoendelea.

Alipoambiwa kuwa mwandishi wa gazeti hili alishatembelea eneo hilo na kuzungumza na mkandarasi ambaye alisema kuwa amekubaliwa kuendelea na kazi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili baada ya kuongezewa kiasi cha fedha, Chenge alikuja na jibu jingine:

“Huo sasa ni umbeya, na kaandike kuwa waziri kasema tunatangaza umbeya… kama ulikwenda eneo la mradi kwa nini usiongee nao ili kupata taarifa?” alihoji.

Alipoambiwa kuwa mkandarasi alitoa taarifa zisizojitosheleza hivyo gazeti limeona ni vyema kutafuta taarifa za uhakika serikalini, Chenge alimtaka mwandishi ampatie taarifa alizozipata katika eneo la mradi kabla yeye hajatoa taarifa alizonazo kuhusiana na makubaliano hayo mapya.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana katika eneo la mradi zinabainisha kuwa Kampuni ya Roughton International inayoishirikisha Kampuni ya Data Consult kusimamia ujenzi wa kipande hicho cha barabara, imeazimia kujitoa katika kazi hiyo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa sharti la kutokutajwa gazetini, wahandisi wa Data Consult walisema Kampuni ya Roughton imefikia uamuzi huo kwa kile wanachodai ni masharti magumu yaliyomo katika makubaliano mapya yaliyofikiwa baina ya serikali na mkandarasi.

Walidai kwamba, masharti yaliyowekwa na serikali kwa Kampuni ya Konoike ni magumu na kwamba wanahofu matokeo yake yatawaumiza iwapo watashindwa kuyatimiza masharti hayo.

“Tulitakiwa kukamilisha kilometa zote 127 Septemba mwaka jana, lakini hadi sasa ni kilometa 63 ambazo zimewekwa lami… na hata hivyo Resident Engineer ameamua kujitoa kutokana na masharti waliyopewa Konoike baada ya kukaa na Wizara ya Miundombinu miezi miwili iliyopita,” kilisema chanzo hicho.

Wakati Kampuni ya Roughton International ikishikilia msimamo huo wa kujitoa, kuna habari kuwa tayari wahandisi wengine wameanza kuondoka na nafasi zao kushikiliwa na watu wengine ambao haijajulikana wanatoka kampuni gani.

“Nafasi ya Resident Engineer inashikiliwa na mhandisi mmoja mwenye asili ya Kenya ila ametokea Uganda, sina uhakika sana na kampuni anayotokea ila tunasubiri hadi Mei 30 ndipo mambo yote yatawekwa hadharani maana wizara ndiyo itakuwa inajua mrithi wa Roughton.

“Unajua tulikuwa tumesimama kwa takriban miezi miwili iliyopita wakati serikali ilipokuwa katika mazungumzo na Konoike kujadili sababu zilizokwamisha kukalika kwa mradi katika muda uliopangwa. Lakini hivi sasa ujenzi unaendelea ambapo Roughton baada ya kuona masharti yaliyo katika makubaliano, imeamua kujitoa,” kilisema chanzo hicho.

Alipotakiwa kulizungumzia suala hilo, Chenge alisema kuwa ni haki ya Resident Engineer huyo kujitoa na kwamba serikali haina nia ya kumtafuta engineer mwingine kutoka katika eneo mbali na mradi.

“Kusema kuwa tunatafuta resident engineer kutoka Kenya ni upuuzi wa mchana… hatuna sababu ya kumtafuta mtu kutoka mbali, tutatafuta palepale, kama yeye ameamua kujitoa ni haki yake, hii ni biashara,” alisema na kuongeza:

“Wewe utaiona kazi itakavyoendelea, kazi yako si kujua (tumeafikiana nini)… inaelekea hautaki kupata taarifa za uhakika kuhusiana na mradi.”

Alipoelezwa kuwa kumpigia simu ili alizungumzie suala hilo ni moja ya jitihada za kutafuta taarifa za uhakika kutoka serikalini kuhusiana na mradi huo, Chenge alikuwa na jibu jingine:

“Sasa wewe si unasema ulienda kule kwenye eneo (la mradi) na umepata taarifa? Basi nipe hizo taarifa zako na mimi ndipo nitakupa za kwangu.”

Mmoja wa wahandisi wa Kampuni ya Konoike, inayojenga barabara hiyo, alithibitisha kuwapo kwa mazungumzo baina ya kampuni hiyo na serikali.

Hata hivyo, hakuwa tayati kutaja masharti mapya waliyopewa na serikali zaidi ya kubainisha kuwa wameongezewa muda wa miaka miwili kukamilisha kazi hiyo.

“Kweli tumekaa na wizara, ambayo pamoja na mambo mengine imetuongezea sh bilioni 10 pamoja na miaka miwili kwa ajili ya kukamilisha hizo kilometa zilizobaki,” alisema mhandisi huyo ambaye naye hakutaka jina lake litajwe.

Miezi kadhaa iliyopita, Naibu Waziri wa Miundombinu, Dk. Makongoro Mahanga, akizungumzia kukwama kwa baadhi ya miradi ya barabara nchini, alisema kuwa serikali haitosita kuzipiga faini kampuni ambazo zitashindwa kutekeleza miradi yao kulingana na mikataba waliyosaini.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.