UCHAGUZI unaoendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) umeanza kufichua udhaifu uliopo miongoni mwa wanachama na viongozi wa chama hicho katika kufuata misingi ya demokrasia waliyojiwekea.
Hadi hivi sasa, chama hicho kimeshafanya uchaguzi katika ngazi ya matawi katika maeneo kadhaa, lakini imeibuka mivutano mizito katika maandalizi ya chaguzi katika ngazi za juu, kuanzia ngazi ya wilaya.
Kwa kiasi kikubwa, mivutano hiyo inatokana na sababu za kweli na nyingine za kupikwa, zenye lengo la kutaka kuwachafua baadhi ya wanachama na wagombea, ili kurahisisha uchaguzi wa baadhi ya watu.
Kwa upande mwingine, maandalizi hayo yameanza kuonyesha mgawanyiko uliopo baina ya makundi yanayowaunga mkono baadhi ya wagombea.
Ingawa chama hicho kimesema hivi karibuni kuwa makundi ndani yake, hasa nyakati za uchaguzi, ni kitu kisichoepukika, lakini uzoefu unaonyesha kuwa inakuwa vigumu kuyavunja makundi hayo baada ya chaguzi.
Hayo yanadhihirishwa na mambo yanayojitokeza katika sehemu mbalimbali nchini, katika maendeleo ya chaguzi hizo ndani ya CCM.
Kutoka Tanga, Kiadi Mohamedi, anaripoti kuwa baadhi ya wanachama wa CCM katika Wilaya ya Tanga, wameelezea hofu yao waziwazi, wakionya kuwapo uwezekano wa chama hicho kukumbwa na mitafaruku kwa kile walichokieleza kuwa vigogo wanaowania madaraka ndani ya chama hicho kupandikiza watu katika uchaguzi huo kwa lengo la kupanga safu ya uongozi.
Baada ya kuona kuwa kilio chao kimekosa msikilizaji katika ngazi hiyo, sasa wanachama hao wanapanga kuonana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba, kumueleza njama hizo zinazofanywa na baadhi ya vigogo wa chama hicho, wanaojiandalia ushindi kwenye uchaguzi ujao wa wilaya na mkoa.
Wanachama hao walieleza hofu yao hiyo kwa nyakati tofauti na kuongeza kuwa kuna makundi ya watu wanaowarubuni wanachama wa chama hicho, ili wawachague wagombea wanaowataka wao, hata kama hawakubaliki.
Walisema kuwa kundi hilo la watu ambalo hushirikiana na baadhi ya makatibu wa kata na madiwani, limekuwa likipita nyakati za usiku kwa wapiga kura, katika kipindi hiki cha uchaguzi na kuwashawishi kwa vitu mbalimbali, zikiwamo fedha na kuwataka wawachague watu wanaowataka wao.
Walisema hali hiyo inawatia hofu kutokana na ukweli kwamba inaweza kukifikisha pabaya chama hicho, kwani inaweza kusababisha chama kikapata viongozi dhaifu waliochaguliwa kwa uwezo wao kifedha.
Wakizungumza na gazeti hili, wanachama hao walisema wana uchungu sana na chama chao na hawatakubali kuona kikihujumiwa na kundi la watu wachache wenye fedha, akiwamo kigogo wa wilaya anayefadhili kundi hilo linalojihusisha na kupanga safu ya uongozi ndani ya CCM.
Walieleza kuwa athari za mkakati unaofanywa na kundi hilo tayari zimeshajitokeza kwa baadhi ya kata kukataa matokeo ya chaguzi zao, baada ya kubaini kuwa baadhi ya watu walioshinda walikuwa wamepandikizwa.
Wakizungumzia njia inayotumika kupanga safu za uongozi, wanachama hao walisema ni pamoja na baadhi ya halmashauri za matawi kutotangaza uchaguzi huo kwa wanachama, ili kuwapa nafasi ya kujiandaa, viongozi kupitisha fomu kwa watu wanaowataka, jambo walilodai kuwa ni ukiukwaji wa taratibu za chaguzi za chama.
Hali kama hiyo imeyakumba matawi kadhaa mkoani Dar es Salaam, ambako baadhi ya chaguzi zilisimamishwa, baada ya kuibuka madai makali ya rushwa, upendeleo na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.
Baadhi ya wanachama wa CCM tawi la Sinza C, waliliambia gazeti hili kuwa, kuna kiongozi mmoja wa eneo hilo, amekuwa akiwashawishi watu wawachague viongozi aliowapanga katika safu yake, kwa madai ya kuunda timu itakayohakikisha ushindi mwaka 2010. Uchaguzi katika kata hiyo ulivunjika.
Katika Kata jirani ya Sinza D, wanachama katika Tawi la Sinza D waliweza kufanya uchaguzi wa kumchagua mwenyekiti lakini hawakufanikiwa kufanya uchaguzi wa nafasi ya katibu mwenezi na siasa, na nafasi ya katibu wa fedha na uchumi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kukosewa kwa taratibu za uchaguzi.
Ilidaiwa kuwa majina ya baadhi ya wagombea yalirudishwa na kupangiwa nafasi ambazo hawakuomba kugombea.
Katika uchaguzi huo uliofanyika hivi karibuni, waligundulika wanachama hewa waliokubali kupiga kura kwa kupewa sh 500 kila mmoja ili wamchague mmoja wa viongozi.
Ikiwa hiyo haitoshi, ilipofika saa nane, kura za wagombea wote zilichanganywa kwa madai kwamba zilichanganywa kwa bahati mbaya, kitu ambacho kilizua vurugu kubwa na kutulizwa baadaye na makada wenyewe.
Katibu wa CCM mkoani Dar es Salaam, Kapteni John Barongo, alilazimika kusimamisha uchaguzi katika Tawi la Midizini, Manzese, kutokana na baadhi ya wagombea kuwekewa majina yao katika nafasi ambazo hawakuziomba.
Kutoka Morogoro, Joseph Malembeka, anaripoti kuwa hofu imeanza kuwakumba baadhi ya wanachama wa CCM, wakihofia chama chao kusambaratika kutokana na kuibuka kwa makundi kama ilivyokuwa kwa Uchaguzi Mkuu wa 2005.
Akitoa taarifa kwenye mkutano wa halmashauri ya siasa ya chama hicho mkoa, Katibu wa CCM mkoani hapa, Mary Chatanda, alisema kutokana na hofu hiyo huenda hata uchaguzi wa viongozi ndani ya chama hicho unaoendelea hivi sasa ukaharibika.
Alisema mbali na chama hicho kuwataka wanachama wake kuvunja makundi na kuungana kulijenga taifa, baadhi ya maeneo makundi yameendelea kuwepo, hali inayohatarisha uimara wa chama hicho.
Alizitaja wilaya ambazo zimeshamiri kuendeleza makundi hayo ya mtandao kuwa ni Morogoro Mjini na Mvomero, ambapo wanachama wamegawanyika tofauti na inavyotakiwa katika kuharakisha maendeleo kwa wananchi.
Naye Murugwa Thomas anaripoti kutoka Tabora kuwa CCM Wilaya ya Sikonge imekumbwa na mgawanyiko kiasi kwamba wanachama wake wamegawika kuelekea chaguzi za ndani ya chama.
Habari ambazo zimelifikia gazeti hili kutoka wilayani Sikonge zinadai kuwa mgawanyiko huo umetokana na kutoelewana kati ya Mbunge wa jimbo hilo, Said Nkumba na mweka hazina wa chama hicho, Alaija Mwiga.
Uhasama baina ya makundi wilayani humo ulichukua sura mpya wiki iliyopita baada ya Nkumba kutumiwa jeneza na sanda yake, kupitia ofisi za CCM Wilaya ya Sikonge.
Inadaiwa kuwa jeneza hilo lilitumwa na mweka hazina wa chama hicho wilayani humo na lilipokewa katika ofisi hizo Mei 18, mwaka huu.
Habari zinaeleza kuwa mweka hazina huyo alichonga jeneza, kununua mafuta, sabuni na sanda yake na kutaka akabidhiwe Mbunge Nkumba, kwa kile kilichodaiwa kuwa ni familia ya mweka hazina huyo kudhalilishwa na kunyanyaswa na kauli za mbunge.
Baadhi ya wanachama walisema kuwa mgogoro huo unatokana na makundi yaliyosababishwa na uchaguzi unaoendelea ndani ya chama.
Visa hivyo vinadaiwa kuanza zamani kidogo. Februari 2005, mweka hazina huyo alifiwa na mkewe na baada ya msiba huo kutokea, mbunge alitoa vifaa vyote kwa ajili ya maziko.
Walisema kuwa vifaa vilivyotolewa na mbunge huyo ilikuwa ni jeneza, sanda, mafuta na sabuni, ili kufanikisha mazishi hayo.
Inadaiwa kuwa viongozi hao wawili wamekorofishana baada ya kujikuta katika makundi mawili tofauti katika kampeni za uchaguzi wa ndani ya chama, huku Nkumba akidaiwa kumuunga mkono mwenyekiti wa sasa wa chama wa wilaya.
Habari zaidi zinadai kuwa mweka hazina huyo aliamua kuchonga jeneza hilo baada ya kupata tuhuma nzito kwamba amekuwa akikutana na watu mbalimbali usiku na kumsema mbunge huyo, huku akisahau kuwa alitoa msaada mkubwa katika mazishi ya mkewe.
Alipovifikisha vitu hivyo katika ofisi za CCM, alivikabidhi kwa Katibu wa CCM wa Wilaya, Ndaluone Mbogo, ili avikabidhi kwa Nkumba, lakini ikashindikana kwani uongozi wa CCM ulikataa kuhusika na mgogoro huo.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka Sikonge, mweka hazina huyo alisema kwamba baada ya kufikisha jeneza hilo, siku iliyofuata alikamatwa na polisi, kwa madai ya uvunjifu wa amani.
Mwiga aliendelea kudai kuwa baada ya kukamatwa na polisi alipelekwa kituoni ambako alitoa maelezo na sababu iliyosababisha kufanya hivyo, na baadaye alidhaminiwa. Ametakiwa kuripoti kituoni hapo Mei 24 mwaka huu.
Alipohojiwa kuhusiana na hilo, Mbogo alisema suala hilo halikihusu chama, bali ni ugomvi wa watu wawili.