KUTOELEWEKA vyema kwa utaratibu wa matumizi ya barabara za Ali Hassan Mwinyi na Morogoro, nyakati za asubuhi kwa magari yanayokuja katikati ya jiji, jana kulisababisha usumbufu uliowafanya baadhi ya wakazi wa jiji kuona utaratibu huo kuwa ni kero badala ya suluhisho la msongamano wa magari.
Utaratibu huo uliotangazwa juzi na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, James Kombe, unataka sehemu za barabara hizo, zitumike kama njia tatu, ili kuwezesha magari mengi yanayoelekea jijini nyakati za asubuhi kuwahi kufika na kupunguza msongamano wa magari hayo.
Chini ya mpango huo, sehemu ya kipande cha barabara ya Ali Hassan Mwinyi kuanzia Morocco hadi maeneo ya katikati ya jiji, ambacho hupitisha magari yanayotoka katikati ya jiji kuelekea Mwenge, kitaruhusiwa kupitisha magari yanayoelekea jijini kuanzia saa 12 hadi saa 3:00 asubuhi.
Hali kadhalika, zoezi kama hilo linatakiwa kufanywa katika sehemu ya kipande cha Barabara ya Morogoro.
Hata hivyo, hali hiyo iligeuka kuwa kero katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi kati ya Namanga na njia panda inayoelekea katika Kanisa la Mtakatifu Petro, kwani magari yaliyokuwa yameruhusiwa kutumia barabara hiyo yalisababisha foleni mpya ya magari yanayotokea mjini.
Kutokana na hali hiyo, polisi wa kawaida na wale wa usalama barabarani waliokuwa wanasimamia zoezi hilo, walilazimika kuyarejesha magari hayo katika njia zake za kawaida katika njia panda hiyo na hivyo kujikuta wakizidisha msongamano zaidi, kwani magari mengine yanayokwenda mjini kwa kutumia njia ya kawaida, yalilazimika kusimama.
Wakitoa maoni yao baada ya kukabiliana na adha hiyo, baadhi ya wakazi wa jiji waliliambia gazeti hili kuwa mpango huo haukupaswa kuanzishwa haraka namna hivyo.
Akizungumza jana katika ofisi za Tanzania Daima, mmoja wa wananchi hao alisema mtazamo wa kutumia njia tatu kwa Barabara ya Morogoro na Ali Hassan Mwinyi kwa lengo kupunguza msongamano huo hakutasaidia kuondoa tatizo hilo.
Alisema katika utekelezaji wa agizo hilo, jana barabara hizo zilikuwa na msongamano maradufu tofauti na siku nyingine.
Mwishoni mwa wiki, uongozi wa Mkoa wa Dar es Saalam, baadhi ya mawaziri, makamanda wa polisi na wadau wa masuala ya usafiri walikubaliana kuanzia sasa barabara hizo zigawanywe, ili kupunguza foleni nyakati za asubuhi na jioni.
Kikao hicho, kiliitishwa na Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
Mkazi huyo, alisema barabara hizo zimejengwa mahususi kwa mfumo wa njia ya barabara mbili, hivyo kulazimisha ziwe njia tatu, bila kuufanyia marekebisho muhimu, ni kuzalisha tatizo jipya badala ya kutatua lililopo.
“Leo (jana) kulikuwa na foleni kubwa sana hasa katika makutano ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi kuelekea Oysterbay.
“Serikali inapaswa kuboresha usafiri wa umma na kuwa wa uhakika. Mfano, watu wanaotoka maeneo ya Tegeta na Mbezi kuacha magari yao Mwenge, ili waweze kutumia usafiri huo, kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza idadi ya magari yanayokwenda mjini,” alisema mkazi huyo ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini.
Pia ameishauri serikali kuharakisha utekelezaji wa mradi wa mabasi yaendayo kasi katika kukabiliana na tatizo hili.
Mkazi mwingine, alisema katika kukabiliana na tatizo hili, huduma mbalimbali za kijamii pamoja na ofisi mbalimbali zingetawanywa katika maeneo mbalimbali ya mji.
Alisema msongamano huo unatokana na kwamba nyakati za asubuhi watu wengi wanalazimika kwenda mjini ambako ndiko zinapatikana huduma nyingi muhimu, zikiwamo za maofisi mengi ya serikali na za watu binafsi.
“Msongamano wa magari mjini unatokana na kuwapo kwa maofisi mengi na huduma nyingi muhimu kupatikana huko. Maofisi haya na huduma hizo zikitawanywa, msongamano utakwisha, kwa kuwa si watu wote watakuwa wakilazimika kwenda mjini,” alisema.
Mwingine, aliyejitambulisha kwa jina la Daniel Mfuru, mkazi wa Sinza, Dar es Salaam, alisema suala la kuongeza taa za barabarani si suluhisho la msongamano wa magari.
Alisema kinachopaswa kufanywa ni kuboresha taa zilizopo, kabla ya kufikiria kuongeza taa nyingine za barabarani.
“Taa nyingi za barabarani zilizopo hazifanyi kazi. Kinachotakiwa kufanyika ni kuboresha taa zilizopo. Pia sielewi suala la taa za barabarani kuwa zinafanya kazi na wakati huohuo kuna askari wa kuongoza magari.
“Kutokana na hali hii, inaonekana kuwa taa hizi hazina maana na tunafuja fedha za serikali, kwani taa zinawaka bila ya kuwa na matumizi,” alisema.
Alitoa mfano wa taa za barabarani katika makutano ya Uhuru/Bibi Titi, Nkrumah/Bibi Titi/ Lumumba, Mandela/ Uhuru zimeharibika muda mrefu bila kufanyiwa matengenezo.
Mfuru alishauri mamlaka zinazohusika zinapaswa kukaa chini na kuvumbua taa ambazo zinaweza kuhisi upande fulani kuna foleni kubwa na kuruhusu magari ya upande huo kwa muda mrefu, tofauti na eneo ambalo kuna magari machache.