Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
‘Teknohama kikwazo cha maendeleo’
http://www.habaritanzania.com/articles/3660/1/‘Teknohama-kikwazo-cha-maendeleo’
By Habari Tanzania
Published on 05/21/2007
 
IMEELEZWA kwamba kiwango duni cha elimu kuhusu teknolojia ya mawasiliano ya kisasa (TEKNOHAMA), ni moja ya sababu kubwa zinazofanya vita dhidi ya umaskini na ujinga isifanikwe nchini.

na Sitta Tumma, Mwanza


IMEELEZWA kwamba kiwango duni cha elimu kuhusu teknolojia ya mawasiliano ya kisasa (TEKNOHAMA), ni moja ya sababu kubwa zinazofanya vita dhidi ya umaskini na ujinga isifanikwe nchini.

Serikali kupitia Wizara ya Miundombinu, imetakiwa kushirikiana vyema na wadau kutoka sekta mbali mbali za mawasiliano, ili kuboresha na kusambaza huduma hiyo hadi vijijini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Mawasiliano Kanda ya Ziwa (SWOPnet), Abubakar Karsan, aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye mdahalo wa mawasiliano uliofanyika jijini hapa.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa kutoboreshwa kwa mawasiliano ya teknolojia ya kisasa, hususan katika sekta za elimu, afya na kilimo, ndiyo sababu kuu inayochangia kudidimiza maendeleo na uchumi nchini.

“Umefika wakati serikali ione umuhimu wa kupeleka kompyuta mashuleni, hospitalini, vituo vya afya na ipeleke mawasiliano hayo vijijini kwa wakulima ili na wao waweze kufanya kazi zao kwa upeo na utandawazi zaidi,” alishauri.

Akifafanua, Karsan ambaye pia ni Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Waandishi mkoani Mwanza (MPC), aliitaka serikali kuona umuhimu wa kubuni mbinu mpya za kukabiliana na lindi la umaskini lililowagubika Watanzania.

Alisema njia pekee ya kuondokana na adha hiyo ni kuwekeza katika teknolojia ya mawasiliano na kwamba ni vyema wananchi wakawezeshwa kwa kuboreshewa mawasiliano hayo.