CHAMA Cha Mapinduzi (CCM, leo kinafaya mabadiliko ya uongozi wake wa juu kwa Mwenyekiti wa sasa Benjamin Mkapa, kung'atuka, na nafasi yake kushikwa na Rais Jakaya Kikwete.
Umekuwa ni utamaduni, kwa anayekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, kuwa pia Mwenyekiti wa CCM. Kikwete anakuwa Mwenyekiti wa nne wa CCM, baada ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Mkapa.
Wajumbe zaidi ya 1,800 leo watakuwa wanakumbuka kazi waliyoifanya Mei 4, 2005 ambako katika ukumbi huu huu wa Chimwaga, walimpitisha kwa kura nyingi, Kikwete, kuwania urais kupitia chama hicho.
Kikwete hana mpinzani, hivyo haitarajiwi kuwa atakosa kura za kumwezesha kushika wadhifa huo.
Mkutano Mkuu Maalumu ulifunguliwa jana, na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka mikoa yote 26 ya Tanzania .
Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula, alitoa taarifa ya kazi za chama, akielezea mafanikio makubwa ya chama hicho, hasa kwenye ushindani unaoshirikisha vyama vingi vya siasa.
Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliwasilisha taarifa ya serikali ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005-2010.
Lowassa, alieleza mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipini kifupi tangu serikali ya awamu ya nne ilipoingia madarakani, Desemba, 2005.
Aliwahakikishia wana CCM na wananchi wote kuwa ahadi zilizotolewa na mgombea urais kupitia CCM wakati wa kampeni za mwaka 2005, zimeanza kutekelezwa.
Alisema utekelezaji wa ahadi hizo unakwenda sambamba na utekelezaji wa yaliyomo kwenye ilani ya uchaguzi ya chama hicho.
“Leo tunajivuna kwa kupewa ridhaa na kazi kubwa ya kushika dola, wananchi wametuamini kuwa CCM ndicho chama chenye uwezo wa kutoa uongozi utakaowezesha kutatua kero.
“Taarifa hii ninayoiwasilisha leo inatupa fursa ya kuelewa tulipo na kazi kubwa iliyo mbele yetu. Tunaungwa mkono na wananchi wengi, wananchi wana matumaini makubwa, ni wajibu wa chama chetu kuhakikisha kuwa imani na matumaini hayo yanajibiwa,” alisema