Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Wizi wa magari waibuka Z’bar
http://www.habaritanzania.com/articles/3659/1/Wizi-wa-magari-waibuka-Z’bar
By Habari Tanzania
Published on 05/21/2007
 

LIMEIBUKA wimbi la wizi wa magari visiwani humu, hasa katika kumbi za starehe na kuibua hofu miongoni mwa watu wanaomiliki vyombo hivyo vya usafiri.


na Mwandishi Wetu


LIMEIBUKA wimbi la wizi wa magari visiwani humu, hasa katika kumbi za starehe na kuibua hofu miongoni mwa watu wanaomiliki vyombo hivyo vya usafiri.

Tukio la kwanza la wizi wa gari lilitokea katika ukumbi wa burudani wa Gymkhana, ambapo gari aina ya ESCUCO liliibiwa usiku.

Tukio la pili lilitokea juzi baada ya mfanyakazi mstaafu wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Abdul Mshangama, kuibiwa gari aina ya Starlet, lenye namba za usajili ZNZ 16151.

Akizungumza mjini Zanzibar, Mshangama alisema gari lake liliibwa majira ya saa 4:00 usiku alipokuwa ameliegesha katika ukumbi wa burudani katika eneo la Maisara, jirani na Makao Makuu ya Jeshi la Magereza.

Alisema kwamba alikwenda katika eneo hilo kwa ajili ya mazungumzo na rafiki yake, lakini baada ya kumaliza mazungumzo na kutoka nje hakulikuta gari lake mahali alipokuwa amelipaki.

“Nimeripoti tukio hili katika kituo cha Polisi Mwembe Madema, lakini hadi jana gari langu lilikuwa halijapatikana,” alisema.

Alisema gari hilo lina thamani ya sh milioni 3.5 na tukio hilo limempa mshituko mkubwa kwa vile limekuja siku chache tangu yeye na wafanyakazi wengine wa PBZ kustaafishwa kwa lazima katika mpango wa serikali kubinafsisha benki hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Bakar Khatib Shaaban, alithibitisha kujitokeza vitendo vya wizi wa magari na kueleza kwamba hatua za kukabiliana na matukio hayo zimeanza kuchukuliwa.

Hata hivyo, alisema kwamba gari aina ya ESCUDO lililoibwa awali, lilipatikana likiwa limetelekezwa katika maeneo ya Kisauni, nje ya mji wa Zanzibar.

Alisema kwamba kufuatia tukio hilo, mtu mmoja anaendelea kushikiliwa na Polisi huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

“Matukio hayo yametokea na Polisi inaendela kufanya uchunguzi, ingawa tuna wasi wasi huenda ikawa ni vitendo vya kihuni,” alisema kamanda huyo.

Matukio ya wizi wa magari ni mapya katika mji wa Zanzibar. Kutokana na kutokuwapo kwa vitendo hivyo, watu wengi wamejenga mazoea ya kulaza magari yao na pikipiki nje ya nyumba zao hasa katika nyumba za maendeleo Kilimani na Michezani.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni kumekuwapo vitendo vya wizi wa magari na mashine za kupandishia vioo aina ya ‘Power Window’, pamoja na vioo vyake.