WAKATI viongozi wakikuna vichwa kupunguza ajali za barabarani, Jeshi la Polisi nchini limetangaza mipango yake inayolenga kudhibiti hali hiyo.
Moja kati ya mipango ya jeshi hilo, ni kuhakikisha kuwa kuanzia sasa, utoaji wa leseni za udereva unadhibitiwa ili kuhakikisha kuwa wasiostahili hawapati nafasi ya kuendesha magari, hasa ya abiria.
Akizungumza katika kipindi cha Kipima Joto, kilichorushwa na kituo cha Televisheni cha ITV cha jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, James Kombe, alisema hatua ambazo Jeshi la Polisi inapanga kuzichukua, zinakusudia kupunguza utitiri wa leseni hizo mitaani.
Alisema chini ya mabadiliko hayo, leseni ya daraja C, ambayo inamruhusu mwenye nayo kuendesha gari la aina yoyote hivi sasa, itafutwa kabisa.
“Tumekubaliana kufanya mabadiliko makubwa ya leseni zote ikiwemo Class C, kwani imeonekana kutolewa bila utaratibu… hii leseni ni ajira tosha kwa dereva anayeipata,” alisema Kamanda Kombe.
Alisema leseni hiyo itagawanishwa katika sehemu tatu ambapo itakuwa daraja C1, C2 na C3, ambapo kila moja itakuwa na kazi yake maalumu katika shughuli za uendeshaji wa magari barabarani.
Alisema leseni daraja C1 itahusisha mabasi yanayobeba abiria kuanzia 45 hadi 30, wakati daraja C2 itahusika magari yenye uwezo wa kubeba abiria 30 hadi 15 na daraja C3 itahusika na magari yanayobeba abiria wachache.
Mabadiliko hayo yanatarajia kuanza wakati wowote kuanzia sasa, na kwamba wadau wanaohusika wanapaswa kuyazingatia ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
Aidha, jeshi hilo limewaonya madereva wote kuanzia wa mabasi makubwa yanayokwenda mikoani, na wale wanaondesha daladala, kuwa hawatapatiwa leseni bila kutimiza masharti yaliyowekwa.
Moja ya masharti hayo ni kila dereva kupata masomo ya udereva katika Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), kilichopo Ubungo, kwa ajili ya kupata masomo yanayohusu leseni hizo mpya.
“Hakuna dereva atakayepata leseni hizo bila kwenda Chuo cha Usafirishaji pale Ubungo kusoma kwa muda uliopangwa, na kwa hili tumejipanga kisawasawa kukabiliana nalo,” alisema Kamanda Kombe.
Alisema ili kupunguza wingi wa ajali, tayari jeshi hilo linaanza kufanya kazi ya kukaa katika vyuo vinavyoendesha mafunzo ya udereva kote nchini ili kubaini kama mafunzo yanayotolewa yanakidhi mahitaji yanayokubalika.
“Tutaanza kazi ya kukagua vyuo hivi, kwa maana vipo ambavyo vina magari ya kutolewa mafunzo yakiwa katika hali mbaya ya uchakavu, sasa mambo kama haya hatuwezi kuyavumilia,” alisema.
Alisema jeshi hilo mpaka sasa limefanikiwa kukamata magari zaidi ya 1,464 na yamepiga faini ya jumla ya sh milioni 42 kwa makosa mbalimbali.