WAUMINI wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), wameyafikisha madai dhidi ya Askofu wao Mkuu, Godfrey Mdimi Mhogolo, katika ngazi za juu za uongozi wa kanisa hilo, imefahamika.
Katika ‘mashitaka’ yao, waumini hao wanamtuhumu askofu wao huyo kwa kukumbatia vitendo visivyoendana na maadili ya kanisa hilo, ubadhirifu wa mali za kanisa pamoja na kuliongoza kanisa kibabe.
Mashitaka hayo ni dhahiri yanafuatia kauli iliyowahi kutolewa na Katibu Mkuu wa kanisa hilo nchini, hivi karibuni kuwa, uongozi wa juu hauwezi kuingilia mgogoro uliopo baina ya waumini wa DCT, hadi pale watakapofikisha suala hilo rasmi na kuomba msaada wa kusuluhishwa.
Kwa muda sasa, kumekuwa na mgawanyiko baina ya waunini wa kanisa hilo katika dayosisi hiyo, uliotengeneza makundi mawili. Moja ya kundi hilo linamuunga mkono na kumkubali Askofu Mkuu wa Dayosisi hiyo, Mhogolo wakati kundi jingine limejitokeza kumpinga na kumuunga mkono Askofu Msaidizi, Ainea Kusenha.
Mgawanyiko huo wa waumini wa Kanisa Anglikana, umetokana na kuwepo kwa tuhuma dhidi ya Askofu Mhogolo kuwa, anaunga mkono vitendo vya ushoga na usagaji, kuhimiza matumizi ya kondomu miongoni mwa waumini wa kanisa hilo na kuongoza kanisa kwa mabavu.
Taarifa iliyotolewa na Mchungaji Christopher Milimo wa Parishi ya Haneti, kwa niaba ya Umoja wa Maparishi, katika kikao kilichofanyika mwishoni mwa wiki, ilibainisha kuwa mpaka sasa jumla ya Parishi 132 hazitaki kuhudumiwa na Askofu Mhogolo.
Alisema parishi hizo 132 hazitaki huduma ya Mhogolo kutokana na yeye kuendelea na msimamo wake katika kutetea ushoga, hata baada ya kuelezwa kuwa jambo hilo si zuri na halikubaliki katika kanisa.
Taarifa hiyo ilitaja sababu nyingine ya kumkataa Mhogolo kuwa, ni kitendo chake cha kutumia umasikini wa watu kwa manufaa yake binafsi.
Ikifanunua suala hilo, taarifa hiyo ilisema kuwa, askofu huyo amekuwa akiomba misaada kutoka nje ya nchi kwa niaba ya waumini wa kanisa hilo, lakini inapopatikana anadaiwa kuitumia yeye mwenyewe binafsi bila kuitolea maelezo yoyote.
Aidha, taarifa hiyo inadai kuwa, mahubiri ambayo yanatolewa na askofu huyo, hayalingani na dini inavyotaka, kwani mara nyingi amekuwa akitetea matumizi ya kondomu badala ya kukataza uasherati.
Inadai taarifa hiyo kuwa, Muhogolo amekuwa na utawala wa kimabavu, dharau na kuwanyanyasa Wakristo na viongozi wenzake kwa kuwafukuza kazi bila sababu za msingi na kinyume cha Katiba ya DCT. Mfano unaotolewa katika hilo ni kufukuzwa kazi kwa askofu aliyekuwa msaidizi wake, Kusenha.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, kutokana na tuhuma hizo na nyingine ambazo wameziwasilisha kwa Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana, Donard Mtetemela, wameamua kumkataa rasmi Muhogolo katika kutoa huduma ya kiroho kwenye parishi hizo 132.
Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT) ina jumla ya parishi 200 na 68 zilizosalia, hazijatoa tamko lolote na zinaendelea kupokea huduma ya Mhogolo.
Askofu Kusenha alipokea barua ya kusimamishwa kazi kutoka kwa Askofu Muhogolo, Februari mosi, mwaka huu ikimtaka aache kuendesha misa na kusimamia kazi za kanisa, arudishe gari la kanisa na ahame katika nyumba ya kanisa kwa tuhuma za upotevu wa fedha za kanisa.
Baada ya kupokea barua hiyo, Kusenha aliijibu na kudai kuwa kwa mujibu wa sheria za Kanisa Anglikana, na kwa mujibu wa Katiba ya DCT, Mhogolo hakuwa na mamlaka ya kumfukuza kazi.
Tangu alipopewa barua hiyo, askofu huyo hajawahi kuendesha misa kanisani hapo wala kupokea mshahara wa uaskofu ambapo alinyang’anywa gari alilokuwa akilitumia, lakini aligoma kuhama katika nyumba ya kanisa ambako anaishi mpaka sasa.
Kwa mara ya kwanza tangu kusimamishwa kwake, Kusenha jana aliongoza misa katika Kanisa Kuu Anglikana mjini Dodoma. Misa hiyo ilihudhuriwa na idadi kubwa ya waumini ambao wanamuunga mkono.
Akihubiri katika misa hiyo alisema, Kanisa Anglikana Tanzania haliwezi kukubali vitendo vya ushoga na usagaji, kwa kuwa licha ya kuzua mzozo mkubwa duniani, ni dhambi inayolidhalilisha kanisa kwa ujumla.
Alisema wale wanaotetea ushoga kwa sababu ya kupata fedha, wanasahau au kukataa neno la Mungu lisemalo “Itamsaidia nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akaipoteza nafsi yake?”
Alisema mashoga ni jamii ya watu wachache walioko Ulaya wanaolazimisha watambuliwe, hivyo kanisa la Afrika na Ulaya lazima likemee uovu huo kwa nguvu zote kwani watu hao ni wagonjwa waliovurugikiwa akili.
Akizungumza na waandishi wa habari kanisani hapo baada ya misa, Kusenha alisema ameamua yeye binafsi kurudi kwa nguvu mpya katika huduma, baada ya kuona anakubalika na Wakristo walio wengi na kuona kuwa kusimamishwa kwake hakukufuata katiba.
Alisema amekuwa na migogoro ya kiuongozi na Muhogolo kwa muda mrefu, hata baadhi ya waumini na viongozi wa kanisa wanatambua migogoro hiyo, ambayo pia ilishafikishwa katika Halmashauri ya DCT na kutolewa maamuzi.
Alisema tangu asimamishwe kazi, hajawahi kupata mshahara wowote kutoka kanisani hapo, wala posho yoyote ambapo kwa muda wote huo, amekuwa akitunzwa na mama yake mzazi anayeishi kijijini.
“Sing’ang’anii kufanya kazi, lakini ninachotaka ni kutetea kanisa na kusimamia misingi ya dini na Katiba ya DCT, hivyo sitafurahi kuona DCT ikigawanyika kwa ajili ya kasoro za watendaji,” alisema askofu huyo kwa masikitiko.
Alisema kwa sasa ataendelea kutoa huduma kwa waumini wote wanaomkubali na kuendesha zoezi la kuweka mikono katika parishi zilizomkataa Mhogolo.
Alibainisha kuwa, atakubaliana na maamuzi ya kumsimamisha iwapo taratibu za kikatiba zitafuatwa katika kumuachisha kazi kupitia kikao cha SINODI kitakachofanyika mwezi Julai mwaka huu.
Alisema kuwa, hayupo tayari kuhamishiwa eneo jingine na angependa aendelee kubakia Dodoma.
“Nimefanya kazi ya Mungu na kulitumikia kanisa kwa miaka 33, mpaka sasa ambapo imebaki miaka kama mitano nistaafu, ndiyo nakutana na majaribu haya… nimedhalilishwa sana, lakini namuachia Mungu,” alisema Kusenha.
Alibainisha kuwa, hakuna taarifa yoyote inayoonyesha fedha za misaada kutoka kwa wahisani zinazoingia kanisani, lakini kila siku Mhogolo amekuwa akipokea fedha za misaada kutoka nje ya nchi.
Awali, akitoa maelezo kuhusu mzozo huo, Mchungaji mstaafu, Kanoni Elia Nhukuwala, alisema hawapo tayari kuona kanisa likiyumba na kugawanyika kutokana na ugomvi wa watu binafsi.
Alisema wao wanachojua ni kumuabudu Mungu na kufuata misingi ya dini, ambapo pia wanaukataa ushoga katika kanisa kwani ni dhambi.
Nhukuwala alisema, kama Halmashauri ya DCT imeshindwa kuwasemea waumini kuhusu kuukataa ushoga, wameamua kusimama wenyewe na kuonyesha msimamo wao kama waumini walio hai.
Alimtaka Askofu Muhogolo kujiuzulu kwa madai kuwa amepoteza sifa ya kuwa askofu ili kulinusuru kanisa na mgawanyiko huo.