SIKU moja baada ya Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) na kile cha Kilimo cha Sokoine huko Morogoro (SUA) kutangaza kuwarejesha wanafunzi waliokuwa wamesimamishwa masomo, baadhi ya vyama vya upinzani vimetoa tamko la pamoja kueleza kuwa hatua hiyo haitasitisha azma yao ya kuishitaki serikali kuhusu suala hilo la wanafunzi.
Vyama hivyo, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na TLP, vilisema jana katika tamko la pamoja kuwa, baada ya wanafunzi wote kurejeshwa vyuoni, sasa mashitaka yao yatalenga kuipinga sera inayowataka wanafunzi kuchangia asilimia 40 ya gharama za masomo.
Akisoma tamko hilo jana mbele ya waandishi wa habari, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema watafungua kesi ya kuitaka mahakama itamke kuwa sera ya kuwataka wanafunzi kulipia asilimia 40 ya gharama za masomo ni batili.
Aidha, wapinzani hao walisema kuwa mashitaka yao yatalenga pia katika kupinga vigezo vilivyowekwa na serikali kuhusu wanafunzi wanaostahili kupata mikopo hiyo ya serikali.
Kwa mujibu wa taratibu zilizopo, kwa upande wa wavulana, wanaostahili kupata mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa elimu ya juu, ni wale waliopata daraja la kwanza wakati wasichana wanaostahili kupata ni wale waliopata daraja la kwanza na la pili katika matokeo ya mitihani yao ya kidato cha sita.
“Utaratibu huu pia tunapenda ufahamike kuwa ni wa kibaguzi na ni kinyume cha sheria iliyoanzishwa na bodi ya mikopo ya mwaka 2004, ambayo inaipa bodi uwezo wa kuweka vigezo itakavyovitumia kuwatambua Watanzania wanaostahili kupewa mikopo.”
Akizungumzia mchakato wa kulifikisha suala hilo mahakamani, Profesa Lipumba alisema tayari wameshalifikisha suala hilo kwa wanasheria ambao wanalifanyia uchambuzi kwa lengo la kuandaa mashitaka hayo.
Aidha, Lipumba alisema bado wanachunguza uwezekano wa kufikisha utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mahakamani kwa vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu cha kuwapa wanafunzi saa tatu wawe wameshaondoka katika maeneo ya chuo.
Muda huo ulitolewa kwa wanafunzi siku uongozi wa UDSM ulipotangaza kuwasimamisha masomo wanafunzi hao waliokuwa wamegoma kupinga kulipa asilimia 40 ya gharama za masomo.
“Wanafunzi walijikuta wametupwa barabarani bila hifadhi au usalama wowote wa mali zao na maisha yao, sheria za kidikteta zinaweza kuruhusu uvunjwaji wa haki hizi, lakini tayari Tanzania imeondoka katika utawala wa aina hiyo,“Kwa mujibu wa katiba ya nchi, kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake, hii ni ibara ya 14, pia katiba yetu inalinda haki ya kila mtu kuwa huru na kuishi kama mtu huru kupitia ibara ya 15.
“Ieleweke pia kuwa kwa mujibu wa katiba yetu, kila mtu anayo haki ya kuheshimiwa na kupata hifadhi ya nafsi yake, maisha yake binafsi na pia heshima na hifadhi ya maskani yake kama ilivyoainishwa katika ibara ya 16. Hivyo ni lazima kanuni za uendeshaji wa vyuo vikuu zifungamane na masharti haya ya katiba ya nchi,” alisema.
Wakizungumzia kuhusu hatua ambazo watawala wa chuo kikuu umekuwa ukizichukua dhidi ya viongozi 56 wa wanafunzi, wanasiasa hao wametoa wito kwa uongozi wa chuo kikuu kutowabughudhi na kuwaathiri kisaikolojia viongozi hao kiasi cha kuwafanya wasifaulu vyema mitihani yao.
Walisema kuwataka wajieleze na kuendelea kuwachunguza ni kuwanyima haki ya kufanya kazi zao kama viongozi halali wa Daruso, chombo ambacho kiliundwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Hata hivyo, wanasiasa hao wameitaka Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, iendeshe mjadala wa kitaifa kuhusu sera ya elimu ya juu mapema kabla ya bunge la bajeti, ili wananchi na wadau wengine waweze kushiriki na kutoa mawazo yao.
Walisema kwa kiasi kikubwa, sera hiyo ya uchangiaji gharama ina walakini mkubwa na ndio chanzo cha migomo mingi vyuo vya elimu ya juu hapa nchini.
Pia wameitaka wizara kuachana na dhamira yake ya kutaka kuifanyia mabadiliko sheria namba 9 ya mwaka 2004 kwa lengo la kuweka madaraja ya viwango vya kufaulu kuwa kigezo rasmi kwa wanafunzi kupatiwa mkopo wa elimu ya juu.