Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Tossi amgusa IGP
Tossi amgusa IGP
By Habari Tanzania | Published  05/19/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Happiness Katabazi


YULE kamanda maarufu wa polisi katika kusimamia na kuongoza operesheni za uhalifu ulioshindikana, Venance Tossi, amerejeshwa makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam kuongoza kitengo kipya kilichopewa jukumu la kuendesha operesheni maalum, zikiwamo zile za kukabiliana na uhalifu nchini.

Tossi ambaye hadi hivi karibuni alikuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, alikopelekwa mahususi kupambana na majambazi hatari wanaojumuisha askari wa kutoka nchi jirani, anakwenda makao makuu kutokana na mabadiliko ya makamanda wa jeshi hilo yaliyofanywa na mkuu wake, IGP Said Mwema.

Mwema anamhamisha kamanda huyo maarufu kwa jina la ‘Mti Mkavu’, kwa mara ya pili katika kipindi kifupi, baada ya kwanza kumfanya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro kabla ya kumhamisha na kumpeleka Kagera.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msemaji wa Jeshi hilo, (ACP) Esaka Mugasa, alisema kitengo hicho kipya ndani ya Jeshi la Polisi, kilianzishwa Mei 15, ikiwa ni sehemu ya kuboresha ufanisi wa utendaji wa Jeshi la Polisi nchini katika kukabiliana na uhalifu.

Mugasa alisema kitengo hicho kipya kimepewa madaraka ya kutokomeza uhalifu nchi nzima, kwa kusaidiana na makamanda wa polisi wa mikoa.

“Kitengo hiki kipya cha Operesheni Maalum, kimeanzishwa baada ya jeshi hili kubaini kwamba, ipo haja ya kuwa na kitengo hicho, hasa ukizingatia kuwa wahalifu kila kukicha wamekuwa wakibuni mbinu mpya,” alisema.

Mugasa alisema, Tossi ambaye ana cheo cha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), ameonekana kama mtu anayefaa kuongoza kikosi hicho maalum cha operesheni, baada ya kazi yake ya kukabiliana na majambazi kuvuta hisia za watu wengi, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, ambaye hivi karibuni alimmwagia sifa za kipekee.

Sifa za hivi karibuni, alizipata baada ya kuhamishiwa mkoani Kagera, ambako alifanikiwa kusambaratisha vikosi vya majambazi waliokuwa wakijificha katika misitu mkoani humo, na kutumia silaha za kivita kushambulia wananchi na kuwapora mali zao.

Aidha, akijibu swali la mwandishi kwa nini Tossi amekuwa akibadilishwa vituo vya kazi mara kwa mara, tena kwa muda mfupi, Mugassa alisema katika utendaji wake, Tossi amefanikiwa kuonyesha jinsi anavyojiamini, na utendaji kazi wake kuwa mzuri.

“Tossi ni mtendaji mzuri na hili halina ubishi, na kutokana na ubunifu na ujuzi alionao, IGP ameona amlete hapa Makao Makuu asaidiane na maofisa wenzake katika kushughulika na mambo mbalimbali, yakiwemo majanga ya moto na utekaji nyara pamoja na kusimamia vikosi mbalimbali nchini,” alisema.

Aliwataka wananchi wa Kagera wasifadhaishwe na kuhamishwa kwa Tossi, kwani amepewa majukumu yatakayomwezesha kuwatumikia Watanzania wote na si wa mkoa mmoja pekee.

Mugasa alisema chini ya madaraka yake mapya, SACP Tossi atahusika katika operesheni zinazohusisha vikosi mbalimbali ndani ya jeshi hilo.

Alivitaja vikosi hivyo kuwa ni Kikosi cha Usalama Barabarani, Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Kikosi cha Wanamaji, Kikosi cha TAZARA, Kikosi cha Reli, Mbwa na Farasi, Viwanja vya Ndege, Anga, Wizi wa Mifugo, Kikosi cha Mawasiliano na kuongeza kuwa atashughulikia majanga ya moto na utekaji nyara.

Mugasa alitoa maelezo hayo kutokana na uwezekano wa wananchi hawa wa Mkoa wa Kagera, kulalamikia hatua hiyo kutokana na ujasiri aliouonyesha Tossi mkoani humo, ambako hivu sasa alikuwa anatarajiwa kukamilisha kazi aliyoianza ya kuusafisha mkoa huo.

Katika mabadiliko megine ndani ya jeshi hilo, SACP Abdallah Msika, aliyekuwa Afisa Mnadhimu Fedha na Utawala Kanda Maalum Dar es Salaam, anakwenda kuchukua nafasi ya Tossi mkoani Kagera. Kabla ya kwenda Dar, Msika alikuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga.

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, (ACP) Isaya Mungulu, amepelekwa Makao Makuu ya Polisi, katika Kitengo cha Ukaguzi wakati Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, (ACP) Simon Sirro, amepelekwa kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga.

Aidha, ACP Mselem Mtulia, ameondolewa kutoka Makao Makuu ya Polisi na kuteuliwa kuwa Kamanda wa Kikosi cha TAZARA. Na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha TAZARA, (ACP) Henry Salewi, anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani.

Wengine ni aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, (ACP) Shaibu Ibrahim, anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga na (ACP) Liberatus Lyimo, anayetoka Upelelezi Makao Makuu Dar es Salaam, anakwenda Polisi Kanda Maalum, kuwa Afisa Mnadhimu wa Fedha na Utawala.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.