HALI katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) bado ni tete, kufuatia kusimamishwa kwa wanafunzi 56, ambao wengi wao ni viongozi wa serikali ya wanafunzi.
Jana uongozi wa UDSM ulilazimika kuomba ulinzi wa ziada kutoka vyombo vya dola, kufuatia tetesi za wanafunzi kupanga kufanya mgomo kushinikiza wenzao waliosimamishwa warejeshwe chuoni wakati matatizo yao yanashughulikiwa.
Wanafunzi walikuwa wamejiandaa kugoma lakini walitulizwa na viongozi wa serikali ya wanafuzni wa UDSM (Daruso), ambao waliwaomba watulie mpaka leo, wakati uongozi wa chuo hicho utakapotoa hatma ya wenzao waliosimamishwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Makamu wa Rais wa Daruso, ambaye kwa sasa anakaimu nafasi ya rais, Rushahu Bernadetha, alisema waliamua kusitisha mgomo wa wanafunzi baada ya kuombwa na uongozi wa chuo.
Maamuzi ya kufanya mgomo huo yalifikiwa juzi katika mkutano uliofanyika eneo maarufu la ‘Revolution Square’ kabla ya kikao hicho kufanywa tena jana na kukubali kusitisha mipango ya mgomo.
“Uongozi wa Chuo Kikuu umeomba mkutano huo uwe kesho (leo). Umesema tuwape muda watoe maamuzi baada ya wanafunzi hao kujieleza kwenye kikao kitakachowajadili,” alisema Bernadetha.
Alisema uongozi wa UDSM umetoa baraka zote kwa mkutano huo kufanyika leo saa 11:00 jioni.
Bernadetha alisema kuwa, jana saa 4:00 asubuhi, wanafunzi walibandika tangazo lao la kuitisha mkutano ambao ni lazima viongozi nao wawepo.
Alisema baada ya muda askari waliyabandua matangazo hayo na kubandika tangazo kutoka kwa uongozi ambalo liliwataka wanafunzi wasijihusishe na vitendo vyovyote vilivyo kinyume na pia kuwataka waingie madarasani.
Kwa mujibu wa makamu huyo wa rais wa Daruso, baada ya wanafunzi kutaka kufanya mkutano saa 4:00 asubuhi, uongozi wa Daruso uliwaomba mkutano huo ufanyike saa 7:00 mchana, ambapo walitumia muda huo kuongea na uongozi wa chuo kujua hatma ya wenzao.
Pamoja na mvua kunyesha, Tanzania Daima, ilishuhudia umati mkubwa wa wanafunzi waliokuwa wamekusanyika katika eneo ambalo walikuwa wafanyie mkutano, hadi baaada ya Makamu wa Rais kuwajulisha maamuzi waliyoafikiana na uongozi wa chuo hicho.
Alisema uongozi ulisitisha mkutano huo wa wanafunzi kwa sababu ulisema kuwa utahatarisha hali ya usalama chuoni hapo.
Lakini uongozi wa chuo ulionekana kujihami na hali hiyo kwa kuomba ulinzi wa ziada. Askari kutoka Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), makachero na polisi wa kawaida, walifika chuoni hapo na kuongeza ulinzi wakiwa na vifaa vyao.
Pamoja na vifaa vingine, askari hao walikuwa na mabomu ya machozi pamoja na gari maalumu la kutuliza ghasia linalotoa gesi ya kutoa machozi, maji yanayowasha pamoja na yale ya rangi kwa ajili ya kuwatambua watu walioshiriki katika vurugu.
Askari wa FFU walikuwa wameweka kambi katika maeneo tofauti karibu na chuo. Wapo waliokuwa wameweka kambi katika geti lililo karibu na Chuo cha maji cha Rwegalulira na wengine walikaa karibu na Kanisa la Full Bible Gospel Fellowship katika Barabara ya Sam Nujoma, karibu na Mlimani City.
Askari kanzu na mashushushu walionekana wakiwa wanazunguka katika maeneo mengi ya chuo huku baadhi yao wakiwa wamejichanganya na wanafunzi bila kujulikana.
Hata hivyo, Bernadetha alisema hali hiyo haiwatishi na wanasubiri kwa hamu maamuzi yatakayotolewa baada ya wenzao kuhojiwa na ikibidi, wataitisha mgomo kushinikiza wenzao warejeshwe chuoni.
Alikiri kuwa mgomo mwingine unanukia chuoni hapo endapo wenzao hawatarudishwa chuoni, kwani inaonekana kuwa wanafunzi wengi wana uchungu juu ya wenzao ambao hawajarejeshwa.
Alisema hatima ya mitihani iliyopangwa kuanza Jumatatu ijayo nayo inategemea kwa kiasi kikubwa maamuzi yatakayofikiwa leo na kamati itakayowahoji wanafunzi waliosimamishwa.
“Kuhusu suala la mitihani, tutakaa na kutathmini watu wote ndani ya bunge na kutoa tamko rasmi kesho,” alisema makamu huyo wa rais.
Alisema endapo wanafunzi hawataridhishwa na maamuzi ya kamati ya maadili, wapo tayari kugomeo mitihani hiyo. Hata hivyo, alikiri kuwa chuo kinajua kabisa hali ya kifikra iliyoko kwa wanafunzi endapo wenzao hawatarejeshwa.
Aidha, Bernadetha alionyesha kushangazwa na usumbufu anaoupata kutoka kwa baadhi ya watendaji chuoni hapo wakati anapoitisha mikutano ya baraza la viongozi wenzake.
“Napata usumbufu, nimeita baraza nasumbuliwa na askari wa chuo kwa kuulizwa nina haki gani ya kuitisha vikao. Hatuwezi kuzuia hali ya wanafunzi kama hali itakuwa tofauti,” alisema.
Alipoulizwa iwapo mgomo wao hautafanikiwa zitachukuliwa hatua gani, Bernadetha alisema kuwa viongozi wote wa Daruso wapo tayari kujiuzulu iwapo uongozi wa chuo utaendelea kukataa maombi yao.