Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kibao chawageukia wasiri wa IGP, DCI
Kibao chawageukia wasiri wa IGP, DCI
By Habari Tanzania | Published  05/17/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Christopher Nyenyembe, Mbeya


KUNDI la wazee kutoka Mkoa wa Mbeya ambalo hivi karibuni liliripotiwa kupeleka taarifa za siri za uhalifu za mkoa huo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, liko katika wakati mgumu.

Kikundi cha wazee hao wanaodai kuwawakilisha wenzao zaidi ya 160, jana kilijikuta katika mazingira magumu baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, kuwaita ofisini kwake na kuwapa onyo kali.

Akizungumza jana jioni ofisini kwake, Mwakipesile alisema kitendo cha wazee hao kutoa taarifa ovyo ovyo kinaharibu sifa za mkoa, hasa inapotokea kuwa taarifa hizo hutolewa kabla ya kufanyiwa utafiti wa kutosha.

Msimamo huo wa Mwakipesile aliyekuwa akihojiwa na gazeti hili ofisini kwake jana, siku moja tu baada ya kukutana na wazee hao, umekuja kutokana na wazee hao kutoa taarifa za uhalifu mkoani humo ambazo zinawahusisha baadhi ya maofisa wa polisi na viongozi wengine.

Miongoni mwa wazee hao yumo mkulima mmoja aliyepata kutangaza azma ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi vya siasa mwaka 1995, kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM), akitokea mkoani Mbeya, azma ambayo ilikwama katika hatua za awali.

Kwa upande wake, Mwakipesile alikikana kikundi hicho cha wazee ambacho kimekuwa kikitoa taarifa mbalimbali kwenye vyombo vya habari na kusema kuwa si rasmi, hakitambuliwi na uongozi wa mkoa huo na hajawahi kuonana na viongozi wake.

Alionyesha mshangao kusikia habari za uhalifu kuhusu Mkoa wa Mbeya zikipelekwa na wazee hao hadi Dar es Salaam, wakati yeye akiwa hana taarifa hizo, wakati wakifahamu fika kuwa mkoa huo unao viongozi wa serikali na kudai kuwa kitendo cha wazee hao kinaashiria uchochezi.

“Hawa wazee siwajui na hakuna mtu anayewazuia kutoa taarifa za uhalifu, wanachotakiwa lazima wafuate taratibu… kikundi kinachojulikana na kilichosajiliwa cha wazee ni cha Mbeya City Elders au UWAJIMBE, sasa hawa ambao hata siku moja sijawaona ofisini kwangu, sijui wanatoka wapi!” alisema Mwakipesile kwa mshangao.

Alisema kuna taarifa zisizokuwa rasmi zilizoifikia ofisi yake kuwa kuna baadhi ya wazee wanaojifanya kuwa ni watu wa Usalama wa Taifa, jambo ambalo ni la hatari, na kwamba taarifa hizo zinapaswa kuchunguzwa ili kubaini kama kuna ukweli wa madai hayo.

“Nimesikia kwamba wanajifanya Usalama wa Taifa, huo ni utapeli mkubwa, japokuwa sina ushahidi kamili… tumeanza kufanyia kazi madai hayo. Pia tuna habari kuwa wanawarubuni wafanyabiashara wa nyama wa Tukuyu ambao ndugu zao wanatuhumiwa kwa ujambazi na kesi ipo mahakamani… wanachukua fedha ili waweze kuwasaidia. Tukichunguza na kubaini hivyo, tutawapeleka mahakamani mara moja,” alisema Mwakipesile.

Alisema inashangaza wazee hao kwenda Dar es Salaam kutoa taarifa hizo wakati hawajawahi kwenda ofisini kwake na taarifa na wakapuuzwa.

Mwakipesile alisema hakizuii kikundi cha wazee hao kutoa taarifa kwa manufaa ya nchi, isipokuwa hawapaswi kuingilia kesi zilizopo mahakamani, kwa kuanza kuwarubuni watu kuwa wanao uwezo wa kuwasaidia.

Tanzania Daima ilifanikiwa kukutana na baadhi ya wazee hao walioitwa na mkuu wa mkoa huo, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuhifadhi Mazingira Mkoa wa Mbeya (MRECA), William Mwamalanga, wakisubiri kuingia ofisini kwa madai kuwa wamepokea taarifa za vitisho.

Akizungumza na gazeti hili huku machozi yakimtoka, Mwamalanga alisema kuwa kitendo cha kuitwa na kuelezwa kuwa wao ndio watoaji wa taarifa za uhalifu za mkoa huo, kinaweza kuwaingiza matatani, kwa kuwa taarifa hizo ni za siri na zimekuwa zikitolewa bila wahusika kujulikana.

“Kinachoniliza ni wananchi hawa wazee wakivamiwa watauawa kwa sababu majambazi ni watu wa hatari, mkuu wa mkoa ni mlinzi wa amani na amedai kuwa taarifa iliyopelekwa kwa (Robert) Manumba (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai - DCI) haitashughulikiwa, wakati taarifa hiyo ilikuwa ya siri,” alisema huku akilia.

Alisema kuwa kikundi hicho kimekuwa kikifanya kazi ili kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete, alilotoa akiwataka wananchi kupeleka taarifa kwake na kwa viongozi wanaoweza kutunza siri, hasa za matukio yanayohusiana na ujambazi.

Baadhi ya wazee wanaounda kundi hilo, wanadai kuwa Mkoa mzima wa Mbeya una idadi ya wazee 160,000, ambao wamekuwa wakifanya kazi za kufichua wahalifu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.