HABARI kubwa katika gazeti hili leo, ni ile inayozungumzia kufika katika hatua za mwanzo za mwekezaji aliyeshinda zabuni ya kukodishwa uendeshaji wa miundombinu ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), kuanza kuliendesha rasmi.
Kwa maelezo yoyote yale, habari hiyo inao umuhimu mkubwa kabisa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Tanzania baada ya kazi ya kuanza kwa mchakato huo kuchukua miaka takriban mitano sasa.
Umuhimu wa shirika hilo ambalo harakati za kulikodisha zilianza mapema mwaka 2002, chini ya usimamizi wa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) uko wazi.
Reli ya Kati yenye urefu wa kilometa 2,707 ikiunganisha mikoa mbalimbali ya Tanzania, imekuwa kitovu muhimu kabisa cha maendeleo ya uchumi wa taifa hili na baadhi ya nchi jirani.
Mwenendo wake wa kusuasua na kuzorota kwa uwezo wake wa kusafirisha mizigo katika maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi yetu, kwa kiwango kikubwa yameathiri hali ya uchumi wa taifa.
Wakati ikiwa katika hali nzuri, Reli ya Kati iliyojengwa zaidi ya miaka 100 iliyopita ndiyo iliyokuwa njia yenye uhakika zaidi katika kusafirisha mizigo na abiria kwa maelfu kati ya Dar es Salaam na mikoa ya Dodoma, Tabora, Shinyanga, Kigoma na Mwanza kwa upande mmoja na Tanga, Kilimanjaro na Arusha kwa upande mwingine.
Kudorora kwa huduma katika reli hiyo kwa kiwango kikubwa kuligeuka na kuwa mzigo mkubwa kwa wasafiri, wafanyabiashara, bandari zetu za Dar es Salaam na Tanga na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ni kwa kutambua umuhimu wa reli hiyo, ndiyo maana taarifa za hivi karibuni kutoka serikalini zinazoonyesha kuanza kupatikana kwa mwanga mwema, zikawa ni za matumaini makubwa katika kipindi kifupi kijacho.
Aidha, taarifa kwamba, mara baada ya mwekezaji mpya kukabidhiwa uendeshaji wa reli hiyo safari za kati ya Dar es Salaam na mikoa mingine zitarejeshwa baada ya kusitishwa kwa muda mrefu, ni za faraja kwa Watanzania wanaoipenda nchi yao.
Lakini kikubwa katika safari hizo ni taarifa kwamba, kwa sababu ya mahitaji yaliyopo, kutakuwa na safari sita za treni za abiria kwa wiki zinazoanzia Dar es Salaam, zinaleta faraja ya kumalizika kwa shida kubwa ya usafiri kati ya jiji hilo na mikoa ya kati ya Tanzania na ile ya Kanda ya Ziwa na magharibi.
Aidha, taarifa za hivi karibuni zilizokuwa zikionyesha kuwa serikali ilikuwa ikilazimika kutoa ruzuku ya shilingi milioni 60 kila siku ili kuinusuru TRC iliyokuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi ni jambo jingine ambalo tunaamini litakoma baada ya mwekezaji mpya kuanza kazi.
Kama hiyo haitoshi, tunaamini kwamba, kuporomoka kwa mapato kutoka sh milioni 143.89 kwa siku Novemba 2005 kulikofia sh milioni 83.19 kwa siku, Novemba mwaka jana, litakuwa ni jambo la kihistoria na badala yake tutashuhudia kupanda kwa mapato ya shirika hilo na hatimaye pato la taifa.
Kwa sababu hiyo basi, tunapenda kuiasa serikali kuupa uzito unaostahili mchakato huo wa kulikodisha shirika hilo muhimu kitaifa, hali ambayo hatimaye itakuwa ni ya manufaa kitaifa.
Tunasema hivi kwa sababu tunaamini kwamba, ukodishwaji wenye mafanikio hatimaye utamaliza msongamano wa matatizo ya kiuendeshaji na kimtaji yanayoikabili TRC kwa sasa, sambamba na kumaliza matatizo mengi mengine waliyoanza kuwa nayo Watanzania wengi tangu shirika hili lilipoanza kuyumba hata kufikia hatua ya kufa kabisa.