SERIKALI imewazawadia wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita, iliyofanyika mwaka jana na matokeo yake kutangazwa hivi karibuni na Baraza la Mitihani la Taifa.
Zawadi hizo zinajumuisha kompyuta 12, pamoja na fedha taslimu sh milioni 6.5, zilizotolewa kwa wanafunzi 12 waliofanya vizuri katika mitihani hiyo.
Hafla ya utoaji wa zawadi hizo, ilifanyika jana katika Ikulu Ndogo ya Chamwino, nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma, na kuongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Kikwete, alisema kuwa zoezi la kutoa zawadi kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani ya kuhitimu masomo kwenye ngazi mbalimbali, linapaswa kuwa endelevu.
Alisema zoezi hilo linapaswa kuwa endelevu kwa sababu kutolewa kwa zawadi kwa wanafunzi wanaofanya vizuri kunaleta hamasa kwa wanafunzi wengine kuongeza bidii katika masomo yao ili nao waje wazawadiwe.
Kila mmoja kati ya wanafunzi 12 waliofanya vizuri alipatiwa cheti, kompyuta pamoja na sh 500,000, isipokuwa mwanafunzi mmoja ambaye alipatiwa sh milioni moja.
Rais Kikwete alisema kuwa upo uwezekano mkubwa wa wanafunzi waliopo shuleni kupunguza uzembe na
kuongeza bidii katika masomo baada ya kuona wenzao wanaofanya vizuri wanapatiwa zawadi.
Alitoa changamoto kuwa pamoja na wanafunzi wa sekondari kuzawadiwa, upo umuhimu wa kuhakikisha kuwa zawadi pia zinapaswa kutolewa kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika madaraja mbalimbali ya elimu ikiwamo elimu ya juu.
Rais Kikwete aliwapongeza walimu na wanafunzi hao kwa kazi nzuri ya usikivu na ufundishaji ambayo imewafikisha katika hatua hiyo ya kuifanya nchi ijivunie kwa kuwa na wasomi wanaostahili pongeni.
Aliwapongeza wanafunzi hao kwa kuzingatia masomo na kuacha kufuatilia muziki wa kisasa ujulikanao kama Bongo Flava, kama ilivyo kwa wanafunzi wengi wa sasa wenye mapenzi na muziki huo.
Awali, akitoa taarifa kuhusiana na wanafunzi hao, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Margaret Sitta, alisema kuwa wanafunzi hao wamegawanyika katika makundi manne ambayo miongoni mwao wapo wanafunzi wa shule za serikali na zile zisizo za serikali.
Alisema kundi la kwanza ni la vijana waliofanya vizuri kutoka shule za sekondari za serikali ambao ni Martin Chegere kutoka Shule ya Sekondari Pugu, Japhet Frederick (Mwika) na Ditrick Rwegasira kutoka Kibaha Sekondari.
Kundi la pili ni la wasichana waliofanya vizuri kutoka shule za sekondari za serikali ambao ni Nhandala Daudi kutoka Dakawa, Zuhura Ally wa Nangwa Sekondari na Doreen Tesha kutoka Kilakala.
Kundi la tatu ni la wavulana watatu kutoka shule zisizo za serikali, ambao ni Prosper Mrutu (Feza), Mohamed Nassor (Feza) na Moses Mwageni (Mt Joseph Kilocha).
Kundi la nne ni la wasichana waliofanya vizuri kutoka shule ambazo si za serikali ambao ni Tabu Said (Mukidoma), Augusta Kamule (Mt Mary) na Jane Nelson (Sangu).
Chegere, ambaye ameibuka mwanafunzi bora nchini, ndiye aliyezawadiwa sh milioni moja, cheti na seti ya kompyuta.