WAKATI Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kimetangaza kuwazuia wanafunzi 36 kurejea chuoni, uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) umewataka wanafunzi 56 wa shahada ya awali waliosimamishwa masomo, kufika chuoni leo kwa ajili ya kuchukua barua zao.
Taarifa ya Kaimu Mkuu wa SUA, Profesa Magishi Mgasa, iliyotolewa jana, inasema uongozi wa chuo hicho umeamua kurejeshwa kwa wanafunzi hao ili kuiachia bodi ya mikopo kutambua wenye uwezo wa kulipa na wale wasio na uwezo.
“Tumeachia bodi ya mikopo itambue nani anastahili kulipa na nani asamehewe, hivyo wanafunzi wote isipokuwa 36 ambao majina yao tuliyataja awali, hao hawaruhisiwi kurejea,” alisema Profesa huyo.
Alisema kuwa wanafunzi hao watatakiwa kuripoti kwa wakuu wao wa idara au wa vitivo na kujaza fomu za mikopo na kutakiwa kuzirejesha katika bodi ya mikopo kabla ya Juni 30 mwaka huu.
Aidha, alisema kuwa kila mwanafunzi atapitia kipimo maalumu cha kuangalia uwezo wake wa kipato katika familia wanazotoka, kwa lengo la kubaini wanaostahili msamaha na wasiostahili.
Alisema kuwa baada ya kipimo hicho wale wote watakaoonekana wana uwezo wa kulipa, watatakiwa kulipa asilimi 40 na gharama zingine kwa mwaka ujao na ndipo wataruhusiwa kurejea chuoni hapo.
Hata hivyo, Profesa Mgasa alisema kuwa baada ya kipimo hicho, wanafunzi wote watajaza fomu kwa lengo la kukubaliana na matokeo ya kipimo hicho.
Pia alisema kuwa wanafunzi hao watapatiwa namba ya mtihani kwa ajili ya utambulisho wawapo chuoni hapo.
Vile vile aliwataka wanafunzi wa mwaka wa pili, ambao hawakuandika barua za kuomba msamaha na walioandika kurejea chuoni hapo na risiti zao au barua.
Wanafunzi hao walisimamishwa masomo Aprili 18 mwaka huu, kutokana na kugoma kuingia madarasani wakiishinikiza serikali iwapatie mkopo wa asilimia 100 badala ya utaratibu wa sasa unaowataka wachangie asilimia 40.
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa UDSM, Julius Saule, aliliambia gazeti hili jana kuwa wanafunzi 56 wa chuo hicho waliosimamishwa wanatakiwa kuchukua barua zao kwa wakuu wao wa vitivo vya huduma za wanafunzi leo.
Kwa mujibu wa Saule, wanafunzi hao ni wale wa sehemu ya Mlimani, Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi na Usanifu wa Majengo (UCLAS), Chuo kikuu kishiriki cha Walimu cha Chang’ombe (DUCE) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Walimu cha Mkwawa (MUCE).
“Wanafunzi wote waliosimamishwa masomo wanatakiwa kufika chuoni kesho (leo) kuchukua barua zao za kutoa maelezo,” alisema Saule.
Naye Kaimu Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa UDSM (Daruso), Ali Selemani, alisema kuwa, wenzao waliosimamishwa watatakiwa kujaza barua hizo ambazo zitawaruhusu kuingia kwenye kamati ya nidhamu kesho Alhamisi.
Alisema kamati hiyo ndiyo itakayosikiliza maelezo yao ili kubaini wenye makosa.
Awali, uongozi wa Daruso ulisema kuwa unaendelea kujadiliana na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ili kujua hatima ya wanafunzi wenzao 56 waliosimamishwa.
Selemani alisema baada ya wanafunzi wa shahada ya awali kurejeshwa chuoni Jumatatu wiki hii, Daruso imekuwa na mazungumzo na uongozi wa chuo ili kuona ni jinsi gani wenzao watarejeshwa.
“Tumekuwa tukiusihi uongozi wa chuo juu ya wenzetu waweze kurudi na kama kuna taratibu nyingine ziendelee kufanyika wakiwa chuoni. Tunapenda Jumatatu ijayo tuweze kuanza nao mitihani.
“Chuo kiko tayari kuzungumza, na sisi tuko tayari kuzungumza nao juu ya suala hili la wenzetu,” alisema Selemani.