Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  TRC kutoka ICU
TRC kutoka ICU
By Habari Tanzania | Published  05/16/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu


BAADA ya kipindi kirefu cha kusuasua usafiri wa Reli ya Kati unaoanzia Dar es Salaam kwenda mikoani, uko katika hatua za kurejeshwa chini ya mwekezaji mpya.

Habari kutoka serikalini zilizothibitishwa na maofisa wa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) zinaeleza kwamba, mkataba rasmi kati ya mwekezaji mpya na serikali utakaopitisha kuanza kwa safari hizo za kila siku kwa treni za abiria na mizigo unaweza kusainiwa wakati wowote kuanzia sasa.

Kikubwa kilichoivuta serikali kufikia makubaliano na wawekezaji hao kutoka India ni uamuzi wao wa kuwa na safari sita za treni ya abiria kwa wiki, zitakazoanzia Dar es Salaam kuelekea mikoani, hususan katika mikoa ya Tabora, Mwanza na Kigoma.

Habari hizo zinaeleza kuwa makabidhiano ya uendeshaji wa Reli ya Kati, kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni mpya itakayoendesha reli hiyo ya Tanzania Railways Limited (TRL), yatafanyika wakati wowote kuanzia sasa.

Makabidhiano hayo yatafuatia kukamilika kwa mchakato mzima wa kutafuta mwendeshaji mpya wa reli hiyo, baada ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) kukumbwa na matatizo makubwa ya kifedha na uchakavu wa miundombinu, yakiwamo mabehewa na reli yenyewe.

Iwapo kweli mipango hiyo itafanikiwa, basi kiasi cha shilingi milioni 60 ambacho serikali hulazimika kukitoa kila siku kwa TRC kama ruzuku ili kuliokoa shirika hilo lisife kitakoma.

Aidha, kusainiwa kwa mkataba huo kunaweza kukawa habari njema kwa wafanyakazi wa shirika hilo ambao baadhi yao wanatarajia kulipwa mafao yao baada ya mwekezaji mpya kukabidhiwa jukumu la kuanza kuendesha shughuli za sasa za TRC.

Akizungumza na Tanzania Daima mwanzoni mwa mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Linford Mboma, alikiri kwamba hali ya kifedha katika shirika hilo ilikuwa imefikia hatua mbaya.

Mboma aliiambia Tanzania Daima kuwa, shirika hilo limekuwa likipokea kiasi cha sh bilioni mbili kwa mwezi, sawa na wastani wa sh milioni 60.7 kwa siku kutoka serikalini kama ruzuku ya kujiendesha.

Aidha, alisema shirika hilo limekuwa likijiendesha kwa hasara kubwa kutokana na kuendelea kuporomoka kwa mapato yake.

Takwimu za hadi Januari zilikuwa zikionyesha kuwa, mapato ya shirika hilo yalikuwa yameporomoka kutoka sh milioni 143.89 kwa siku, Novemba 2005 hadi kufikia sh milioni 83.19 kwa siku Novemba mwaka jana.

Kutokana na kuporomoka kwa mapato, serikali ilijikuta ikilazimika kulipatia shirika hilo ruzuku ili kuliona likiendelea kujikongoja hadi hapo mchanganuo kamili wa kumkabidhi mwekezaji mpya kutoka India utakapokamilika.

Mboma aliieleza Tanzania Daima wakati huo kwamba, shirika hilo bila ya mwekezaji lilikuwa halina uwezo wa kurejesha usafiri wa treni kutoka bara kuja Dar es Salaam, hadi hapo mwekezaji atakapokuwa amekabidhiwa kutokana na upungufu mkubwa wa vitendea kazi, vikiwamo injini na mabehewa.

Taarifa za kutoka ndani ya PSRC zinaonyesha kuwa, Kampuni ya Tanzania Railways Limited (TRL) itakayokabidhiwa TRC itaundwa kwa pamoja na wabia mbali mbali, wabia wakubwa katika kampuni hiyo wakiwa ni Kampuni ya RITES ya India na Benki ya UTI kutoka huko huko India, ambazo kwa pamoja zitamiliki asilimia 51 ya hisa ndani ya kampuni mpya wakati serikali itakuwa ikimiliki asilimia 49 ya hisa zilizosalia.

Makubaliano kati ya serikali na mwendeshaji huyo, yanaonyesha kuwapo safari nne za treni kati ya Dar es Salaam, Mwanza na Kigoma kila wiki, na safari mbili za moja kwa moja.

Moja ya safari hizo mbili itaanzia Dar es Salaam hadi Mwanza na kurudi, wakati nyingine itatoka Dar es Salaam hadi Kigoma na kurudi Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa habari hizo, safari hizo nne zitaanzia Dar es Salaam, kwa kuwa na mabehewa manane, ambayo yataongezewa matatu treni hiyo ikifika Morogoro, moja jingine litaongezwa ikifika Dodoma na hatimaye kuwasili Tabora ikiwa na jumla ya mabehewa 12.

Mjini Tabora, kwa mujibu wa habari hizo, treni hiyo itagawanywa katika sehemu mbili, moja ikienda Mwanza na nyingine ikienda Kigoma.

Ile ya Mwanza itaongezewa mabehewa matatu na ile itakayokwenda Kigoma itaongezewa mabehewa matatu, na hivyo kuifanya treni hiyo kuwasili Mwanza ikiwa na mabehewa 10, na ile ya Kigoma ikiwa na mabehewa tisa. Safari za kurudi Dar es Salaam zitakwenda kwa utaratibu huo huo.

Kuhusu safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, na kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma, habari zinasema kuwa safari hizo zitakuwa na mabehewa matano kila moja, na zitafanyika mara moja kwa wiki, bila kuongezwa na kupunguzwa mabehewa mengine njiani.

Habari hizo pia zinasema kuwa baada ya makabidhiano hayo, safari nyingine zote za treni kwa ajili ya abiria na mizigo zitafunguliwa katika njia nyingine za reli kwenye njia hiyo ya Reli ya Kati.

Kwa mfano, kutakuwapo na safari tatu za treni kila wiki kwenye njia hiyo kati ya Tabora na Mpanda kupitia Kaliua, na pia safari tatu kwa wiki kati ya Dodoma na Singida kupitia Manyoni.

Kwa sasa njia ya Reli ya Kati inakabiliwa na matatizo makubwa, ukiwamo ukachakavu mkubwa wa njia ya reli ambao umesababisha kusimamishwa kwa safari za treni kati ya Dodoma na Dar es Salaam.

Serikali kupitia PSRC, imekuwa inafanya juhudi za kupata mwekezaji ambaye ataiendesha Reli hiyo ya Kati iliyojengwa kiasi cha miaka 100 iliyopita, kuendesha usafiri katika reli hiyo na kuwekeza kwa pamoja katika reli hiyo kati yake na Serikali ya Tanzania.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, usafiri wa abiria kwa kutumia reli hiyo kuelekea bara unaanzia Dodoma, na mwanzoni ilielezwa kuwa usafiri huo ungerejeshwa Dar es Salaam baada ya kukamilika kwa matengenezo ya njia ya Reli ya Kati, ya Dar es Salaam na Dodoma.

Hali hiyo imezidi kupoteza matumaini ya wakazi wa mikoani, hasa Kanda ya Ziwa na Kigoma, ambao usafiri huo umekuwa mkombozi mkubwa kwao kutokana na barabara nyingi kutokupitika wakati wa mvua na nauli za magari kupanda kiholela.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.