MJI wa Dodoma umefunikwa na idadi kubwa ya wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliowasili hapa tayari kuanza kikao cha Mkutano Mkuu wa Saba wa chama hicho.
Maelfu ya watu - wajumbe wa mkutano mkuu huo, maafisa wa serikali, wasaidizi wao, wafanyabiashara na viongozi mbalimbali, wapo mjini hapa kwa ajili ya mkutano huo.
Kama ilivyo ada, wapambe nao idadi yao si haba. Hawa ni wale wasiotaka kukosekana kwenye shughuli kama hizi, huku wakiwa wamevalia mavazi yenye rangi za CCM, na kutembea kwa madaha wakimfurahisha kila mjumbe.
Wajumbe wa mkutano huo ambao ni zaidi ya 1,500, walianza kuwasili hapa mapema wiki hii, hasa kwa wale wanaotoka sehemu zenye shida ya usafiri.
Wanaungana na wenzao ambao ni wabunge wa CCM walioko katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Kwa wiki mbili sasa, wapo katika Mkutano wa Bunge la Bajeti utakaoendelea hadi Agosti 15, mwaka huu.
Idadi ya wajumbe hao, ikijumuishwa na mamia ya maafisa wa serikali, madereva na watumishi wengine kutoka mikoa mbalimbali, inaufanya mji wa Dodoma “usipumue”.
Pamoja nao, kuna kina dada wafanyabiashara ya asili kutoka mikoa mingi, hasa Dar es Salaam , Arusha, Mbeya, Iringa, Singida na Mwanza. Hawa wapo makini kwani wanajua kuwa kwa siku hizi mbili, watapata soko la uhakika.
Wamekuwa wakionekana karibu kila baa na katika kumbi nyingine za starehe. Imekuwa rahisi kuwatambua kutokana na ukarimu wao.
Nyumba za wageni zimejaa wapangaji. CCM, kwa kutambua kuwa watu wangekuwa wengi, walilipia vyumba katika gesti nyingi tangu Aprili, mwaka huu.
Ndiyo maana wapangaji wengine, walio kwenye shughuli za Bunge, wamejikuta wakitakiwa wawapishe wajumbe wa Mkutano Mkuu.
Hali hiyo imewalazimu wengine watumie chumba kimoja, alimradi tu kuhakikisha wanamaliza kipindi hiki kigumu kwao.
Bei ya vyakula, iko juu. Nyama zilizochomwa, za kuku, mbuzi au ng'ombe, hazishikiki. Kwa waliotoka Dar es Salaam , hawaoni tofauti ya bei.
Kuku aliyechomwa anauzwa kuanzia sh 4,000 hadi sh 5,000.
Mlo wa ugali na samaki, au wali kwa samaki, nao haushikiki. Chini ya sh 2,000 kwa sahani, mtu anaweza kulala au kushinda bila kula.
Mkutano Mkuu unaanza leo katika Ukumbi wa Chimwaga, kwa kufunguliwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais mstaafu Benjamin Mkapa.
Dondoo zitakazowasilishwa mkutanoni ni pamoja na taarifa ya kazi ya chama, taarifa za serikali za utekelezaji wa Ilani na Mwelekeo 2000-2010.
Serikali zote mbili, ya Muungano na Zanzibar , zitatoa taarifa.
Nyingine ni majadiliano ya taarifa zote, Mkapa kutangaza uamuzi wake wa kung'atuka, uchaguzi wa Mwenyekiti wa CCM, kutolewa kwa zawadi za mikoa kwa Mwenyekiti, na mwisho itakuwa ni kufunga mkutano. Dondoo hizo ni za siku zote mbili.
Kesho saa 4:00 hadi saa 4:30 asubuhi; kama mambo yatakwenda kwa mujibu wa ratiba, Mkapa atatangaza uamuzi wake wa kung'atuka.
Baada ya hapo, utasomwa wasifu wa mgombea nafasi ya Mwenyekiti. Mgombea pekee ni Rais Jakaya Kikwete.
Ratiba inaonyesha kuwa, kutakuwapo na burudani za muziki, ngonjera na utenzi.
Mkutano huu ni wa saba kwa uhai wa CCM, tangu ilipozaliwa Februari 2, 1977.