MARA baada ya kurejea chuoni jana, viongozi wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), ambao hawajasimamishwa, waliitisha kikao, ambacho moja ya ajenda zake kubwa ni kutafuta namna ya kuwatetea viongozi wenzao waliosimamishwa.
Mmoja wa viongozi wa Daruso ambaye alirejea chuoni jana baada ya msamaha wa jumla, alilithibitishia gazeti hili kuwa, wamepanga kutafuta mbinu za kuwatetea wenzao ili warejeshwe chuoni ‘kwa gharama yoyote ile.’
“Tunaendelea na kikao chetu na hoja kubwa ni kutafuta namna ya kuwarejesha wenzetu chuoni kwa gharama yoyote,” alisema kiongozi huyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Mmoja wa viongozi wa Daruso aliyesimamishwa alisema kuwa, pamoja na wao kusimamishwa, bado Serikali ya Daruso ipo na Makamu wa Rais wa serikali hiyo, Benadeta Lushahu ndiye anayekaimu nafasi ya rais aliyesimamishwa.
“Makamu wa Rais hajasimamishwa. Serikali ya Daruso ipo na bado wanaweza kukaa vikao vya maamuzi kwa ajili ya kuwatetea wenzao,” alisema.
Tanzania Daima jana ilishuhudia umati wa wanafunzi waliorejea chuoni hapo wakijaza fomu maalum zilizowataka kuahidi kutii masharti yote yaliyowekwa na uongozi wa chuo hicho.
Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Rwekaza Mukandala jana alikataa kuzungumza na waandishi wa habari, ambao walitaka kupata maelezo mbalimbali kutoka kwake likiwamo lile linalohusu hatima ya wanafunzi waliosimamishwa.
Pamoja na waandishi wa habari kumweleza nia ya kutaka ufafanuzi huo, Prof. Mukandala alimtuma msaidizi wake na kuwaeleza waandishi wa habari kuwa, taarifa zote zinapatikana katika ofisi ya uhusiano chuoni hapo.
Hata hivyo, Afisa Uhusiano wa chuo hicho, Julius Saule, alipofuatwa, alisema alikuwa hana habari mpya wala hakuwa na lolote la kuzungumza na waandishi.
Waandishi wa habari walipomfuata kwa mara nyingine tena Prof. Mukandala, hakuwa tayari kusema lolote na badala yake akaonekana akichukua mkoba wake na akaondoka na gari yake yenye namba za usajili SU 35959 aina ya Land Cruiser.
“Kwa leo sina la kuzungumza, wala siko tayari kujibu maswali,” alisema Prof. Mukandala huku akiwa anatoka nje ya mlango wake ambapo aliongozana na waandishi wa habari hadi alipoingia kwenye gari lake na kuondoka.
Jumamosi iliyopita, uongozi wa chuo kikuu hicho, ulitangaza uamuzi wake wa kuwarejesha wanafunzi wote wa shahada ya awali waliosimamishwa, isipokuwa wanafunzi 56 ambao wamesimamishwa kwa muda usiojulikana.
Kwa maelezo ya Prof. Mukandala, wanafunzi hao waliosimamishwa, wanatakiwa watoe maelezo zaidi kuhusu kushiriki kwao kwenye mgomo huo, na wale watakaoonekana hawakuwa vinara wa mgomo, ndio watakaoruhusiwa kuendelea na masomo.
Katika kampasi ya Mlimani, wamesimamishwa wanafunzi 22, Chuo Kishiriki cha Ualimu Chang’ombe (DUCE) wanafunzi 11, Chuo Kishiriki cha Ualimu Mkwawa (MUCE) wanafunzi sita na Chuo cha Ardhi na Usanifu wa Majengo (UCLAS) wanafunzi 16.