Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Anglikana sasa vurugu tupu
Anglikana sasa vurugu tupu
By Habari Tanzania | Published  05/13/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Rahel Chizoza, Dodoma


UFA unaosababishwa na matendo ya ushoga umezidi kuongezeka katika Kanisa la Anglikana hapa nchini.

Ufa ambao hapo awali ulikuwa ukitishia kuwagawa viongozi wa kanisa hilo, sasa umeanza kuwagawa waumini wa kanisa hilo, ambao tofauti na viongozi, wao wamekuja na msimamo mmoja wa kupinga vitendo vya ushoga.

Katika hatua ambayo haikutarajiwa na wengi, waumini wa kanisa hilo wa Parishi ya Chimuli, jana waliwakataza watoto wao kupokea Sakramenti ya Kipaimara iliyokuwa ikitolewa na Askofu Godfrey Mdimi Muhogolo, wa kanisa hilo Dayosisi ya Dodoma kwa madai kuwa anaunga mkono ushoga.

Waumini hao waliamua kufunga kanisa hilo kwa kufuli na kubandika tangazo kuwa hakukuwa na kipaimara kanisani hapo, baada ya kubaini kuwa mhusika ni Askofu Muhogolo, ambaye amekuwa akitajwa kuwa kiongozi wa kanisa hilo anayeunga mkono vitendo vya ushoga.

Baada ya kufungwa kwa kanisa hilo, waumini wote hata waliokuwa na shida nyingine kanisani hapo walishindwa kuingia ndani hadi baada ya polisi kufika, ambapo kiliitishwa kikao cha dharura cha viongozi wa kanisa hilo kwa ajili ya kutafakari hali hiyo.

Waumini hao ambao walifika kanisani hapo kwa ajili ya ibada ya Kipaimara, walibadili msimamo wa kushiriki katika ibada hiyo baada ya kutaarifiwa kuwa Askofu Muhogolo ndiye ambaye angewawekea mikono kichwani watoto, wakati wakipokea sakramenti hiyo.

Wakieleza sababu za kuwazuia watoto wao kuwekewa mikono na askofu huyo, walisema iwapo watawaruhusu watoto wao kuwekewa mikono na askofu huyo, itakuwa ni ishara ya kuunga mkono vitendo vya ushoga.

“Hatuwezi kukubali awawekee mikono watoto wetu maana na sisi tutaonekana tunaunga mkono vitendo vya ushoga kama yeye, labda tuletewe askofu mwingine,” alisema mmoja wa waumini hao waliokuwapo nje ya kanisa hilo la Chimuli.

Mmoja wa waumini hao ambaye pia ni mchungaji aliyeachishwa kazi na askofu huyo kutokana na hatua yake ya kupingana na askofu huyo kuhusu matumizi ya kondomu kwa waumini, aliyejitambulisha kwa jina la Elia Mbalaga, alisema askofu huyo amewachosha waumini kwa vitendo ambavyo vipo kinyume cha maadili ya dini.

Alimlaumu kwa upotoshaji mkubwa wa mafundisho ya dini na sheria za nchi kwa maelezo kuwa mtu yeyote anavyochochea ushoga anakuwa anahalalisha ushoga, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi.

“Kama ushoga ni halali, basi waliofungwa kwa kulawiti waachiwe huru, maana hawana Kosa, lakini kama haukubaliki, sisi pia hatukubaliani na yeye,” alisema mchungaji huo.

Alibainisha kuwa kukataliwa kwa askofu huyo kumedhihirisha wazi matendo yake mabaya katika jamii, kwani waliomkataa ni waumini waliokuwa wakiongozwa naye awali.

Alisema anao ushahidi kuwa viongozi wote wanaomuunga mkono Muhogolo katika Dayosisi ya Dodoma wamepewa rushwa ili waendelee kumlinda na kumtetea.

Mchungaji huyo aliendelea kueleza kuwa mara nyingi askofu huyo amekuwa mstari wa mbele kutetea mambo yanayohusu zinaa, likiwamo suala la ushoga na matumizi ya kondomu kwa waumini, badala ya kukataza zinaa, kwani kutetea kondomu si kazi yake.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Vijana, Dinali Dickson Ndolosi, alisema walikwisha kumwandikia barua askofu huyo kwamba atoe maelezo kuhusu kuunga mkono ushoga lakini hakujibu.

Alisema parishi zote zilimwandikia barua askofu huyo kuhusu suala hilo huku zikimtaka arekebishe kauli yake kupitia vyombo vya habari, hata hivyo hakufanya kama alivyotakiwa na ndipo uamuzi wa kumsuburi siku ya kipaimara ulipofikiwa.

Ndolosi alieleza kuwa wanachokikataa wao ni askofu, lakini si watoto wao kuwekewa mikono, hivyo angepatikana askofu mwingine walikuwa tayari kuruhusu ibada hiyo iendelee.

Askofu Muhogolo alifika kanisani hapo majira ya saa nne na nusu na kukuta watu wote wakiwa nje ya kanisa huku likiwa limefungwa.

Alipokewa kwa kelele za kumzomea na kuelezwa kuwa hatakiwi kuonekana katika oneo la kanisa hilo.

Alipofika kanisani hapo alikwenda moja kwa moja kwenye mlango wa kanisa na kubandua tangazo lililokuwa limebandikwa mlangoni, lililokuwa likisomeka, “KULINGANA NA TUHUMA ZA ASKOFU NA DCT, KIPAIMARA HAKUNA KWA KANISA LOLOTE”.

Baada ya kubandua tangazo hilo, askofu aliingia ndani ya ofisi ya mchungaji ambako aliungana na viongozi wengine wa kanisa kwa ajili ya kuendelea na kikao lakini waumini waliokuwa na hasira walibandika tangazo jingine lenye ujumbe kama wa awali.

Baada ya kikao hicho kwisha, waliamua kuhamia katika kanisa jingine la Ipagala, ambako ibada nyingine ilikuwa ikiendelea chini ya ulinzi mkali wa polisi wenye silaha, akiwamo Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Dodoma.

Askofu Muhogolo ambaye alifanikiwa kuongoza ibada katika kanisa hilo, aliwaeleza waumini wa kanisa hilo kuwa wanaomkataa kiongozi wa kanisa na kufanya fujo pasipo kufuata utaratibu, wanao uhuru wa kuabudu katika kanisa lolote watakalopenda.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.