RAIS Jakaya Kikwete, amemteua aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Omari Mapuri na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Adadi Rajabu kuwa mabalozi wa Tanzania nchi za nje.
Kwa hali hiyo, Mapuri ambaye hadi uteuzi huu unafanyika alikuwa Katibu Mwenezi wa Itikadi na Sera wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameaga rasmi nafasi hiyo aliyosusiwa na waandishi wa habari mwaka jana.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu Dar es Salaam jana, ilisema Mapuri ameteuliwa kuwa Balozi nchini China wakati Adadi, anakwenda Harare , Zimbabwe .
Mapuri anaziba nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Charles Sanga, aliyeteuliwa kuwa Mshauri wa Rais katika Masuala ya Kidiplomasia wakati Adadi anachukua nafasi ya Brigedia Hassan Hashim Mbita ambaye amemaliza mkataba wake.
Wengine walioteuliwa na nchi wanazokwenda kwenye mabano ni Mwanaidi Sinare Maajar ( London , Uingereza), Ahamada Rweyemamu Ngemera (Ujerumani) na Hussein Said Khatib ( Muscat- Oman ).
Mwanaidi ni wakili wa kujitegemea na mshauri wa masuala ya sheria na anachukua nafasi ya Balozi Hassan Gumbo Kibelloh anayehamishwa kituo kutoka Uingereza na kwenda Ufaransa kujaza nafasi iliyoachwa na Balozi Juma Mwapachu. Mwapachu ameteuliwa kuwa Katibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wa Balozi Ngemera, anachukua nafasi ya Balozi Ali Abeid Karume ambaye atapangiwa kazi nyingine. Balozi Ngemera kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hadi Machi mwaka huu ambako alisimamia masuala ya fedha na utawala.
Mapuri, akiwa Katibu Mwenezi wa CCM, alisusiwa na waandishi wa habari mwaka jana baada ya kutoa taarifa ya kuwadhalilisha. Tangu wakati huo, licha ya kuwa msemaji wa CCM, hakupata ushirikiano wa waandishi na CCM iliacha kumtumia katika utoaji wa taarifa za chama.
Mapuri alikuwa mmoja wa wabunge kumi walioteuliwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa na kuukwaa Uwaziri wa Mambo ya Ndani.
Leo CCM inafanya mkutano wake mkuu mjini Dodoma na moja ya nafasi zitakazojazwa ni ya Mapuri. Mmoja wa watu wanaotajwa kujaza nafasi hiyo, ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam , Yusuph Makamba aliyeteuliwa wiki iliyopita kuwa mbunge.