Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Makamba asema CCM haina wanamtandao
Makamba asema CCM haina wanamtandao
By Habari Tanzania | Published  05/12/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

Na Yahya Charahani

SIKU moja baada ya Katibu Mstaafu wa CCM, Phillip Mangula, kuliambia gazeti hili kuwa makundi katika chama yanakikosesha uhai na kumtaka Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kuyakemea; Katibu Mkuu wa sasa, Yusufu Makamba, ameibuka na kusema kuwa hakuna makundi katika CCM.

Kauli ya Makamba inapingana na zile za wachunguzi wa masuala ya siasa ambao mara kadhaa wamesikika wakizungumzia kuendelea kuwepo kundi la wanamtandao, ambalo asili yake ilikuwa kumuunga mkono Rais Kikwete katika uteuzi wa kuwania nafasi hiyo kupitia CCM.

Makamba aliliambia gazeti hili kuwa; "Sikiliza bwana sisi hatuna makundi, kinachotokea ni kwamba wakati wa uchaguzi, watu hujipanga kimikakati na kwa maana hiyo ndiyo maana wakati mwingine kunakuwa na makundi fulani yanamuunga mkono mgombea fulani na mengine mgombea mwingine, lakini haya ni wakati wa uchaguzi tu na unapomalizika CCM imebakia kuwa moja."

Kundi la mtandao linaelezwa kuendelea kuwepo na taarifa za hivi karibuni zilizopatikana kabla ya mkutano wa saba wa Bunge uliofanyika mwezi uliopita, zilieleza kuwa kundi hilo sasa limegawanyika na kuwa mawili.

Tena kumekuwa na kauli za chini chini kutoka kwa wanachama wa CCM ambao wanalalamika kuhusu teuzi mbalimbali za nafasi za madaraka kufanywa kwa kutazama waliomo katika kundi hilo.

Wana CCM ambao walionekana kupingana nalo kwa sasa wanahaha kuhakikisha wanapata nguvu walau ya kuongoza katika chama kufuatia CCM kuwa na Uchaguzi Mkuu mwaka huu.

Uchunguzi zaidi unaonyesha wazi pia kuwa, kuna hali ngumu kwa wana CCM ambao hawakuwahi kuwemo katika mtandao kushinda uchaguzi. Hii inatokana na kuwepo pia nia ya kuhakikisha kuwa miongoni mwa viongozi kutoka katika mtandao, wanaandaliwa kwa ajili ya chaguzi zijazo.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwananchi nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam juzi, Mangula alisema kuwa na makundi wakati wa kampeni ni jambo la kawaida na linaruhusiwa, lakini makundi hayo yanatakiwa kuvunjwa mara baada ya kampeni.

Mangula alizungumza hayo baada ya kuulizwa kuhusu kundi la wanamtandao, lililokuwa likimpigia kampeni Rais Kikwete na ambalo hata baada ya uchaguzi kumalizika, limeendelea kuwapo na hata baada ya Rais kukemea kuendekeza makundi ndani ya chama, kundi ambalo limejipa nafasi ya pekee katika siasa za nchi.

“Wakati wa kampeni za kugombea uteuzi wa ndani wa CCM, makundi yanaruhusiwa, mgombea akipatikana tu, makundi yote ni lazima yavunjwe na libaki kundi moja, ikiwa kiongozi ataruhusu kuendelea kwa makundi ataleta mvurugano ndani ya chama,” alionya Mangula.

Mangula alisema kwa kawaida kutofautiana kimawazo si jambo baya katika siasa, lakini mawazo hayo yanapoendelea kutofautiana hata mnapofikia muafaka, si jambo zuri.

Mangula ambaye amekuwa Katibu Mkuu wa CCM kwa muda wa miaka kumi mfululizo (1996 – 2006) alisema CCM inafanikiwa kuwa chama kinachoongoza katika chaguzi mbalimbali zilizofanyika nchini kwa sababu ni chama chenye oganaizesheni nzuri na mtandao mpana.

Mangula alisema wakati akiwa Katibu Mkuu, amesimamia chaguzi ndogo 29 na kati ya hizo CCM imeshindwa katika majimbo mawili tu.

“Unajua ukishindwa unaumia sana, hivyo ilikuwa ni kazi yangu kama Katibu Mkuu kuweka mikakati ya ushindi kila unapotokea uchaguzi hata uwe mdogo kiasi gani. Mahali tunaposhindwa katika uchaguzi tunaliita kila tawi, kila kata, kila tarafa na uongozi wa wilaya na mkoa waeleze tumeshindwaje? Sisi kwa kweli hatutegemei sana jukwaa bali tunategemea oganaizesheni za ndani," alisema Mangula na kuongeza;

“Kiongozi hata awe mzuri jukwaani, lakini ikiwa chama chake hakina mikakati mizuri ya ushindi ni vigumu kushinda, kwani unapopanda jukwaani ni sawa na kuandika barua ‘kwa yeyote anayehusika’ hivyo si ajabu barua hiyo ikawafikia hata wasiohusika,” alisema.

Kuhusu kulinganishwa kwake na Katibu Mkuu aliyepo sasa, Yusuf Makamba ambapo chambuzi za masuala ya kisiasa ziliwahi kusema kuwa ‘viatu vya Mangula havimtoshi Makamba,’ Mangula alisema anaamini kwamba chama si mtu bali ni oganaizesheni iliyopo na pia hakuna mtu anayejenga uwezo kwa siku moja bali mtu anapopewa nafasi ya uongozi, anapaswa ajifunze.

“Si kweli kama mwaka 1996 nilipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama nilikuwa naelewa kila kitu katika chama, taratibu nimejifunza na baada ya miaka 10, kweli nimetoka nafahamu mambo mengi na pia nimekabiliana na changamoto nyingi, hasa nyakati za uchaguzi na hasa nikifahamu kuwa jukumu langu ni kuleta ushindi katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.”

Wakati huo huo, Makamba amesema CCM haishtushwi hata kidogo na muungano wa vyama vya siasa vya upinzani kwa kuwa hata sasa wamekuwa wakikabiliana navyo bila ya upinzani wowote.

Makamba alisema hana tatizo na muungano wa vyama hivyo kwa kuwa tu ni katika kuimarisha demokrasia ya vyama vingi ingawa hawawezi kuchukua madaraka.

"Sikilizeni nawaambia hawa wapinzani kama wanaungana ili kuimarisha demokrasia sawa, lakini kama wanaungana eti kuing'oa CCM wanajidanganya hawatuwezi, sababu tumekuwa tukikabiliana nao katika majukwaa mbalimbali na tumewashinda," alisema.

Alisema anachokijua ni kwamba CCM iko imara na imejiimarisha kiasi kikubwa na kwamba changamoto ambazo wanazipata sasa ndizo zinazowafanya waimarike zaidi na hawawezi kusumbuliwa na muungano kama huo.

"Hebu kumbukeni siku zote tumekuwa tukikabiliana nao, mfano mzuri jimbo la Tunduru ambapo vyama vitatu vya siasa vya CUF, TLP, na NCCR viliungana ili kumuunga mkono mgombea wa CUF ashinde, lakini nani alishinda?" alihoji.

Alisema CCM imefika hapo ilipo na itaendelea kuwa hivyo kwa sababu ya mshikamano na maelewano mazuri yaliyojengeka kihistoria tangu chama hicho kianze na ndiyo maana wameshinda na wataendelea kushinda.

"Wapinzani wakiungana sisi tunashikamana na katu hawawezi kutung'oa wataishia kuwa hivyo hivyo na walie tu," alisema.

Juzi vyama vinne vya upinzani nchini, vilitiliana saini vipengele 10 vya ushirikiano wa kisiasa katika nyanja mbalimbali, kuanzia ngazi za chini hadi taifa kwa lengo la kuunganisha nguvu katika kukabiliana na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hatua hiyo ilifikiwa ikiwa ni sehemu ya mchakato wa mikakati ya vyama hivyo ya kuelekea kuing’oa CCM madarakani katika chaguzi mbalimbali, ukiwamo uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji utakaofanyika mwaka 2009 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Utiaji saini huo ulifanyika katika ofisi za makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wakuu na baadhi ya wanachama wa vyama hivyo.

Vyama vilivyotia saini tamko juu ya ushirikiano huo, ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na Tanzania Labour Party (TLP).

Chadema iliwakilishwa katika utiaji saini katika tamko hilo na Katibu Mkuu wake, Dk Wilbroad Slaa wakati CUF iliwakilishwa na Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba.

NCCR-Mageuzi iliwakilishwa na Mwenyekiti wake, James Mbatia na TLP iliwakilishwa katika utiaji saini huo na Mwenyekiti wake, Augustine Mrema.

Viongozi wengine wa vyama hivyo walioshuhudia utiaji saini tamko hilo, ni pamoja na Katibu Mkuu wa CUF, Seif Shariff Hamad na manaibu wake Tanzania Bara na Zanzibar, Wilfred Lwakatare na Juma Duni Haji.

Wengine, ni Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Polisya Mwaiseje, Kaimu Naibu Katibu Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Vijana wa Chadema, John Mnyika na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Erasto Tumbo.

Katika tamko hilo lililosomwa na Mbatia katika sherehe hizo, vyama hivyo vimekubaliana kwamba vitashirikiana katika masuala yote ya kisiasa, ikiwa ni pamoja na kuwa na msimamo wa pamoja bungeni na katika vyombo vingine vya uwakilishi wa umma.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.