Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Waziri Diallo chupchupu kufa maji
Waziri Diallo chupchupu kufa maji
By Habari Tanzania | Published  05/12/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

Waandishi Wetu, Mwanza na Ukerewe

WAZIRI wa Maendeleo ya Mifugo na vigogo kadhaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali katika mikoa ya Mwanza na Kagera, jana walionja harufu ya kifo, baada ya kukaa kwa saa nzima katika ziwa Victoria wakining'inia kwenye maboya.

Mkasa huo ambao kila mmoja alizungumzia kwa namna yake, uliwapata viongozi hao baada ya boti walilopanda kwenda Ukerewe, kukumbwa na dhoruba na kuzama ziwani majira ya saa 4.30 jana asubuhi.

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Peter Toima Kiroya, aliyekuwa mmoja wa wahanga hao, alisimuliwa kwa huzuni namna walivyolazimika kukaa majini kwa saa moja wakisubiri kuokolewa na mitumbwi ya wavuvi iliyosambaa katika sehemu kubwa ya ziwa hlo.

"Tulikaa kwa muda mrefu kiasi kwamba tulikata tamaa ya kuokolewa. Kila mmoja alichoka kutokana na kushikilia boya kwa muda wote huo. kwa kweli tulikata tamaa ya kuishi," alisema Kiroya.

Mbali na Diallo na Kiroya, wengine waliokuwa katika boti hiyo iitwayo MV Mlinzi, mali ya Idara ya Maliasili ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Pius Ngeze,
Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Rajab Kundya na Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Mwanza, Simon Mangelepa.

Wengine walionusurika kufa maji katika ajali hiyo ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Ali Mambile na Mkurugenzi wa Hoteli ya Monarch, Oswald Mwizarubi, ambao wote walikuwa wakienda kuhudhuria mazishi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ukerewe, Edward China, aliyefariki dunia Mei 6.

Habari zinasema boti hiyo iliyoondoka Mwanza saa 2.00 asubuhi, ikiwa imebeba abiria kumi, ilikumbwa na dhoruba kali ziwani na baadaye kuzama, lakini watu wote waliokuwamo walifanikiwa kudaka maboya kujiokoa na kifo.

Habari za kutokea kwa ajali hiyo ziliutikisa mji wa Mwanza na vitongoji vyake mapema jana asubuhi na baadhi ya ndugu wa viongozi hao walianza kuhaha kufuatilia hatima ya ajali hiyo huku wengine wakitokwa na machozi.

Inaelezwa kwamba chanzo hasa cha meli hiyo kuzama ni dhoruba kubwa iliyolikumba ziwa hilo, dakika chache kabla boti hiyo haijafika Ukerewe.

Dhoruba hiyo ilisababisha boti kugonga kitu ambacho hadi sasa hakijajulikana iwapo ilikuwa ni chuma au mwamba uliosukumwa kwa nguvu ya dhoruba na kusababisha litoboke na kuanza kuingiza maji.

Wavuvi waliokuwa wakifanya kazi katika ziwa hiyo hatimaye walifanikiwa kuwaona viongozi hao na kuwaokoa kabla ya kuwakimbiza kwenye Hoteli ya Monarch ambako walipatiwa huduma ya kwanza kabla ya kukimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe.

Alipopigiwa simu muda mfupi baada ya ajali hiyo, Diallo alikiri kukumbwa na mkasa huo, lakini akamwomba mwandishi aliyempigia amwacha apumzike kwa kuwa alikuwa amechoka.

"Ni kweli tupemepata ajali. Kwa nini usimuulize Mkuu wa Wilaya?...naomba niache kwanza nipumzike utanitafuta baadaye," alisema Diallo kisha akakata simu.

Akisimulia mkasa huo, Mangelepa alisema kutokana na kukaa kwa muda mrefu ziwani, huku wakiwa wameshikilia maboya, wote walichoka sana na nusura Ngeze aachie boya kama si Diallo kuanza kuwapa moyo wenzake.

Mangelepa alisema hata Mbunge wa Viti Maalum, Maria Hewa, naye alichoka, lakini wote kwa pamoja walikuwa wakifarijiwa na Diallo aliyekuwa akiwasihi wasikate tamaa na waendelee kushikilia maboya yao hadi watakapookolewa.

Kwa upande wake, Kundya alisema kuna wakati walifikiria kuogelea kwa maboya kwa msaada wa nahodha wa boti iliyozama hadi katika Kisiwa cha Mabibi, lakini hawakuweza kutokana na uchovu waliokuwa nao.

Wakati huo huo, fedha za rambirambi kwa ajili ya msiba wa China
zilizokuwa zimetolewa na chama hicho ngazi ya taifa
zimezama majini kutokana na ajali hiyo.

Akizungumza jana wakati wa kutoa salamu za chama mwakilishi wa chama aliyeteuliwa kumwakilisha Katibu Mkuu, Yusufu Makamba, Pius Ngeze alisema Sh300,000 ambazo zilipaswa kutolewa katika msiba huo zimezama wakati wa ajali.

Ngeze alisema katika ajali hiyo, watu wote waliokuwemo ikiwa ni pamoja na nahodha wa boti iliyozama, Herman Lubala waliokolewa, lakini mizigo yao, ikiwa ni pamoja na simu za mkononi ilizama.

Hata hivyo, kutokana na ajali hiyo, ratiba ya maziko ililazimika kubadilika na viongozi hao wakatoa salamu zao za mwisho na kurejea Mwanza kwa kutumia meli ya MV Clalias.

Wakati huo huo, Mbunge wa Ukerewe, Gertrude Mongella amesema serikali inapaswa kufikiria uwezekano wa kujenga daraka katika eneo la Kisorya na Rugezi ili kupunguza ajali za mara kwa mara za mitumbwi na maboti zinazotokea katika Ziwa Victoria.

Pia aliiomba serikali kukitangaza kisiwa cha Ukerewe kama sehemu ya hatari kwa usafiri ili ipewe kipaumbele katika kufikiriwa kutatuliwa kwa tatizo hilo. 

Mongella alisema wakati viongozi hao wakipata ajali ziwani, wananchi na viongozi wengine ambao walikuwa wakija katika msiba huo pia walikwama kuvuka katika kivuko cha Rugezi kutokana na kivuko hicho kuharibika na wakalazimika kuvushwa kwa mitumbwi.

Alisema kwa miaka mingi, wakazi wa Ukerewe wamekuwa wakisumbuliwa na tatizo sugu la usafiri ambalo makali yake huongezeka zaidi pale meli zinazosafiri kati ya kisiwa hicho na maeneo mengine zinapokuwa mbovu.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Augustine Uromi,  alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, lakini akasema asingeweza kuwataja watu wote waliookolewa kwa majina kwa kuwa taarifa alizokuwa nazo zilikuwa bado hazitoshelezi.

“Tutatoa  taarifa baadaye kwa kuwa sasa bado tunafuatilia ila ni kweli tukio hilo lipo, waziri, Mkuu wa wilaya na Katibu wa CCM wa Mkoa na wenzao waliozama wote wameokolewa,” alisema


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by washawasha)
    Rating
    Safi kabisa na hii ndio itakayoboresha usafiri wa majini maana viongozi wetu wamejisahau na mapajero yao
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.