KUNA kila dalili za mgawanyiko katika Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dodoma, unaosababishwa na matendo ya ushoga na usagaji.
Hali hiyo imedhihirika hivi karibuni baada ya kikao cha siku moja kilichofanyika mjini humo kilichohusisha baadhi ya waumini wa kanisa hilo Kanda ya Kati, wanaopinga ushoga na usagaji kanisani humo.
Kikao hicho kiliitishwa kama moja ya mikakati ya kuandaa na kuitisha mkutano wa waumini wote wa kanisa hilo katika dayosisi hiyo, ili kuwatenga waumini wanaokwenda kinyume cha maadili ya kanisa.
Lakini, gazeti hili limeambiwa kuwa mlengwa mkubwa wa mikakati hiyo ni Askofu Mkuu wa Dayosisi hiyo, Godfrey Mhogolo, ambaye ameponzwa na kauli yake kuwa anawapenda mashoga kama vile Yesu alivyowapenda watenda dhambi.
Kauli hiyo imetafsiriwa na waumini wengi ndani ya kanisa hilo, wakiwamo viongozi wengine wa ngazi za juu, kuwa askofu huyo anatetea mashoga, kinyume cha msimamo wa kanisa hilo nchini.
Vyanzo kutoka ndani ya kanisa hilo katika Dayosisi ya Dodoma, vimeifahamisha Tanzania Daima kuwa Askofu Mhogola anakabiliwa na tuhuma nyingine za kulifanya kanisa hilo kama taasisi yake binafsi.
Akizungumza kwa huzuni, mmoja wa viongozi wa kanisa hilo, alieleza kuwa kiini cha mgawanyiko huo ni ushoga na udikteta katika maamuzi unaofanywa na Askofu Mhogolo.
Inadaiwa kuwa Askofu Mhogolo anakiuka taratibu na mara kadhaa amechukua maamuzi ya kuwafukuza viongozi wa juu wa kanisa hilo, akiwamo Askofu Msaidizi wake, Ainea Kusenha.
Pamoja na tuhuma hizo, askofu huyo anadaiwa kuwatishia baadhi ya waumini wanaopinga matendo yake, kwa kuwazuia kushiriki masuala yahusuyo kanisa na kuwanyima haki yao ya msingi kama waumini wa kanisa hilo.
Kadhalika, Askofu Mhogolo anadaiwa kumfukuza kikatili mwakilishi wa walei kutohudhuria kwenye kikao kikuu cha dayosisi hiyo, kilichoshirikisha viongozi na maaskofu.
Inaelezwa kuwa Askofu Mhogolo, aliwahi kutoa kauli inayolenga kuwatetea mashoga, wakati wa mkutano wa maaskofu wakuu wa Anglikana uliofanyika Februari mwaka huu jijini Dar es Salaam, kitendo kilichowaudhi waumini hao.
Aidha, hatua ya askofu huyo kumfukuza kinyume cha taratibu msaidizi wake, kutokana na kupingana naye kuhusu msimamo wa kukumbatia mashoga na wasagaji, kumeibua sura mpya miongoni mwa waumini wa kanisa hilo.
Inadaiwa pia Askofu Mhogolo aliwahi kukiri hadharani kuwa anawapenda na hatawabagua wasagaji na mashoga kwa kuwa wote ni wana wa Mungu na mara kadhaa amekuwa akisema anawapenda kama Yesu alivyowapenda wenye dhambi.
“Kinachowaudhi waumini wa Dodoma ni ukatili anaowafanyia baadhi ya viongozi na waumini wanaopingana na msimamo wake.
“Tumechoshwa naye, na katika mkutano wa kesho (leo) tumeandaa agenda 10, lakini tatu kati ya hizo zitahusu tabia mbovu ya Askofu Mhogolo na tutahakikisha tunamtoa madarakani.
“Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo tutamtaka Askofu Mkuu Donald Mtetemela awe mwenyekiti wa Sinodi (Kikao cha Wakristu wote) kitakachofanyika Julai 4 hadi 7 mwaka huu na yeye atakuwa mjumbe wa kawaida tu.
“Tutazungumzia pia ukaidi wa Askofu Mhogolo na amri ya Askofu Mkuu, Mtetemela ya kutomrudisha madarakani Msaidizi wake, Askofu Kusenha, aliyemfukuza bila sababu za msingi, kitendo kilichowakera waumini wengi.
“Waumini pia tutahoji sababu za Askofu Mhogolo, kumfukuza kikatili kwenye kikao kikuu cha dayosisi mwakilishi wa walei…aliwanyima haki ya kupata habari za maendeleo ya kanisa waumini wote,” kilisema chanzo hicho kwa njia ya simu.
Hata hivyo, msuguano katika kanisa hilo ni wa muda mrefu unaodaiwa kusababisha baadhi ya waamini kukosa uaminifu kwa viongozi wao.
Juhudi za kumpata Askofu Mhogolo kuzungumzia madai hayo hazikufanikiwa kwani kila mara simu yake ilipopigwa, ilikuwa haipatikani.