KUNDI la polisi waliojitambulisha kuwa ni wakuu wa vituo (OCS) nchini, limempelekea Rais Jakaya Kikwete, waraka unaofichua maovu yanayofanywa na baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa na viongozi wengine waandamizi katika Jeshi la Polisi.
Nakala ya waraka huo imepelekwa kwa Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu, na kwa vyombo vya habari.
Mwapachu jana alikiri kupokea waraka huo, na kusema kwamba anaufanyia kazi kwa kina.
Hata hivyo, hauelezi kama watuhumiwa hao ni wale waliokuwa ma-RPC, au ni hawa wapya ambao Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Said Mwema, kawateuwa hivi karibuni.
Ma-OCS hao wametoa tuhuma nyingi dhidi ya wakuu wao, wakisema wananyimwa fedha na vitendea kazi, na kutakiwa “watumie akili zao” kufanikisha kazi.
Waraka huo unasomeka hivi: “Mheshimiwa Rais, tunachukua nafasi hii adimu na nadra sana ambayo ni nje ya utaratibu wa Jeshi la Polisi kwa madhumuni maalumu ya kukupongeza kwa uamuzi wako thabiti wa kuamua kuunda wizara kamili na inayojitegemea ya Usalama wa Raia.
“Tukiwa askari polisi tulitegemea kwamba shida kubwa tuliyokuwa nayo askari wa vyeo vya chini na wakuu wa vituo, yaani OCS itapungua kama si kwisha kabisa, lakini cha ajabu shida ni kubwa sasa kuliko ilivyokuwa hapo awali.
“OCS tunaendesha vituo vya polisi na kambi wanazoishi askari kwa gharama zetu wenyewe. Tunatumia fedha zetu au kuomba kwa matajiri ili tuweze kufanikisha kazi kama vile kununulia vifaa vya ofisi, yaani stationery zote za kituo, kununua rangi na chokaa kwa ajili ya kupaka vituo vya polisi na nyumba za kuishi askari.
“Viongozi wetu, yaani makamanda wa polisi wa mikoa (RPC) na wakuu wa polisi wa wilaya (OCD) wanachotaka ni kuona kazi zinafanyika bila malalamiko. Ukiwaomba vitendea kazi unatishwa kwamba ‘hiyo nafasi utaipoteza sasa hivi' na kutakiwa tutumie akili kuendesha vituo.
“Makamanda hawa wanapata stationeries, fedha kwa ajili ya simu zao za mikononi, nyumbani na kila kitu kutoka serikalini. Yeye haambiwi ‘tumia akili'. Ukiwa na gari la kituo utajuta kwani unapewa lita 200 kwa mwezi mmoja na nusu au miwili. Yakiisha utaendelea kununua kwa ajili ya kufanikisha kazi, vinginevyo uelewe kwamba utakuwa matatani kama itatokea kazi au utaitwa na kiongozi halafu useme ‘sina mafuta ya gari'.
“Inapofika muda wa kulipeleka gari kwa ajili ya service maalumu, utalazimika kununua mafuta ya kwenda na kurudi na gharama za matengenezo. Ukisema huna uwezo wa kufanya hivyo, unaweza kunyang'anywa wadhifa huo au gari.
“Mheshimiwa Rais, Kamanda wa Polisi wa Mkoa anapanga ratiba ya kufanya ukaguzi wa vituo vyote vya polisi na majengo wanayoishi askari polisi. Anakuta vituo vimepakwa rangi pamoja na nyumba wanazoishi, lakini haulizi njia iliyotumika kupaka rangi vituo hivyo.
“Wakati wa ukaguzi huo, wakuu wa vituo wanabeba majukumu mazito sana . RPC pamoja na timu yake ya ukaguzi, wanatakiwa kwa muda wote watakapokuwa eneo lako wapate chai asubuhi, chakula cha mchana, cha jioni pamoja na malazi kama watalala. Wakiondoka baada ya ukaguzi OCS anajikuta ana mzigo wa madeni yaliyotokana na ugeni huo. Utafanyaje ulipe madeni hayo jibu ni ‘tumia akili'.
“Tatizo jingine ni kuhusu simu za vituo. Simu zote za vituo zimefungwa kwenda nje ya mkoa. OCS anapopata tatizo linalohitaji mawasiliano na kituo chochote nje ya mkoa, inambidi atumie simu yake ya mkononi.
“Kana kwamba haitoshi, Katibu muhtasi wa RPC yaani PS anakupigia simu kwamba umpigie kamanda simu kwani anahitaji kuzungumza nawe. Utatekeleza amri hiyo kwa kutumia simu yako ya mkononi. Bila kuona huruma kwamba unatumia simu na fedha zako, RPC ataongea kwa muda mrefu akikupa maelekezo aliyokusudia.
“Mheshimiwa Rais, Kamanda huyo huyo anatumia magari yasiyopungua matatu kwa ajili ya shughuli za kikazi na binafsi. Hanunui mafuta ya magari hayo, hanunui vocha ya simu ya mkononi, hatengenezi magari hayo kwa fedha zake, bali ni fedha za serikali. Hata kulisha mahabusu walio ndani ya Lock-Up kuanzia chakula cha mchana na jioni hilo ni jukumu la OCS na askari wanaopangwa CRO.
“Kamanda wa polisi anapopata uhamisho, stahili ya malipo yake analipwa yote. Askari wa vyeo vya chini hawalipwi hata robo, bali wanaamriwa watekeleze amri ya kuhama haraka, la sivyo washitakiwe. Malipo yako ya unakotokea na ukakokwenda, utalipwa akipenda labda umkute kamanda anayejali ubinadamu na mwenye huruma.
“Mheshimiwa Rais, shuhudia uroho na ubinafsi wa baadhi ya viongozi hawa pale watakapobaini kwamba kuna magari, mitambo, na pikipiki zilizopo vituoni ambazo hazina mwenyewe. Watajaza Inventory kwa bei ndogo na kujiuzia wenyewe. Kibaya zaidi, wanawasahau askari wao ambao ndio waliofanikisha ukamataji wa mali na vitu hivyo.
“Pengine Mheshimiwa Rais, tumalize waraka huu kwako kwa kukuthibitishia kwamba wakuu wa vituo na askari wao, wamebeba msalaba ambao uzito wake haupimiki.
“Tunakuomba ututoe motoni. Tunaamini serikali yako itatuongezea mishahara (ambayo tunaamini na makamanda nao wataongezewa), lakini kama viongozi wetu hawataacha tabia ya kutoa amri za kiutendaji bila vitendea kazi, au kama hawataacha kutamka kwamba “tumia akili”, mapambano dhidi ya rushwa katika Jeshi la Polisi yatakuwa sawa na kutwanga maji kwenye kinu.
“Tunaamini kwa Ari mpya, Kasi mpya na Nguvu mpya, mabadiliko yanawezekana.”
Waraka huo hauonyeshi ma-OCS hao waliketi wapi na kuamua kuuandaa kwa ajili ya kumpelekea Rais Kikwete.