KAMPUNI ya utalii ya Nomad Tanzania, yenye makao yake makuu Usa-River wilayani Arumeru, mkoani Arusha, imepongezwa kwa kuwa mstari wa mbele kutangaza nje ya nchi vivutio vya utalii nchini.
Balozi mstaafu, Jenerali Mirisho Sarakikya, alitoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki na kusena kuwa hatua hiyo inasaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini na hivyo kuongeza pato kutokana na sekta hiyo.
Alitoa pongezi hizo wakati wa ufunguzi wa jengo la kampuni hiyo katika mji mdogo wa Usa River.
Alisema kuwa kampuni hiyo iliyoanzishwa mwaka 2003, hivi karibuni imechangia sh milioni 140 kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika vijiji viwili wilayani Ngorongoro, pia imeweza kulipa sh bilioni nne kama kodi ya mapato kwa serikali.
Alisema kuwa taifa linahitaji fedha nyingi za kigeni, hivyo juhudi zinazofanywa na kampuni hiyo za kuitangaza nchi, zinapaswa kuungwa mkono na kuigwa na kampuni nyingine za utalii.
“Kampuni hii imekuwa na mchango mkubwa kwa taifa na jamii kutokana na mchango wake wa uchumi kwa kulipa kodi ya serikali bila ya matatizo,” alisema.
Awali, mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, John Corsre, alisema kuwa lengo la kampuni hiyo ni kuendelea kuitangaza Tanzania nje, kuwa ni nchi yenye vivutio vingi vya utalii ambavyo havipatikani sehemu nyingine ulimwenguni.
“Tunayo furaha kuwa sehemu ya nguvu za msukumo wa pamoja wa sekta ya utalii katika kusaka masoko nje ya nchi,” alisema.