MAOFISA afya wa Manispaa ya Dodoma, wameteketeza nyama zilizokuwa zinauzwa katika mabucha mawili, katika eneo la Chang'ombe mjini hapa, baada ya wamiliki wa maduka hayo kuyafungua na kuanza kufanya biashara pasipo kukidhi kanuni za afya.
Taarifa kutoka Ofisi ya Afya Manispaa ya Dodoma ilieleza kuwa wafanyabiashara hao walikutwa wakiuza nyama zao katika mazingira machafu.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kutokana na wafanyabiashara hao kukiuka sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003 kwa kuuza chakula katika mazingira machafu, walitakiwa kuteketezewa nyama waliyokuwa wanauza.
Kabla ya kuteketezwa kwa nyama hiyo, walitakiwa kujaza fomu maalumu ambayo inaonyesha kuwa walikiri kosa na kukubali nyama kuteketezwa na maofisa afya hao.
Nyama hiyo kilo 33, iliteketezwa kwa kuzikwa ardhini chini ya uangalizi wa maofisa afya na viongozi wa Mtaa wa Chamwino.
Wafanyabiashara hao wamepewa onyo kali kutokana na kuwa hilo ni kosa lao la kwanza na kutakiwa kuripoti polisi kwa muda wa siku tatu kuanzia jana, wakati uchunguzi unafanyika kubaini iwapo nyama ambayo walikuwa wameiuza ilileta madhara yoyote kwa walaji.
Hiyo ni moja ya hatua zinazochukuliwa na idara ya afya mkoani humu kufuatia kuzuka kwa homa ya Bonde la Ufa (RVF).